SIASA: SIRI KUBWA YAFICHUKA CCM, LOWASSA AIBUKIA NDANI ACT YA ZITTO KABWE, KUMBE NDIYE MFADHILI WA ACT

https://jaridahuru.blogspot.com/2014/07/siasa-siri-kubwa-yafichuka-ccm-lowassa.html
IMEGUNDULIKA kwamba Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa (CCM) ndiye
mfadhili mkuu na mpanga mikakati mkuu wa kundi linalomfuata Mbunge wa
Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), ambalo limeanzisha chama kipya
cha siasa, Allaince for Change and Transparency (ACT-Tanzania).
Kwa wiki kadhaa za hivi karibuni, makundi ya wanachama, washauri na
wapanga mikakati wa Lowassa na Zitto wamekuwa wakikutana katika maeneo
kadhaa jijini Dar es Salaam na kupeana mbinu, lengo kuu likiwa ni jinsi
ya kumega Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika mapande ili
kidhoofike kabla ya uchaguzi mkuu 2015.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya habari, Lowassa amejiaminisha kwamba
ndiye atakayekuwa mgombea urais kupitia CCM. Kazi kubwa anayoona mbele
yake ni kuanza mapema kusambaratisha CHADEMA ili kupunguza upinzani
wakati wa kampeni utakapofika.
Zitto naye, ambaye uanachama wake kwa CHADEMA umebaki kwenye
makaratasi tu, anatajwa kuwa ndiye mwasisi mwenza wa ACT, na amekuwa na
uhusiano wa “kikazi” na Lowassa, hata kabla hajaingia kwenye matata ya
wazi na chama chake, ambacho mwishoni mwa mwaka jana kilimvua vyeo vyake
vyote vya uteuzi ndani ya CHADEMA kwa tuhuma mbalimbali.
Katika hatua mojawapo, chanzo kimoja kilicho karibu na Lowassa
kimesema kwamba mapema mwaka juzi, Zitto alimwendea Lowassa na kumwambia
kuwa mustakabali wake kisiasa ndani ya CHADEMA si mzuri, na kwamba
alikuwa tayari kumsaidia Lowassa kufanikisha malengo yake, lakini kwa
sharti kwamba iwapo mbunge huyo wa Monduli atafanikiwa kupata urais,
basi amteue kuwa Waziri Mkuu.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, kauli hiyo kwanza ilimstua Lowassa kwa
sababu ilimuonesha Zitto kama kiongozi asiye mwaminifu, ambaye yupo
tayari kufanya hujuma dhidi ya chama chake, jambo ambalo lilimfanya
Lowassa atilie shaka lengo la ombi hilo.
Jambo la pili lililomshtua Lowassa ni cheo kilichopendekezwa na
Zitto, maana kwa mujibu wa Katiba ya sasa, Waziri Mkuu lazima atokane na
wabunge wa majimbo, na awe kwenye chama chenye wabunge wengi.
Kwa kuwa hoja hiyo ilitolewa katika mazingira ya Katiba ya sasa, na
kwa kuwa haikujulikana wakati ule kama Zitto alikuwa bado ni mwanachama
na kiongozi wa CHADEMA, Lowassa hakuipata nafasi kauli hiyo, lakini
amekuwa anaitumia kujadili sura halisi ya Zitto.
Hata hivyo, taarifa zinasema uhusiano wao umeimarika baada ya Zitto
kuchukuliwa hatua na CHADEMA, huku wapambe wa Lowassa wakipita huku na
kule kusambaza propaganda kuwa CHADEMA bila Zitto inakufa.
Taarifa ambazo hazijathibitishwa zinasema Zitto anatarajiwa kujiunga
rasmi na ACT mwanzoni mwa mwezi Septemba mwaka huu, na timu ya Lowassa
imedhamiria kumfadhili ili kujenga taswira ya mpasuko ndani ya CHADEMA,
na kuipa CHADEMA mpinzani mpya ambaye ataifanya ishindwe kumfuatilia na
kumshambulia Lowassa.
Katika kikao cha mwisho kilichofanyika kati ya timu ya Lowassa na
“Vijana wa Zitto” kilijumuisha baadhi ya wapambe wakuu wa Lowassa wenye
kauli ndani ya Umoja wa Vijana wa CCM, watu wa karibu kifamilia na
Lowassa na washauri wa karibu wa Zitto, akiwamo Mhadhiri mmoja wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam.
