SIASA: MAMBO MATANO YALIYOIBUKA KATIKA ZIARA YA KINANA TABORA

https://jaridahuru.blogspot.com/2014/06/siasa-mambo-matano-yaliyoibuka-katika.html
Katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana amekuwa akifanya ziara katika mikoa mbalimbali nchini.
Kwa siku 11 alikuwa Tabora na kutembelea Igunga, Nzega, Uyui, Sikonge, Urambo, Kaliua na Tabora Mjini.
Kinana akiwa na katibu wake wa itikadi na uenezi,
Nape Nauye walikagua uhai wa chama na kukutana na changamoto nyingi
katika ziara hiyo ambazo wananchi wa Tabora wanataka zipatiwe ufumbuzi.
Ujenzi wa bomba la maji
Wilayani Igunga na Nzega lilijitokeza tatizo kubwa
la maji na wananchi wakakumbuka ahadi iliyowahi kutolewa na Rais Jakaya
Kikwete ya ujenzi wa bomba la maji kutoka Ziwa Victoria hadi mkoani
humo.
Hivi sasa bomba hilo kutoka Ziwa Victoria linaishia mkoani Shinyanga.
Mwenyekiti wa CCM wa Tabora, Hassan Wakasuvi
alimweleza Kinana kuwa tatizo la maji ni kubwa na kwamba wananchi wa
mkoa huo wanaikumbuka ahadi iliyotolewa na Rais kwamba angewaletea maji
kutoka Ziwa Victoria.
“Mkoa huu ni ngome ya CCM kwa sababu wabunge wote
na zaidi ya asilimia 90 ya madiwani ni wa CCM. Tunaomba katibu mkuu
ukamkumbushe Rais kwamba tunaomba ahadi yake itekelezwe kabla hajamaliza
kipindi chake cha uongozi mwaka 2015,” alisema.
Baada ya kuwasiliana na Serikali, Kinana alisema
kwamba serikali wakati wowote kuanzia sasa itasaini mikataba ya upembuzi
yakinifu na michoro ikiwa ni maandalizi ya utekelezaji wa mradi wa
bomba la maji kutoka Shinyanga kwenda Tabora.
“Tena nimeongea na Waziri wa Maji, Profesa Jumanne
Maghembe kwamba mikataba hiyo isainiwe Tabora ili wananchi waweze
kushuhudia kuanza kwa mradi huo,” anasema na kuongeza kwamba wakati
upembuzi huo ukifanyika Serikali inatafuta fedha za ujenzi wa bomba
hilo.
Hifadhi ya Misitu
Kilio kikubwa kilichotolewa na wanachama wa CCM ni ufinyu wa ardhi kwa ajili ya makazi na kilimo na ufugaji.
Kilio hicho kiliungwa mkono na mkuu wa mkoa, Fatma Mwasa ambaye
alisema asilimia 70 ya ardhi ya mkoa huo ni hifadhi ya misitu na
asilimia 30 ndiyo inayotumika kwa ajili ya kilimo.
Hali ni mbaya zaidi kwenye Wilaya ya Sikonge
ambayo asilimia 95 ya ardhi `imefunikwa’ na misitu ambayo ni hifadhi ya
misitu ambayo hairuhusiwi kuitumia kwa shughuli za kibinadamu.
Wana-CCM ambao ni wafugaji walilalamikia kukamatwa
na maofisa misitu kila wakati mifugo inapoingia kwenye hifadhi na
kuomba Serikali iongeze eneo la matumizi ya binadamu kwa sababu watu
wanazidi kuongezeka. Akijibu hilo, Mwassa anasema ameshapeleka
mapendekezo Wizara ya Maliasili na Utalii ili waweze kushughulikia
tatizo hili.
“Katibu mkuu hili ni tatizo kubwa katika mkoa huu.
Tunaomba maeneo ya hifadhi yamegwe kwa sababu idadi ya watu hivi sasa
inazidi kuongezeka. Hakutakuwa na maana kutenga eneo la hifadhi kubwa
wakati wananchi wanapata shida,” anasema. Kinana kwa upande wake
aliahidi kufuatilia suala hilo serikalini.
Zahanati
Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Elibariki Kingu alitoa
kilio cha wananchi kwamba licha ya kuhamasisha wanavijiji kujitolea
kujenga zahanati katika kijiji na kufanikiwa kujenga zahanati 70, tatizo
ni kwamba hazijasajiliwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii hivyo
hazijaanza kufanya kazi kwa sababu hakuna nyumba za watumishi.
