KATIKA kutekeleza majukumu yake ikiwemo Baraza la Mitihani la
Tanzania (NECTA) limepata mafanikio mbalimbali kuboresha Mfumo wa
Usahihishaji wa Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) na kupanga
shule kulingana na kiwango cha ufaulu “Ranking” kwa kuonesha shule
zilizofanya vizuri na shule ambazo hazikufanya vizuri.
NECTA ni taasisi ya umma chini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ambayo ilianzishwa Mwaka 1973.
Kaimu Katibu Mtendaji wa NECTA Dk. Charles Msonde, anasema mafanikio
mengine ni kudhibiti udanganyifu katika mitihani, matumizi ya
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA) katika usajili wa
watahiniwa, kuweka picha ya mtahiniwa husika kwenye cheti na kujenga
kituo cha usahihishaji Mbezi Wani.
Akizungumza kwa kina anasema kuanzia mwaka 2012 watahiniwa wa
Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) walianza kufanya mtihani wa kutumia
karatasi maalum za (OMR) ambazo husahihishwa kwa kutumia mfumo wa
kompyuta.
Mfumo huo anasema umekuwa na manufaa ikilinganishwa na usahihishaji
wa mkono. Anabainisha kuwa kwa kutumia mfumo wa OMR, idadi ya watahini
na siku za kusahihisha Mtihani zimepungua na hivyo kupunguza gharama za
usahihishaji.
“Mtihani wa mwaka 2013 jumla ya watahini 301 walishirki katika
zoezi la usahihishaji ikilinganishwa na idadi ya watahini zaidi ya 4000
ambao walikuwa wakishiriki kabla ya mfumo wa usahihishaji wa kompyuta
haujaanza. Usahihishaji huo ulifanyika kwa siku 16 badala ya siku 30
zilizokuwa zikitumika awali. Pia usahihishaji ulifanyika kwa usahihi
zaidi ikilinganishwa na usahihishaji wa kalamu unaofanywa kwa mkono.
“Ili usahihishaji wa kutumia mkono uwe sahihi, miaka ya nyuma Baraza
la Mitihani lililazimika kuwa na hatua nyingi za uhakiki ili kuepusha
kuwepo kwa makosa machache ya kibinadamu, jambo ambalo lilifanya kazi
ya usahihishaji kutumia muda mrefu, watu wengi na gharama kubwa.
“Tumewahi kulinganisha kati ya wasahihishaji wa mkono na Mfumo wa
Kompyuta ambapo ilithibitika kuwa Mfumo wa Kompyuta husahihisha kwa
usahihi wa asilimia mia moja wakati msahihishaji wa mkono aliweza
kufanya makosa ya kibinadamu katika zoezi hilo na hivyo kufanya kazi ya
usahihishaji kuwa na hatua nyingi za uhakiki katika kuondoa dosari
zinazobainika,” anasema.
Dk. Msonde anaedelea kueleza kuwa baada ya kuanza kutumia mfumo wa
OMR na kusahihisha kwa kutumia kompyuta, Baraza la Mitihani limeweza
kufanya uchambuzi kuonesha namna watahiniwa wanavyojibu maswali kwa
kubainisha maswali waliyopata, waliyokosa, majibu waliyojaza na namna
walivyoelewa maswali ya mitihani.
Anasema uchambuzi huo wa kitaalam umeandaliwa na kuchapwa katika
vitabu maalum ambavyo vinasambazwa katika shule zote ili kuwawezesha
walimu kujua namna ya kuwasaidia wanafunzi katika kujibu maswali
ipasavyo. Hii itasaidia kuboresha ufaulu wa watahiniwa katika mitihani
ijayo.
Dk. Msonde anasema baraza limefanikiwa kupanga shule katika
makundi mbalimbali ya ufaulu na kufafanua uwezo wa kila kundi. Taarifa
hii imewekwa katika tovuti za Baraza la Mitihani la Tanzania, Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Ofisi ya waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (Tamisemi) na itawawezesha wadau
mbalimbali wa elimu kufanya maamuzi yenye lengo la kuboresha elimu kwa
kila shule kulingana na uwezo uliooneshwa.
Anafafanua kuwa taarifa hii itasaidia Serikali katika kupima
mafanikio yaliyopatikana kwa kila shule kwa kulinganisha na uwekezaji
wa rasilimali kwa kipindi husika.
