SIASA: UKAWA YABAINIKA KUWA MCHAWI WA CHADEMA, YADAIWA KUSABABISHA FIGISU ZINAZOTOKEA NDANI YA CHADEM
https://jaridahuru.blogspot.com/2014/07/siasa-ukawa-yabainika-kuwa-mchawi-wa.html
IMEBAINIKA kwamba msukosuko unaotokea katika Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) unatokana na hasira za serikali kushindwa kushawishi
chama hicho na vingine vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA)
kurejea kwenye Bunge la Katiba mwezi ujao.
Habari za uhakika kutoka vyanzo vyetu ndani ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM) na serikali zinasema kuwa hata mgogoro kati ya Ofisi ya Msajili wa
Vyama vya Siasa na CHADEMA una msukumo wa serikali, ili kudhoofisha
chama kikuu cha upinzani kabla ya kuendea vingine kabla ya Agosti, mwaka
huu.
Serikali imekuwa inashinikiza kila taasisi itoe kauli dhidi ya
msimamo wa UKAWA kutorejea bungeni, lakini nguvu kubwa imeelekezwa kwa
CHADEMA kwa kuwa ndicho kinaonekana kuongoza UKAWA, na kwamba hicho
kikiyumba, vingine vitayumba na kuingiliwa kirahisi.
Baadhi ya makada wa CCM ambao hawakubaliani na msimamo wa chama chao
kuhusu rasimu ya pili ya katiba, waliliambia gazeti hili kwamba hata
suala la mgogoro unaoibuka kati ya CHADEMA na Ofisi ya Msajili wa Vyama
vya Siasa, ni wa kutengenezwa ili kudhoofisha chama hicho.
Akizungumza kwa kujiamini, na akikubali kunukuliwa bila kutajwa jina, kada huyo alisema:
“Unajua, serikali imeshindwa kushawishi wapinzani wakubaliane na
msimamo wetu kuhusu rasimu. Mara kadhaa umesikia viongozi wa upinzani
wakitoa matamko kwamba hawatarejea kwenye Bunge la katiba, la sharti lao
ni moja, kwamba ili warejee lazima mjadala ujikite katika rasimu
iliyoletwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
“Sasa ukichunguza, utaona kwamba kweli wapinzani wana hoja, lakini
sisi chama chetu kimeamua kufuata kauli ya mwenyekiti, kwamba serikali
tatu haziwezekani, zitavunja Muungano, ingawa si wote tunakubaliana naye
katika hilo.
“Lakini woga wa kumpinga mwenyekiti ndiyo umetufikisha hapo, maana hata sisi tusiokubaliana naye tunalazimika kunyamaza tu.
“Sasa bwana mkubwa ameona atumie viongozi wa dini na watu wenye sauti
katika jamii, ili kusukuma hoja hii, na ndiyo maana unasikia baadhi ya
viongozi wa dini wanasema UKAWA warejee bungeni bila masharti.
“Hata ofisi ya msajili imeshinikizwa, kwamba kwa kuwa CHADEMA ndicho
kinaongoza UKAWA, kikishatetereshwa, uongozi uka-panic kwa sababu ya
presha ya migogoro, hawatakuwa na uwezo wa kusimamia UKAWA, na
wakishalegea hao, itakuwa rahisi kushughulika na wenzao CUF na
NCCR-Mageuzi.”
Alisema ofisi ya msajili inajua fika kwamba Katiba ya CHADEMA haina
matatizo, lakini kwa kuwa wapo wanachama waliofukuzwa ambao walilivalia
njuga suala hilo, na kwa kuwa chama kipo katika uchaguzi wa ndani, na
kwa kujua nafasi ya viongozi wakuu wa chama katika mchakato huo,
serikali iliona ijaribu hata mbinu hiyo.
Hata hivyo, mbinu hiyo imeshindwa kuitikisa CHADEMA kwa kuwa
kimeonyesha kumbukumbu za maelezo kuhusu hoja husika, na viongozi
hawajishughulishi na propaganda hizo, bali wanaendelea na kazi zao.
