https://jaridahuru.blogspot.com/2014/07/siasa-mambo-yazidi-kufunuka-ukweli.html
Dar es Salaam. Uongozi wa Yanga umesema Mwenyekiti wa Kamati ya
ujezi wa jengo la Mafia, Ridhiwani Kikwete siyo mwanachama wa klabu hiyo
kwa kuwa hajalipa ada yake kwa miezi sita mfululizo.
Katika taarifa yake iliyotolewa jana kwa vyombo
vya habari na kusainiwa na Msemaji wa Yanga, Baraka Kizuguto ilieleza
kitendo cha Ridhiwani kupinga hatua ya Wajumbe wa Bodi ya Udhamini na
wanachama wa Yanga kwa pamoja kumuongezea muda wa mwaka mmoja,
mwenyekiti wao, Yusuf Manji hayana uzito kwa kuwa siyo mwanachama.
“Ridhwani Kikwete hajalipa ada zake za uanachama
kwa miezi zaidi ya 6 mfululizo na kwa mujibu wa Katiba ya Yanga ibara ya
13 kipengele cha pili ambacho kinasema kuwa endapo mwanachama hajalipa
ada yake kwa muda wa zaidi ya miezi sita mfululizo atakuwa amekoma kuwa
mwanachama wa Yanga.”
“Maoni aliyoyatoa hayana uzito wa mwanachama wa
Yanga, labda alikuwa akitimiza haki yake ya kutoa maoni kwa mujibu wa
katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tunaamini kama angekuwa ni
Mwanachama hai wa Yanga angetoa maoni yake kwenye Mkutano wa dharura wa
Wanachama uliofanyika Juni Mosi. Pia angeweza kutoa kwenye kitabu cha
maoni ya kupinga maazimio ya Mkutano huo kilichowekwa hapa klabuni
kuanzia Juni 23 hadi 27, hakuna aliyesaini zaidi ya mwenyekiti, Manji.
“Niwakumbushe wanachama wa Yanga sehemu ya
kuchangia maoni yao ni kwenye vikao vya Wanachama na siyo kwenye vyombo
vya habari, wasitafute umaarufu kwa njia za kubomoa kuliko kujenga wala
wasiwadhalilishe waliojitosa kwa hali na mali kuisaidia Yanga kuwa bora
kama Mama Fatma Karume wenye historia ndefu Yanga, tunaona ni sawa na
udhalilishaji kwake, kwa kweli inasikitisha sana.
Taarifa hiyo ya Yanga imekuja ikiwa ni siku moja
baadaya Ridhiwani kukaririwa na gazeti hili akisema haridhishwi na mambo
ya migogoro ya kikatiba yanayoendelea ndani ya Yanga.