Kwa mujibu wa maelezo ya Kaimu Katibu Mtendaji, NECTA kwa
kushirikiana na Kamati za Uendeshaji Mitihani katika ngazi za Mikoa,
Wilaya na Wasamaria wema, limeweza kwa kiasi kikubwa kudhibiti
udanganyifu katika Mitihani.
Dk. Msonde anatoa mfano katika Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi
mwaka 2013 watahiniwa waliofutiwa matokeo kwa kufanya udanganyifu
walikuwa 13 tu idadi ambayo ni ndogo ikilinganishwa na watahiniwa 9,736
waliobainika kufanya udanganyifu mwaka 2011 na 293 mwaka 2012.
Katika mtihani wa kumaliza kidato cha nne mwaka 2013; anasema
watahiniwa waliofutiwa matokeo kwa kufanya udanganyifu walikuwa 272
ikilinganishwa na 789 mwaka 2012 na 3,303 mwaka 2011.
“Katika mtihani wa kumaliza kidato cha sita mwaka 2013 mtahiniwa
mmoja tu ndiye aliyefutiwa matokeo. Idadi hii ni ndogo ikilinganishwa
na watahiniwa watano waliobainika kufanya udanganyifu mwaka 2011 na
watatu mwaka 2012,” anaeleza Dk. Msonde.
Dk. Msonde anasema baraza linafanya usajili wa watahiniwa kwa kutumia
mfumo wa kompyuta ambapo taarifa za watahiniwa wa shule hukusanywa
kwa kushirikiana na Mkuu wa Shule na kuhifadhiwa katika CD ambayo
huwasilishwa NECTA. Pia watahiniwa wa kujitegemea hujisajili wenyewe
kwa kutumia mtandao.
Dk. Msonde anasema miaka ya nyuma watu wengi walikuwa wanatumia vyeti
vya watu wengine au kughushi vyeti. Kuanzia mwaka 2008/2009 NECTA
ilianza utaratibu wa kuweka picha ya mtahiniwa husika kwenye cheti
chake. Mafanikio haya yamelifanya Baraza kuwa na uwezo wa kuwabaini na
kuwachukulia hatua watahiniwa wanaoghushi vyeti au kutumia vyeti vya
watu wengine.
Anasema kazi ya usahihishaji Mitihani hufanyika katika vituo
mbalimbali. Mwaka 2010 Baraza la Mitihani lilikamilisha ujenzi wa Kituo
cha Usahihishaji cha Mbezi Wani ambacho kinao uwezo wa kuweka
washiriki 900 kwa wakati mmoja.
Akizungumzia changamoto katika utekelezaji wa shughuli za Baraza la
Mitihani, Dk. Msonde anaeleza baadhi ya changamoto kwamba watu hutumia
vyeti bandia katika kujipatia ajira, shule au vyuo.
Anatoa mfano kwa kueleza kuwa katika mwaka wa fedha wa 2012/2013
jumla ya vyeti 1,891 sawa na asilimia 3.7 ya vyeti vyote 50,497
vilivyowasilishwa kwa ajili ya uhakiki vilibainika kuwa ni vya
kughushi. Hata hivyo tatizo hilo limekuwa likipungua mwaka hadi mwaka
baada ya NECTA kuanza kutoa vyeti venye picha.
Dk. Msonde anasema baraza linatoa wito kwa waajiri na Vyuo mbalimbali
nchini kuhakikisha kuwa vyeti vinavyowasilishwa kwao vinaletwa Baraza
la Mitihani kwa ajili ya kuhakikiwa.
Anasema pia kuna udanganyifu ingawa vitendo vya udanganyifu katika
mitihani vinazidi kupungua sana, kumekuwepo na vitendo vichache vya
udanganyifu ambao hufanywa kwa mbinu mbalimbali kama vile kuingia na
vijikaratasi vya kutazamia au kuandika majibu mwilini na baadhi ya
Wasimamizi kuwasaidia watahiniwa.
Kwa mujibu wa baraza linaendelea kuimarisha usimamizi wa Mitihani na
kuwachukulia hatua stahiki wale wote wanaobainika kujihusisha na
udanganyifu katika mitihani.
Anasema baadhi ya shule na vyuo huwasajili wanafunzi wasio na sifa
kinyume na taratibu za wizara, hivyo baraza linatoa wito kwa wakuu wa
shule na vyuo vya ualimu kuhakikisha wanazingatia miongozo ya usajili
inayotolewa na NECTA.