Ajenda zao nje nje
Moja ya ajenda zao kuu ni kufadhili na kupandikiza watu ndani ya
mfumo wa CHADEMA ambacho kinaendelea na uchaguzi wa ndani, ili wapate
nafasi za uongozi, wazitumie kupata taarifa na mipango ya chama, na
baadaye wajivue nafasi hizo na kukimbilia ACT, na kuleta msisimko wa
kitaifa.
Gazeti hili lina taarifa kutoka kwa baadhi ya viongozi wa sasa wa
CHADEMA ambao “Vijana wa Zitto” wamekuwa wakiwapigia simu na wakati
mwingine kuwatembelea na kuwashawishi ahadi ya fedha na vyeo ili
wajiondoe CHADEMA.
Baadhi hao ni viongozi wa majimbo na mikoa ambao katika uchaguzi
unaoendelea ndani ya chama hawana uhakika wa kuchaguliwa kutokana na
upinzani mkubwa unaojitokeza baada ya chama kukua na kuvutia wasomi na
wafanyabaishara wenye mvuto katika maneo yao.
Baadhi ya viongozi walioendewa au kupigwa simu wamechukua tahadhari, na wametoa taarifa panapohusika ndani na nje ya chama.
Mbinu mojawapo ambayo imekuwa inatumiwa na “Vijana wa Zitto” kujaribu
kuvunja ngome za CHADEMA ni kuwatangazia viongozi hao kwamba ipo idadi
kubwa ya wabunge wa CHADEMA wanaotarajia kujiunga na ACT. Wanawataja
majina kama njia ya kujenga ushawishi.
Hata hivyo, baadhi ya viongozi hao wameliambia gazeti hili kuwa
wanajua hizo ni mbinu za kipropaganda. Na baadhi ya wabunge wanaotajwa
wamesema hizo ni mbinu za Zitto kutaka kuwagombanisha na chama chao na
kujitafutia njia mpya kwa kutumia majina yao.
Mmoja wao alisema, “Zitto mwenyewe ameshalikoroga. Sasa hii ni tabia
ya kututaja baadhi yetu, mimi na wenzangu kadhaa tumeshasikia, ni ile
ile roho mbaya ya tukose wote. Kwa kuwa yeye amekosana na chama,
anatafuta watu wa kufa naye.”
Mbali na kupandikiza wagombea nafasi za uongozi na kuvizia viongozi
wanaoogopa joto la uchaguzi ndani ya chama, wamekuwa pia na mbinu ya
kushawishi baadhi ya “wagombea watarajiwa” katika baadhi ya majimbo,
wanaotajwa kuweka nia ya kugombea nafasi za uongozi kupitia CHADEMA.
Makada kadhaa kutoka maeneo mbalimbali ya nchi wamezungumza na gazeti
hili na kutumia kauli zijazofanana. Kwa mfano, makada sita walioweka
nia ya kugombea ubunge katika majimbo kadhaa ya kanda ya Ziwa Mashariki
na Magharibi, wamekiri kwamba kila wanapojadili mkakati huu na “Vijana
wa Zitto,” kila mmoja wa nafasi yake anapewa ahadi ya kupewa pesa zote
za kufanyia kampeni.
Vile vile, baadhi yao wamesema kuwa wanaambiwa kwamba iwapo
watakubaliana na mpango huo wa ACT, moja kwa moja watakuwa wamepitishwa,
maana chama hicho hakina mpango wa kupata wagombea kwa kutumia kura za
maoni.
Taarifa zinasema sehemu ya malengo ya vikao ya Zitto na Lowassa ni kutafuta pesa kwa ajili ya mradi huu.
Zipo taarifa zisizothibitishwa kwamba mwezi uliopita Lowassa
aliambatana na Zitto katika ziara ya kimya kimya ya Mkoa mmoja wa kanda
ya Ziwa ambako anasemekana anataka kujenga ngome nzito ya ACT.
“Ninachojua ni kwamba iwapo ACT itafanikiwa kupunguza makali ya
CHADEMA, Mzee atapita kirahisi, maana kikwazo kikubwa alichonacho hadi
sasa hakipo ndani ya CCM, bali CHADEMA,” alisema mtoa taarifa wetu aliye
karibu na Lowassa, ambaye hakutaka kuthibitisha kama wawili hao
walisafiri pamoja kwenda Kanda ya Ziwa.
Mkono mrefu wa CCM ndani ya ACT
Mbali na ufadhili wa Lowassa, imebainika pia kwamba makada wengi wa
CCM wamewekeza raslimali zao katika kuinua ACT na kudidimiza CHADEMA.
