SIASA: MBUNGE WA CHADEMA, EZEKIA WENJE, AUNDIWA SKENDO YA URAIA TENA, MARA HII MAMA YAKE ATISHIWA AMKANE

WAKATI taifa likielekea katika uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na rais, mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenje (CHADEMA), ameanzishiwa tena zengwe la uraia.
Hii si mara ya kwanza kwa mbunge huyo kudaiwa kuwa si raia wa Tanzania, kwani hata mwaka 2010 wakati wa uchaguzi mkuu, mpinzani wake wa CCM, Lawrence Masha, alitumia nguvu nyingi kumwekea pingamizi ili asigombee kiti hicho.
Awali msimamizi wa uchaguzi katika Jimbo la Nyamagana wakati huo, alimwengua Wenje kwa madai kwamba si raia halali wa Tanzania na hivyo kumfanya Masha kuwa mgombea asiyekuwa na mpinzani.
Lakini baada ya Wenje kukata rufaa akionyesha vielelezo vyote husika vya kuthibitisha uraia wake, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilirejesha jina lake na baada ya kura kupigwa aliibuka mshindi.
Akizungumza na gazeti hili jana, Wenje alisema kuwa Juni 5 mwaka huu, saa 2:00 usiku kuna watu wawili walikwenda nyumbani kwao Kitongoji cha Okebe, Kijiji cha Mkoma, Kata ya Mkoma, Tarafa ya Nyancha Wilaya ya Rorya mkoani Mara.
“Walifika kwa mama yangu mzazi, mama Tabitha Wenje, wakidai kwamba wametumwa na serikali na kuna taarifa rasmi kwamba mimi sio raia wa nchi hii.
“Kwamba wana taarifa kwamba mimi sijasoma Tanzania kuanzia darasa la kwanza na taarifa za kuwa nilisoma Michire Shule ya Msingi, Shirati Sekondari, Geita High School, Butimba TTC na St. Augustine University zote ni uongo,” alisema.
Wenje alisema kuwa watu hao walidai kuwa wametumwa kwa dharura kukusanya taarifa haraka ili apelekwe mahakamani, aondolewe urai na ubunge na kuzuiwa kugombea 2015.
“Kimsingi walimtishia mama yangu ili asaini makaratasi ya kunikana kwamba mimi sio mtoto wake ila alikataa. Ikumbukwe kwamba Kijiji cha Mkoma tunaishi ukoo mzima wa Kamsangia, kwa hiyo hizi njama zinaanza tena kama 2010 kwa sababu tu uchaguzi umekaribia,” alidai.