KATIBA: UKAWA WATOA MPYA, WAKWEPA JITIHADA ZOTE ZA USULUHISHI WASEMA HAWARUDI BUNGENI KUJADILI KATIBA YA CCM

https://jaridahuru.blogspot.com/2014/08/katiba-ukawa-watoa-mpya-wakwepa.html
MCHAKATO wa katiba mpya umefikia hatua ngumu zaidi kuliko
ilivyotarajiwa baada ya wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA)
kutangaza rasmi kutoshiriki vikao vya maridhiano na mikutano ya Bunge
Maalum.
Kwa takribani miezi miwili sasa kulikuwa na jitihada za kuwashawishi
wajumbe hao kurejea bungeni baada ya kususia vikao kwa madai ya
kuchoshwa na lugha za ubaguzi, matusi, kejeli na kusiginwa kwa rasimu
iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Msimamo huo wa UKAWA sasa unaonyesha dhahiri huenda mchakato wa
katiba ukakwama licha ya Mwenyekiti wa Bunge Maalum, Samuel Sitta
kutangaza litaanza vikao vyake keshokutwa.
Kukwama kwa mchakato huo kunatokana na ukweli kuwa ili vifungu vya
rasimu vipitishwe ndani ya Bunge, vitahitaji theluthi mbili ya wajumbe
wote kutoka Tanzania Bara na idadi hiyo hiyo kutoka Zanzibar.
Inasadikika kuwa bila ya ushiriki wa wajumbe wa CUF kutoka Zanzibar
waliomo kwenye UKAWA, theluthi mbili haitopatikana wakati wa kupiga
kura.
Kutokana na jambo hilo, zipo taarifa baadhi ya vigogo wa CCM na
serikali wanadaiwa kushiriki kwenye vitendo vya kuwarubuni, ikiwemo
kuwapa fedha wajumbe wa CUF walio UKAWA wakiuke msimamo wa kundi lao na
waingie bungeni.
UKAWA wanena
Wakizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam,
viongozi na wajumbe wa UKAWA, walisema hawataendelea kushiriki
mazungumzo na CCM wala kuhudhuria vikao vya Bunge Maalum.
Wajumbe hao walisema kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya kutafakari na
kuona kuwa tiba ya kuzaa katiba haijapatikana baada ya mazungumzo ya
maridhiano ya kikao cha nne kilichoitishwa na Msajili wa Vyama vya
Siasa, Jaji Francis Mutungi.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam kwa niaba ya wenyeviti wenza wa
UKAWA, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),
Freeman Mbowe, alisema mazungumzo yaliyoratibiwa na Jaji Mutungi hayana
faida kutokana na CCM kuendelea kudai matakwa yao na si muafaka.
Mbowe alisema ushiriki wao katika mazungumzo ya maridhiano
walitarajia mabadiliko ya uendeshaji wa Bunge Maalum kwani rasimu
inabeba taswira ya nini Watanzania wanataka katika katiba.
Alisema UKAWA ilitaka kuona Bunge Maalum linatekeleza wajibu wake
kisheria katika kujadili, kuboresha na kupitisha rasimu ya katiba
iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutokana na maoni ya
wananchi walio wengi na si kuibomoa, kuibatilisha na kuifuta.
Alisema kuwa sura ya 83 inatambua rasmi rasimu ambayo inabeba maoni
ya Watanzania, taasisi na utafiti wa kina ambazo sura zote zinaeleza
serikali tatu.
Alieleza kuwa UKAWA inataka misingi iliyowekwa iheshimiwe na sio
kubomoa kama ambavyo kanuni zilizowekwa na CCM zinavyoruhusu kuibomoa
rasimu hiyo ili wapate kile wanachokihitaji.
Alisema kuwa CCM inatumia jeuri waliyonayo kutokana na kuwa na
wabunge wengi walioongezwa kwa hila kupitia baadhi ya wajumbe 201.
Akizungumzia hotuba ya Rais Jakaya Kikwete, Mbowe alisema kuwa
udhaifu aliouonyesha katika hotuba ya ufunguzi wa Bunge Maalum la Katiba
ameurudia tena Julai 31, 2014 siku moja kabla ya kikao cha nne cha
mazungumzo ya UKAWA na CCM.