Uchunguzi wetu umeonyesha kuwa mbali na Dk. Kitila Mkumbo na Samson
Mwigamba, mmoja wanaoratibu kazi ya Zitto ni kada wa CCM, ambaye ni
mdogo wa mmoja wa mawaziri waliojiuzulu katika sakata la Operesheni
Tokomeza, anayetokea kanda ya Kusini.
Wengine wanaotuhumiwa kujihusisha na mradi huu wa Tokomeza CHADEMA ni
Naibu Waziri mmoja ambaye ni bingwa wa propaganda za CCM, na ambaye
amewahi kutangaza hadharani kuwa ifikapo 2015 CHADEMA kitakuwa kimekufa.
Wamo pia wabunge na viongozi kadhaa waandamizi wa CCM, ambao licha ya
kwamba hawamuungi mkono Lowassa, wanafurahia msukosuko wowote
utakaokipata CHADEMA kuelekea 2015.
Mwingine ambaye anadaiwa kufadhili ACT ni mtoto wa kigogo, ambaye
katika miaka ya karibuni ameingia kwenye kashfa nyingi, kabla ya kukwaa
ubunge hivi karibuni.
Madiwani waliohama waomba radhi warejeshwe
Wakati huo huo, madiwani wawili waliohamia CCM kutoka CHADEMA, katika
kata za Ngokolo na Masekelo, Shinyanga, Sebastian Peter na Zacharia
Machafuko, wameibuka na kusema wanajutia uamuzi wao, na sasa wanafanya
jitihada za kuomba warejeshewe uanachama wa CHADEMA baada ya kukerwa na
hila za CCM na ACT.
Madiwani hao wanadai kuwa walihamia CCM kwa muda kwani waliambiwa
kuwa ACT kitakapokuwa kimepata usajili wa kudumu wangejiunga nacho ili
kuimarisha upinzani nchini.
Madiwani hao walijiunga na CCM Februari mwaka huu na kupokelewa na
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nauye. Baadaye, Katibu Mkuu wa
CHADEMA, Dk Wilbroad Slaa alikituhumu CCM kwa mchezo mchafu.
“Tukishawishiwa kuhamia CCM kwa muda kwa lengo la kuhamia ACT ili
kikipata usajili wa kudumu tuhamie huko pamoja na baadhi ya wanachama wa
CCM.
“Tuliambiwa tufanye siasa za harakati, lakini tulichobaini ni kuwa
tangu tukubali mawazo hayo ya viongozi wa ACT tukijua tunaimarisha
upinzani imekuwa tofauti. Mkakati huo ulianza kuratibiwa na Mwenyekiti
wa UVCCM, Abbakari Gulam ambaye ni mtoto wa Meya wa Shinyanga, wakiwa na
Habib Mchange, kisha tuliona mkakati unatekelezwa na mbunge wa
Shinyanga mjini, Stephen Masele, Nape Nauye, Januari Makamba, Mwigulu
Nchemba na Ridhiwani Kikwete,” walisema katika taarifa yao mbele ya
waandishi wa habari jijini Mwanza.
Wakisimulia mkakati huo walisema walifikishwa Tinde na kiongozi huyo
wa UVCCM kisha wakiwa huko walipigiwa simu na Stephen Masele na
kuzungumza Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA aliyewahakikishia kuwa baada ya
kuondoka CHADEMA watajiunga na ACT ili iwawezeshe kupata nafasi za
uongozi wa kitaifa katika chama hicho kipya, pamoja na kupatiwa kitita
kikubwa cha fedha.
Chanzo chetu cha habari kutoka Shinyanga kimeelezwa kuwa baada ya
kuhamia walipatiwa kiasi kikubwa cha pesa bandia, na katika kitita hicho
waliambulia laki mbili ndio zilikuwa halali, pesa hizo zimetajwa kuwa
zilikuwa ziwe milioni kumi na mbili lakini bada ya kuhesabu zilipatikana
halali laki mbili tu, na zinadaiwa kutolewana na msaidizi wa Masele
akiwa na Mchange katika hoteli ya Karena iliyopo Shinyanga, kabla ya
madiwani hao kuondolewa na gari hadi Mwanza na kusafiri kwa ndege hadi
Dar es Salaam kwa maelekezo ya Nape.
Tamko hilo linaongeza kuwa “kwa kipindi chote cha kudanganywa
tulidhani Zitto anaonewa, hivyo tukaamua kujiunga na Chama chake ambacho
alituhakikishia lakini tumebani kuwa ACT na CCM hawana tofauti,
mikakati inatengenezwa na ACT ila watekelezaji ni CCM, baada ya kubaini
ghiliba hizi tumeshindwa tumetafakari kuwa hata barua zetu tuliandika
zikiwa na makosa ya kikanuni hivyo sasa tumemwandikia tena Meya
kumuuliza ni kwanini hajatualika kwenye vikao viwili kwa kuwa tulikuwa
hatujajiuzulu kisheria.
