https://jaridahuru.blogspot.com/2014/08/vyuoni-tahliso-yadai-sh-16-bilioni.html
Dar es Salaam. Jumuiya ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Tanzania
(Tahliso) imetoa wiki moja kwa Serikali kutoa majibu ya lini vyuo saba
vitapatiwa fedha kwa ajili ya wanafunzi wanaokwenda kwenye mafunzo kwa
njia ya vitendo.
Jumuiya hiyo imesema kama wizara husika itashindwa
kutoa tamko lolote kuhusu fedha hizo, Tahliso itafanya uamuzi mwingine
kuwakomboa wenzao waweze kuendelea na mafunzo ya vitendo kama ratiba
inavyoonyesha.
Akizunguza na waandishi wa habari jana jijini
hapa, mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Musa Mdede alisema wiki nne zimepita
tangu mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi yaanze, lakini bado vyuo saba
havijapata pesa.
Vyuo ambavyo havijapata pesa hadi sasa ni Saut
tawi la Mwanza na Tabora, Tumaini Makumira Arusha, Stephano, Moshi
mkoani Kilimanjaro, Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Teophilo Kisanji,
Mbeya na Chuo Kikuu cha Jordan, Morogoro. Fedha zinazotakiwa ni Sh1.6
bilioni.
“Tunataka Serikali itueleze kwanini baadhi ya vyuo havijapewa pesa hadi sasa wakati mafunzo yameshaanza,” alisema Mdee.
Mkurugenzi wa habari wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya
Juu Tanzania (HESLB), Cosmas Mwaisoba hakuweza kupatikana jana
kuzungumzia suala hilo.
Katika hatua nyingine, Tahliso imewaonya wanasiasa
wanaoingilia masuala ya elimu kupitia umoja wao kwa lengo la
kujinufaisha, kuacha tabia hiyo mara moja.
“Jumuiya yetu ipo kwa ajili ya kutetea masilahi ya
wanafunzi na siyo masilahi ya chama chochote cha siasa. Nawaomba
wanasiasi wajiepushe kujiingiza kwenye umoja wetu kwa vile hawatafaidika
na chochote,” alisema.
“Natoa onyo kwa wanasiasa. Hakuna sababu kwa wao
kuingilia kati utendaji wa Tahliso, kwani dhamira yetu siyo kujiingiza
kwenye siasa ila kutetea haki za wanafunzi nchini,” aliongeza