Alisema kuwa pamoja na kauli za kuvuruga Bunge, Kikwete ndie ameukwamisha mchakato huo.
“Kikwete ameendelea kupotosha matumizi ya kanuni ya 33 ibara ya nane
(i) ya kanuni za Bunge Maalum kuhusu mamlaka ya Bunge hilo na kukwepa
kuzungumzia marekebisho yaliyofanyika Aprili 25, 2014 baada ya wajumbe
wa UKAWA kutoka, ambapo mabadiliko hayo mapya yameingiza kanuni mpya ya
32(6) inayoruhusu Bunge Maalum kupendekeza sura mpya,” alisema.
Alisema kuwa marekebisho hayo yalilenga kupenyeza sura za rasimu ya
CCM ya serikali mbili na sura nyingine zilizo kinyume na maoni ya
wananchi juu ya Katiba ya Shirikisho la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mbowe, alisema msimamo potofu wa Kikwete ndio umekuwa msimamo wa
wajumbe wa CCM na kukwamisha maridhiano ambayo yangewezesha muafaka wa
kunusuru mchakato huo.
Alisema kuwa kutokana na kutorejea katika Bunge la Katiba, wameamua
kuanza mazungumzo miongoni mwa viongozi na wajumbe wa UKAWA na wataeleza
uamuzi mbadala utakaofanyika ili kuwezesha kupatikana kwa katiba ya
wananchi.
NCCR-Mageuzi
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema kuwa katiba ni
suala la kisiasa na si kisheria na ndiyo maana wajumbe wa Bunge Maalum
la Katiba hawakuchaguliwa na wananchi na kuongeza kuwa njia ya
kupatikana katiba ipo ikiwa utashi wa kisiasa katika vyama hasa CCM
utatolewa.
CUF
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema kuwa Rais Kikwete
alipotosha hoja zao wakati UKAWA wanachohitaji ni mambo ya msingi
yanayotokana na wananchi yaheshimiwe.
“Madaraka yasipore maoni ya wananchi ambayo ni mengi ndani ya rasimu
ya katiba, moyo wa rasimu uko katika sura ya sita, Rais Kikwete anasema
kuwa hotuba yake haikuvuruga bali alitoa maoni yake, kwanini
alipoandikiwa barua na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa ajili ya kutoa
maoni yake hakwenda, na hakutoa?
“Kwahiyo aliona sehemu sahihi ya kutoa maoni yake ni kwenye Bunge la Katiba, huo ni usanii wa mtani wangu Mkwere,” alisema.
Mnyika
Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano wa CHADEMA, John Mnyika, alisema kuwa ili katiba ipatikane ni lazima mchakato uwe huru.
Alisema kuwa watawala wa Tanzania ndio wanaweka mazingira ya mchakato
wa katiba kuleta vurugu kutokana na kuwa hakuna nia njema ya watawala
wa ndani kupata katiba na kuongeza kuwa kuitegemea CCM ni kuharibu
mchakato huo.
LISSU
Tundu Lissu, alisema kuwa nia ya UKAWA ni kuona yaliyomo katika rasimu ya katiba hayapinduliwi wala kubatilishwa.
“Aprili 16, 2014 UKAWA ndiyo walitoka bungeni, lakini Aprili 25, 2014
hoja ikapelekwa bungeni ya kubadili kanuni na kuweka vifungu
vilivyoweza kupindua rasimu yote.
“Walijipa mamlaka ya kupindua rasimu, kanuni 32(6) ili kuingiza
rasimu itakayopitisha serikali mbili, hatutarudi na hatuna ajenda
nyingine zaidi ya kutaka tujadili rasimu ya wananchi,” alisema.
Lissu alisema kuwa muundo wa serikali mbili ni kasha tupu kwani Rais
Jakaya Kikwete sio rais wa Zanzibar kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar.
“Muundo wa serikali tatu utatuokoa na hautasambaratisha nchi,
haiwezekani nchi moja iwe na Amiri Jeshi Mkuu wawili, serikali tatu ndio
njia pekee ya kuwa wamoja,” alisema.
Hoja za UKAWA kugoma kurudi kabisa katika Bunge Maalum la Katiba ni
kutotaka kusaliti maoni ya wananchi na kutumia vibaya fedha za umma
kubariki uchakachuaji wa msingi wa rasimu.