“Ili mtu kujiuzulu udiwani, kanuni zinasema kuwa diwani anaandika
barua kwa Meya, unaambatanisha na kitambulisho cha udiwani, na hati ya
ushindi ya udiwani ambayo hatujawapa wala vitambulisho vyetu,
tulichokifanya ni kama kuandikiana barua za kawaida tu, na mtu kutangaza
kujiunga na Chama kiingine bila kuchukua kadi yao sisi sio wanachama
wao na kwa kuwa Chama chetu hakijachukua hatua zozote dhidi yetu basi
tunarejea kwetu upinzani kushindana na CCM,” alisema Sebastian mbele ya
waandishi wa habari.
Walisema CCM na ACT waendelee na kamari zao kuhadaa watanzania,
“jamaa hao wana umakini kidogo ndio maana hawakubaliani kuwa bado
hatujajiuzulu kisheria wakakimbilia kutupeleka jukwaani kushangilia,
sasa sisi tunarudi kutumikia wananchi wetu kwani hatujavunja sheria,
hatukukiuka kanuni za kujiuzulu furaha ya CCM na ACT ni ya muda tu,
tulionda huko tumewabaini.
Kufuatia hali hiyo,madiwani hao waliandika kuwa “tunapenda kuomba
radhi viongozi wote wa CHADEMA, wanachama na watanzania wote watusamehe,
watupokee tukapambane kufanya kazi ya siasa za upinzani wa kweli kuleta
ukombozi wa kweli kwa nchi yetu, tulichokiona huku tumekijua,
tunawatahahadharisha wengine wakionga inafaa wajiunge huko kwa hasara
yao ya maisha yao kisiasa na kufanya kazi ya kujenga CCM.”
Mkakati huu unaratibiwa na mmoja wa wabunge wa upinzani mwenye
mahusiano ya karibu na viongozi wa CCM na serikali anayedaiwa hadi sasa
kuifadhili ACT mabilioni ya shilingi kwa ajili ya kujiimarisha mikoani
kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu.
Kazi ya wanazi wa ACT waliofukuzwa CHADEMA
Kwa sehemu kubwa, imebainika pia kwamba nguzo kuu za ACT ni makada wa
zamani wa CHADEMA ambao kwa sababu kadhaa walipata misukosuko ndani ya
chama hicho na kuchukuliwa hatua kali au kufukuzwa katika maeneo kadhaa
ya nchi.
“Sisi hapa Mwanza tunatambua fika kwamba. Meya Henry Matata, Diwani
Adam Chagulani wa Igoma, na Mushumbusi ndio vinara wa ACT wanaotumika
kujaribu kusambaza ACT kanda ya Ziwa, na kujaribu kupenya na kubomoa
ngome ya CHADEMA. Kwa sasa hata Habib Mchange wa Pwani, yupo Mwanza
anaratibu mipango ya uzinduzi wa chama chao utakaofanyika mapema mwezi
ujao.
“Lakini hapa kuna ukweli ambao haupingiki, kwamba watu hawa
walishafukuzwa CHADEMA, na sasa wanafanya siasa za chuki na visasi,
wakiajribu kurubuni wanaCHADEMA. Pili, ni ukweli kwamba CHADEMA ni imara
kuliko wanavyodhani. Haiwezi kubomolewa na wanachama wake wa zamani
waliaoamua kuwekeza katika Siasa za usaliti. Hata huko waendako
watasalitiana tu,” alisema kada mmoja wa CHADEMA mkazi wa Mwanza, ambaye
hakutaka kutajwa jina kwa kuwa si msemaji.
Alipotafutwa John Nchimbi kwa simu alisema jina lake litakuwa
linachanganywa kwani yeye hajishughulishi na siasa bali ni mdau wa
michezo ambaye historia yake iko Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF), huku Dk. Kitila naye akikana kushiriki mpango wowote wa kuhujumu
CHADEMA.
Alisema kuwa yeye ni mwanataaluma ambaye hajihusishi na siasa za
vyama na kwamba kama wako viongozi wa CHADEMA wanarubuniwa na kukubali
badi chama kinapaswa kujiuliza walipataje uongozi.
Fred Lowassa, Mwigulu Nchemba, Nape Nnauye, Mshumbusi simu zao ziliita bila kupokelewa.