VYUONI: WANAFUNZI ST. JOHN HATARINI KUKOSA NAFASI ZA KUJIUNGA NA VYUO VIKUU NCHINI, WAZAZI WAJA JUU

Wakati wanafunzi hao wakisotea hilo, tarehe ya mwisho, ambayo wanatakiwa wawe wamewasilisha maombi ya kujiunga na vyuo vikuu yakiwa yameambatanishwa na matokeo hayo yenye mhuri wa chuo, ni Alhamisi wiki hii.
Wakizungumza na NIPASHE kwa nyakati tofauti, wanafunzi hao walisema uongozi umekuwa ‘ukiwazungusha’ kuwapatia matokeo hayo licha ya kuyalipia Sh. 10,000 benki na kupeleka stakabadhi za malipo hayo chuoni.
Mmoja wa wanafunzi hao, ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, akizungumza na NIPASHE kwa niaba ya wenzake, alisema baada ya kumaliza masomo Februari, walisubiri matokeo, ambayo yalitoka Aprili, mwaka huu, lakini yakiwa hayajakamilika kwa baadhi ya wanafunzi.
“(Katika matokeo yaliyotoka) utakuta sehemu nyingine mtu hajapatiwa majibu. Hivyo, ilibidi ajaze fomu kuomba kupatiwa hayo majibu. Au kama mtu alihisi kupunjwa maksi, anarekebisha,” alisema.
Alisema baada ya kujaza fomu hizo, walisubiri siku kadhaa na kupata matokeo yote yakiwa yamesawazishwa.
“Sasa kinachofuata inabidi tuombe kujiunga na ngazi ya digrii (Shahada) katika vyuo fulani kupitia Nacte (Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi) kwa njia ya online (mtandao wa kompyuta).”
Alisema utaratibu uliopo unataka mwanafunzi anayetaka kuomba kujiunga na chuo chochote, lazima awe amepata matokeo yote yakiwa na mhuri wa chuo anachotoka ili akubaliwe kujiunga.
“Sasa kuipata hiyo karatasi ya matokeo (revision result) ndiyo imekuwa shida licha ya kwamba, tumeshailipia benki Sh. 10,000 kuipata. Kadri tunavyofuatilia, tunazungushwa. Unaambiwa mara umeme umekatika, mara hivi, mara vile. Ilimradi tunapigwa kalenda kila siku, wakati mwisho wa kuomba kujiunga na vyuo ni Julai 31,” alisema.
Naibu Mkurugenzi wa Chuo hicho Kampasi ya Dar es Salaam, Mwalimu Amani Chipato, akizungumza kwa niaba ya Kaimu Mkuu wa Chuo, Naomi Katunzi, alisema matokeo yalikwishatoka, lakini hayajapelekwa Nacte.
Alisema hiyo inatokana na chuo kuchelewa kupata taarifa za mabadiliko ya kukabidhi matokeo Nacte ili yawekwe kwenye mtandao.
Akijibu swali jinsi gani watawasaidia wanafunzi kupeleka maombi vyuoni kabla ya Julai 31, Mwalimu Chipato alisema: “Ikitokea kwamba imeshindikana, hakutakuwa na namna.”
Hata hivyo, alisema Nacte hawapaswi kulaumiwa, kwani mfumo wa chuo ndiyo unaokabiliwa na tatizo la mawasiliano kati ya makao makuu ya chuo yaliyoko mkoani Dodoma na Kampasi ya chuo cha Dar es Salaam.