Pia kutaka kanuni zilizobadilishwa wakati UKAWA hawapo zifutwe na
lugha za uchochezi, ubaguzi, udini, dharau, dhihaka na matusi ndani ya
Bunge hilo zikomeshwe na badala yake mamlaka ijikite katika kuboresha
rasimu na misingi yake kwa kuzingatia maoni ya wananchi.
Kakobe amlaumu Kikwete
Askofu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zachary
Kakobe, amemshambulia Rais Kikwete kwamba ndiye aliyevuruga mchakato wa
kupatikana kwa katiba mpya.
Kakobe amewataka wajumbe wa UKAWA kutorejea katika Bunge Maalum la
Katiba ambalo alidai limejazwa unafiki na endapo wakiamua kurejea
watakuwa wamerogwa.
Alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam katika maadhimisho ya miaka 25 ya kanisa hilo lililoanzishwa mwaka 1989.
Alisema Rais Kikwete, alipolizindua Bunge Maalum la Katiba, alitumia
fursa hiyo kutoa hoja za kuvuruga rasimu ya wananchi ambayo
iliwasilishwa na Jaji Joseph Warioba.
Askofu Kakobe alisema hoja za Rais Kikwete za kujikanganya alizozitoa
siku hiyo, yalikuwa ni majibu ya maombi ya Jumuiya ya Wakristo wa
Kipentekoste (PCT) ya kuvuruga mchakato wa katiba baada ya kutoa
upendeleo kwa kuwateua baadhi ya wajumbe wakiwamo viongozi wa dini,
kupata uwakilishi kwa baadhi ya Wakristo bila kutenda haki kwa wananchi
wote.
Alisema katika mambo yanayofanywa makusudi na wanadamu, Mungu amewapa
akili ya kuyavuruga, hivyo ndiyo maana wakiwa katika viwanja vya
Sabasaba waliamua kufanya maombi na nguvu ya Mungu inatumika sasa
kuonyesha kuwa mchakato huu ulianzishwa pasipo haki.
“Namtaka Rais Kikwete akiri hadharani kuwa amekosea na awaombe
Watanzania radhi kwa makosa aliyoyafanya hata kusababisha wanasiasa
upande wa upinzani kuunda UKAWA ili haki ya wananchi ipatikane, hivyo
atumie busara kufanya hivyo kwa kuwa ndiye baba wa taifa hili.
“Kuna kauli za viongozi wa CCM kuwa wanataka kutawala milele… sasa
mimi nasema sawa tu wafanye hivyo, lakini kwa kwenda na haki na siyo kwa
kulazimisha kama ilivyo sasa katika suala la katiba… hivyo ni katiba ya
wananchi wote wa Tanzania ambao wamo vyama vya siasa na wasiokuwemo,”
alisema.
Askofu Kabobe alisema katika kujikweza kuwa hajahusika kuvuruga, Rais
Kikwete, amewatumia vibaya viongozi wa dini aliodai wanaegemea upande
wa CCM kuwataka waombee mchakato wa katiba na kuwataka UKAWA warudi
bungeni, huku akijua watumishi hao wanapaswa kufanya kazi isiyo na
upendeleo.
“Daima nitasimama katika kweli nayo itaniweka huru, hapa nasema wazi
kwamba Rais Kikwete ameamua kuwatumia vibaya viongozi wa dini… nao
wakaona bora watumike ili kupata mkate na chai Ikulu ambayo majani yake
ni ya hapahapa nchini, tena Mufindi, siyo dhahabu, wanachoendelea
kukifanya kwa wanachi ni unafiki wala siyo maombi.
“Nilidhani Rais Kikwete atawaambia viongozi hao wamwombee yeye
aliyevuruga mchakato huu na siyo kuuombea mchakato wa katiba na amani…
mimi najua nchi yetu ina amani na amani itavurugwa na hao
wanaong’ang’ania hoja zao, kwani katika hili gumzo la katiba
linaloendelea mtu mjinga tu ndiye atakayewalaumu UKAWA.
“Nawaomba viongozi wa dini wasijikombe kombe Ikulu maana wao
wanamwakilisha Mungu… siogopi kusema kwa sasa hakuna ninachokosa hapa
duniani wala sitaki kupendwa na rais, nitafanya yampendezayo Mungu,”
alisema.