Katika wiki moja iliyopita, vyombo vya habari vimekuwa vinaripoti
habari kutokana na matamko kutoka kwa watu na taasisi kadhaa nchini
yanayowataka wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kurejea bungeni bila
masharti ili kuhakikisha katiba mpya inapatikana.
Waziri Mkuu alitoa kauli yenye kuonyesha kuwa uchaguzi wa serikali za
mitaa utategemea uwapo wa katiba mpya. Mwanasheria Mkuu wa Serikali
mstaafu Jaji Mark Bomani alizugumza na vyombo vya habari akisema ni vema
wajumbe wajikite kwenye masuala mengine kwanza badala ya kubishania
hoja ya muungano na muundo wake.
Mara mbili ndani ya wiki moja, viongozi waandamizi wa Kanisa Katoliki
wametoa kauli za kuwataka wajumbe hao warudi bungeni bila masharti.
Tamko la hivi karibuni ni lile la Baraza la Maaskofu Katoliki
Tanzania (TEC), lililotolewa juzi na Rais wake, Askofu Tarcisius
Ngalalekumtwa.
Katika tamko hilo, waliwataka wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba,
wawe wamoja na kufanya kazi yao kwa mtazamo usioegemea siasa za vyama.
Waliwakumbusha wajumbe hao kuwa yeyote anayedharau hitaji la katiba
mpya ama anayejaribu kupuuza na kuweka kando rasimu ya pili, huyo si
mwakilishi wa utashi wa watu, na kwamba mwisho wake historia itamhukumu.
“Kwa moyo wa sala na tafakari makini, tulifuatilia mlivyojadiliana
katika Bunge la Katiba kuanzia Februari hadi Aprili 2014. Katika siku 67
ninyi wateule wa rais mpatao 600, mlijadiliana pasipo umoja,
mkishambuliana kwa kauli kali kati yenu, mkikashifiana pasipo udhibiti
wa uongozi mliojichagulia wenyewe kwa kanuni na sheria mlizojitungia,”
lilisomeka tamko hilo.
Kwa mujibu wa TEC, mwenendo huo ulikuwa wa kusikitisha na kuchukiza
katika mahali pale panapoheshimika. Kwamba, kanisa lilitegemea
majadiliano katika kuheshimiana hoja za kizalendo na kiungwana
zitokanazo na mambo ya masuala makuu yaliyopendekezwa katika rasimu ya
pili ya katiba.
“Badala yake, tulijionea mabishano makali na mpasuko uliosababisha
upotoshaji wa nia iliyokusudiwa. Hatimaye hila na gilba zikateka kabisa
jukumu adili la Bunge la Katiba.
“Tukumbuke Rais Jakaya Kikwete kwa uthubutu na ujasiri wa kipekee,
alianzisha mchakato wa kuunda katiba mpya, na kisha aliridhia kwa
kuipokea kwa furaha rasimu ya pili ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba,”
lilisomeka tamko hilo.
Kwamba, ni lazima kujiuliza ni nini kilitokea hadi kugeuza kabisa
mwelekeo mzima wa mchakato wa katiba kwa kuikejeli na kuishutumu vikali
rasimu hiyo katika wakati wa kipekee kabisa wa kihistoria wa uzinduzi wa
Bunge Maalumu. Hata kusahau gharama kubwa ambayo ilibebwa na walipa
kodi.
“Na sasa hali hii inaonyesha dhahiri jambo hili limeiingiza nchi
katika mgogoro mkubwa unaoashiria hatari mbeleni,” walisema maaskofu
hao.
Maaskofu waonywa kuhusu UKAWA
Hata hivyo, Mwinjilisti Medard Kyabashasa wa Kanisa la Tanzania
Assemblies of God (TAG), wa Mbagala, Dar es Salaam, amekerwa na matamko
ya viongozi wa dini dhidi ya UKAWA, bila kujali sababu iliyowafanya
kususia Bunge, na bila kumkemea Rais Jakaya Kikwete aliyesababisha mzozo
huo.
Kwa mujibu wa Mwinjilisti huyo, msimamo wa UKAWA ni kusimamia maoni
ya wananchi, wakiwemo maaskofu wenyewe. Hivyo, kilichowatoa bungeni ni
kutetea maoni ya wananchi yanaachwa, ambayo watawala wanataka yapuuzwe,
tume itukanwe na kuacha watu wakileta mawazo yao ya mifukoni.
