jaridahuru

Mitandao

SIASA: PIGO KUBWA CHADEMA, VIGOGO WATATU WAACHIA NGAZI, WADAI WAMECHOSHWA NA UBABE WA VIONGOZI

 



VIONGOZI watatu wa juu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani Kigoma, wamejiuzulu nafasi na uanachama wao kwa madai ya ubabe wa viongozi wa chama hicho kitaifa.

Waliojiuzulu ni Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wazee taifa, Jafari Kasisiko, Katibu wa chama hicho Mkoa wa Kigoma, Msafiri Wamalwa na Katibu wa Baraza la Wanawake mkoani hapa, Malunga Simba.

Akitangaza uamuzi huo kwa niaba ya wenzake mbele ya waandishi wa habari mkoani hapa jana, Kasisiko alisema wameamua hivyo baada ya kuona CHADEMA imepoteza sifa ya kuwa chama cha kidemokrasia.

“Sifa kubwa ambayo ilikuwa imetufanya tuendelee kubakia CHADEMA ni kwamba kilikuwa bado kinaendelea na sifa ya kuwa chama cha kidemokrasia, lakini baada ya kufikia hatua sasa kwamba kimeanza kuwa chama cha kibabe zaidi na kuanza kukiuka misingi ya demokrasia, kwa kweli sina sababu na wenzangu ya kuendelea kubaki katika chama hiki,” alisema.

Kasisiko aliyejiondoa kwenye Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka 1985 na kukaa nje ya siasa kwa muda kabla ya kujiunga CHADEMA mwaka 1994, alitoa mfano unaoonyesha chama hicho kukiuka misingi ya demokrasia kuwa ni suala la aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe aliyevuliwa wadhifa wake baada ya kutangaza nia ya kugombea nafasi za juu ndani ya chama.

“Zitto kosa lake ni kuonyesha nia ya kutaka kugombea uenyekiti wa CHADEMA. Lakini ukipitia Katiba ya CHADEMA tangu ukurasa wa kwanza mpaka wa mwisho, hupati mahala panaposema ni kosa mtu kutamani kugombea nafasi yoyote ndani ya chama.

“Kikubwa zaidi tayari Zitto alikuwa na watu wanaoumuunga mkono, mimi nikiwa mmoja wao basi hili lilionekana ni dhambi kubwa sana.

“Kwa hiyo katika CHADEMA tulikuja kugundua kwamba kumbe uenyekiti sasa hivi, ukiacha uenyekiti wa zama za Mtei, za Makani, chini ya Mbowe ni kitu nyeti ambacho hatakiwi mtu mwingine kugusa.

“Kwa hiyo kitendo hicho kwetu sisi kilionyesha wazi kuwa CHADEMA wamefikia mahala sasa hawapo tayari kufuata taratibu za kidemokrasia,” alisema.

Wamalwa alisema kwa ridhaa yake bila kushawishiwa na mtu ameamua kuondoka CHADEMA, na kwamba kabla ya uamuzi huo alikaa chini na kutafakari, wakati Malunga alisema ameamua kutoka kwa sababu ni chama kisicho na faida na wananchi.

Baada ya kujiuzulu uongozi na uanachama wa CHADEMA, Kasisiko alisema anajiunga na chama kipya cha siasa cha Allience for Change and Transparency (ACT) huku wenzake wakisema hawajajua watajiunga na chama gani.

Related

Siasa 8555656130564370536

Post a Comment

emo-but-icon

Wadhamini

UJUMBE

JH Katika Facebook

Nyayo zetu twitter

Za Juu

Mitandao

Piga Kura

Je ungependa Tanzania iwe na serikali ngapi?
  
pollcode.com free polls 

ADVERTISEMENTS

Msimamo wa ligi mbalimbali

Football results provided by whatsthescore.com

Mechi Live

Walioko Hewani Kwa Sasa

item