Huku akirudia rudia neno lake kwamba “sema ukweli ili uwe huru”,
Askofu Kakobe alisema anawaunga mkono UKAWA kwa hatua yao waliyofikia
hadi sasa hadi hapo Rais Kikwete atakapoomba radhi na kukubali
wakajadili rasimu ya wananchi, kama watarudi bila makubaliano hayo, basi
watakuwa wamerogwa.
“Nawaunga mkono UKAWA asilimia 100 kwa 100 na ninawaongeza 50 kwa
hatua yao… sasa warudi kwa kauli ya rais kukiri mbele ya wananchi kuwa
amekosea, anajirekebisha ili wajadili rasimu ya katiba, wasipofanya
hivyo basi watakuwa wamerogwa… hakuna maridhiano hapo maana nimefuatilia
na kubaini mazungumzo yanayoendelea yamejawa unafiki.
“Kuwaunga mkono UKAWA kwangu si kwamba nashabikia chama kimojawapo
kinachounda umoja huo hapana… nazungumza kama baba wa kiroho mwenye
kuwachunga watoto wengi wenye vyama vyote vya siasa ambavyo vipo nchini,
ambao wanajua kwamba ninasimamia ukweli tupu,” alisema.
Mdahalo wa wanasheria
Watanzania wametakiwa kuwa makini ili kuzuia kutoingia katika
machafuko kama yale yaliyotokea nchini Kenya baada ya kukosekana kwa
katiba.
Akitoa mtazamo wake jana jijini Dar es Salaam katika mdahalo uliokuwa
na mvutano wa makundi yaliyokuwa yakikinzana katika suala la mchakato
wa katiba mpya, Profesa Patrick Lumumba, amewasihi Watanzania kutopita
njia ambazo ni hatari kufikia upatikanaji wa katiba mpya.
“Msipite njia ambayo wengi hawakupita katika kutafuta amani, kwanini
mvuke maziwa na mzame kwenye madimbwi, tuwashurutishe wanasiasa
wasitupitishe njia iliyopitwa na wengi kwa kumwaga damu,” alisema.
Prof Lumumba alisema kuwa wazalendo wengi nchini wanahitaji katiba
mpya na bado wana imani kuwapo nafasi ya kuipata bila kupigana.
Kwa upande wa UKAWA kugoma kurudi bungeni, Prof. Lumumba alisema kuwa
wana sababu za kususia Bunge Maalum la Katiba kwani msingi wake ni
kujadili rasimu.
Alisema kuwa ujumbe wa UKAWA umeshafika ingawa inaonyesha rais ameshakubali kwamba aliteleza na hawezi kukiri.
Alisema kuwa Watanzania asilimia 99 wanataka rasimu ya katiba ijadiliwe na sio katiba ya wanasiasa.
“Watanzania wanataka watu waache itikadi zao, wasimamie Utanzania
wao, Watanzania wanasema, ikiwa hatuwezi kupata katiba kabla ya
uchaguzi, basi tufanye mabadiliko yanayotakiwa na kisha tuwape jukumu
serikali itakayochaguliwa kusimamia upatikanaji wa katiba mpya
inayotakiwa na Watanzania,” alisema.
Prof. Lumumba alieleza kuwa yeye kama Mkenya anafuatilia kuhusu
Tanzania na kueleza kuwa siasa za nchi hii si za kikabila, lakini zina
matatizo.
Alieleza kuwa wananchi ndio wenye katiba na sio ya wanasiasa waliokwatua madaraka hayo.
“Bunge kazi yake ni kuboresha na sio kubadili na hiyo inafanyika
duniani kote, ikitokea nyie mkabadili mtakuwa wa kwanza duniani, na
wananchi wanatakiwa wahakikishe waliyoyatoa kwenye tume yamo, je
wakikuta hakuna itakuwaje?” alihoji.
Kwa upande wake, Jenerali Ulimwengu alisema kuwa udhaifu wa viongozi
unaweza kuwa ulichangia kukwama na kufika hapo katiba ilipo.
“Baadhi walidhani katiba ndiyo mwanzo wa kukidhoofisha chama tawala
na waliopinga nao pia walidhani wanaweza ondolewa madarakani,” alisema.
Alieleza kuwa watawala walianza kuchafua mchakato toka kutungwa kwa sheria ya mabadiliko ya katiba ya awali iliyoanza.