Kutokana na hali hiyo, Kyabashasa amewataka viongozi wa dini wawe wawazi, waache unafiki wa kupamba jambo ovu.
“Viongozi wa dini waache unafiki, kama wanadhamiria kweli kusaidia
katiba ipatikane, lazima wawakemee wabunge wa CCM na mwenyekiti wao kwa
kuvuruga mchakato na kung’ang’ania kujadili vitu ambavyo havimo katika
rasimu ya pili na ambavyo vipo kinyume cha sheria,” alisema Kyabashasa.
Aliongeza kuwa viongozi wote wa dini wanajua wazi kuwa aliyevuruga
mchakato wa katiba mpya ni Rais Jakaya Kikwete. Badala ya maaskofu na
viongozi wengine wa dini kumkemea moja kwa moja, wamekuwa wakifumbafumba
halafu wanalaumu UKAWA na kuanza kuwasihi warejee bungeni.
Alihoji kuwa maaskofu wanapowaomba UKAWA kurejea bungeni, kinachoenda
kujadiliwa baada ya UKAWA kukubali wito wao ni nini? Je, ni rasimu ya
pili yenye maoni ya wananchi kama ilivyoandikwa na Tume ya Jaji Warioba
au kwenda kujadili msimamo wa CCM unaolazimisha maoni ambayo hayapo
kwenye rasimu?
“Tuliona UKAWA walitumia kila njia kuhakikisha maoni ya wananchi
yanajadiliwa ikashindikana na baada ya hapo, wakaamua kutoka kama njia
ya kuonyesha shinikizo kwa wajumbe wenzao kurejea katika mstari wa
kujadili rasimu halali iliyopitishwa kisheria,” alisema.
Mwinjilisti huyo akitoa mifano kutoka katika Biblia, aliwataka
maaskofu na viongozi wengine watakaotoa matamko, kuiga mfano wa Yohana
Mbatizaji, alivyomwambia Herode waziwazi kuwa kuchukua mke wa ndugu yake
lilikuwa kosa.
“Mungu ametupa akili na uelewa, tusifanye mambo kwa makusudi halafu
tunaanza kutegemea maombi, ni kama vile tunaona mtu anatunywesha sumu
kwa makusudi, halafu tunakazana kuomba Mungu sumu isituue,” alisema
mwinjilisti huyo.
Aliwataka viongozi wa dini wailamu CCM wazi wazi, waeleze kosa la CCM
na Kikwete waziwazi, ndipo wapate ujasiri wa kuwasihi UKAWA kurejea
bungeni wakakae wajadili rasimu ya pili ya katiba.
“Viongozi wa dini wawaambie viongozi wa CCM kuwa wanavuruga nchi kwa
makusudi kwa jeuri ya wingi wao bungeni, jeuri ya fedha na dola, hadi
kulazimisha mambo ambayo yapo kinyume cha maoni ya wananchi,” alisema.
CCM hawakuwa na nia ya dhati ya kuleta katiba mpya, walijua mchakato
ukianza ni wapi wataivuruga, hivyo wa kulaumiwa ni wao, ndio maana
wanatamba kwamba mchakato ukikwama turejee kwenye katiba ya zamani.
“Viongozi wa dini tuna nafasi kubwa sana ya kuirejesha serikali
kwenye mstari kama Bunge limeshindwa. Tuikemee serikali waziwazi
inapokwenda kinyume, tumechoshwa na wizi, leo unasikia Escrow, leo
rushwa, lakini viongozi tunapotoa matamko tunaogopa kuiambia CCM kuwa
imefanya hayo, tumebaki tunaomba kusali ili amani iliyopo iendelee…,
iendelee ili waendelee kuiba, kula rushwa na kufanya ujangili?” alihoji.
Tangu UKAWA waamue kutoka bungeni Aprili 16 mwaka huu, kumekuwa
kukitolewa matamko na watu pamoja na taasisi mbalimbali za kidini, huku
mengi yakiishia kuwasihi UKAWA kurejea bungeni bila kuangalia kiini
kilichowafanya watoke.