KITAIFA: POLISI NCHINI WANOLEWA ILI KUJIANDAA NA UCHAGUZI MKUU 2015

https://jaridahuru.blogspot.com/2014/06/kitaifa-polisi-nchini-wanolewa-ili.html
Dar es Salaam. Harakati za kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015 zimeanza. Polisi wameanza mafunzo yatakayowaongezea uwezo wa kusimamia uchaguzi huo.
Mafunzo hayo yanafadhiliwa na Shirika la Mpango wa
Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), kupitia mradi wake wa Uwezeshaji
wa Demokrasia (DEP).
Wakufunzi wanane kutoka Chuo cha Polisi cha Uingereza wanaendesha mafunzo kwa maofisa 88 wa polisi wa ngazi za juu na kati.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo, Naibu
Kamishna wa Polisi, Simon Sirro alisema yamekuja wakati mwafaka wakati
jeshi hilo likijiandaa kwa shughuli hiyo muhimu ya kitaifa.
Mafunzo hayo yanayofanyika Dar es Salaam na
Zanzibar yanalenga kuwajengea uwezo makamanda wa polisi wa kupanga,
kumudu na kuratibu kwa ufanisi hatua za kipolisi za matukio yanayotishia
utulivu wa amani katika jamii.
Alisema katika kila kozi ambayo itaendeshwa kwa
wiki mbili, itatoa mafunzo kwa maofisa hao ya kuheshimu haki za
binadamu, utawala wa sheria na namna ya kudhibiti ghasia na baadaye
kuwafundisha askari wote waliobaki. “Tunataka maofisa wetu wawe na ujuzi
wa kutosha kusimamia wakati wa vurugu ili uchaguzi ujao uwe wa haki na
amani. Wawe na uwezo mzuri wa kuwaelewesha wananchi juu ya kazi yao ili
kuendeleza imani juu ya polisi nyakati kama hizo. Pia yatatusaidia
kutambua namna gani tufanye kazi katika mazingira ya vurugu yenye watoto
na wanawake.”
Alipoulizwa juu ya matumizi ya nguvu nyingi kwa
raia, Sirro alisema wasingependa polisi kutumia nguvu hizo lakini
mazingira husika hulazimisha hali hiyo kutokea.
“Ukiona tumetumia moshi… moshi… tumeona mazingira
yameturuhusu kufanya hivyo. Askari polisi anapotumia moshi kukutawanya
unasema nguvu kubwa… nashindwa kukuelewa. Kwa mfano, wewe una panga na
mimi nina kirungu… unakuja kunipiga na panga hivi nikitumia kirungu
kukupiga ili nikupeleke polisi kuna ubaya?
Mtaalamu wa masuala ya usimamizi wa uchaguzi wa
UNDP nchini, William Hogan alisema taasisi yake inathamini uchaguzi
mkuu, pia namna polisi wanavyotumika katika uchaguzi katika nchi za
kidemokrasia. “Umakini wa polisi wakati wa usimamizi wa uchaguzi hususan
katika kuheshimu haki za binadamu na utawala wa sheria ni moja ya vitu
muhimu ambavyo hupima iwapo uchaguzi husika ulikuwa wa haki na wazi
hivyo polisi wanahitajika kuongezewa uwezo,” alisema Hogan.
Alisema mafunzo hayo ni mwendelezo tu wa mafunzo kwa polisi kwani yalishafanyika 2010 na yalikuwa na mafanikio.
Alisema wanataka uchaguzi mkuu ujao uwe bora ulimwenguni kwa kuanzia na kuheshimu haki za binadamu na utawala wa sheria.