“Wanavijiji wanatembea umbali mrefu kutafuta
huduma za afya huku majengo yao ya zahanati yakiwa yamekamilika,
tunapoulizwa na wananchi kwa nini hazijafunguliwa tunapata wakati mgumu
kuwajibu, tunaomba wizara iache urasimu,” alisema.
Majibu ya Kinana
Kinana anasema huo ni urasimu wa viongozi wa wizara hiyo na kwamba atafuatilia ili zahanati hizo ziweze kusajiliwa.
“Sababu inayotolewa kwamba ni lazima zahanati ziwe
na nyumba za wauguzi ndipo zifunguliwe hazina maana. Mbona walimu
wanapelekwa kwenye shule ambazo hazina nyumba? Hatuwezi kuwaacha
wananchi wateseke wakati zahanati zipo,” alisema Kinana.
Tumbaku
Tumbaku ni zao kubwa la biashara ambalo
linategemewa na wakazi wa mkoa huo, lakini katika miaka ya hivi karibu
limekuwa halina tija kwa sababu ya ufisadi wa baadhi ya viongozi wa
vyama vya ushirika mkoani humo.
Katika kipindi cha miaka miwili, wakazi wa mkoa huo wanadai Sh28 bilioni kwa vyama vya ushirika vilivyopo kwenye mkoa huo.
Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba anadai kuwakataza
wananchi kuuza tumbaku kwenye vyama hivyo kwa sababu ya ufisadi wa
viongozi kwa kuwa wanawakopa huku wakiwa hawana uhakika kama watawalipa
fedha hizo.
Nkumba anasema mwaka juzi, Wizara ya Kilimo,
Ushirika na Chakula ilifanya uchunguzi kuhusu tumbaku na kubaini ufisadi
mkubwa, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa licha ya ripoti hiyo
kutolewa. Waziri wa wizara hiyo, Christopher Hiza hajachukua hatua
zozote kuwawajibisha waliohusika na ufisadi huo.
Mkuu wa mkoa, Mwasa naye alipigilia msumari kwamba
Injinia Chiza ameshindwa kuwachukulia hatua mafisadi wa tumbaku, hali
ambayo inasababisha asieleweke kwa jamii.
Alisema wamefikia hatua ya kuwaruhusu wananchi
kuuza tumbaku yao popote penye soko ambalo litawapatia fedha bila
kukopwa. “Haiwezekani kuwa na watu wanaoishi Dar es Salaam ambao
wananufaika na tumbaku kwa ufisadi wakati wakulima wakiendelea kuwa
maskini kwa miaka mingi,” anasema.
Akizungumzia hilo, Kinana alisema matatizo ya
wakulima wa tumbaku ni ya muda mrefu na akaahidi kwamba tatizo hilo
linatakiwa kumalizika. “Nitakwenda kuzungumza na rais ili tatizo hilo
liweze kufikia kikomo, hatuwezi kuendelea na tatizo hili tena ni lazima
achukue hatua zitakazomaliza tatizo hili.”
Majengo yatelekezwa
Majengo saba ambayo yalitakiwa kujengwa vituo vya
afya chini ya mpango wa kunusuru vifo vya kinamama yametekekezwa bila
kumalizika katika zabuni iliyotolewa na Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii kwa mkandarasi, Humphrey Contractors wenye thamani ya Sh2 bilioni.
Nkumba alimweleza Kinana kwamba majengo hayo yapo wilayani Sikonge
lakini yameshindwa kukamilika. Anasema mkataba wa ujenzi huo ulikuwa
ukamilike tangu mwaka 2002 lakini hadi sasa yamebaki `mapagale’.
“Tunashindwa kufahamu nini kimetokea, wizara
imekaa kimya, mkandarasi haendelei na ujenzi, tumebaki tunashangaa,”
alisema. Kinana alishangazwa na kitendo cha wizara hiyo kuingia mkataba
na mkandarasi huyo badala ya kazi hiyo kufanya na Halmashauri ya Wilaya
ya Sikonge ambayo ingekuwa rahisi kufuatilia.
“Nashangaa watu wanavikubali vyeo wakati hawana
uwezo wa kuwatumikia wananchi, wanakaa ofisini wakati mambo huku
yanaharibika, kwa nini hawavikatai vyeo hivyo, hawa ndiyo aina ya
viongozi wanaofanya sherehe wakati wakiteuliwa huku wakiwa hawana uwezo
wa kufanya kazi,” alisema.
Kinana alisema atapambana hadi aone nini kilitokea
kwenye zabuni hiyo na kwamba atawajulisha wakazi wa Sikonge
atakapobaini ukweli.
“Nitapambana nao hadi kieleweke, kazi ya chama ni
kusimamia Serikali kutekelezaji ya ilani ya chama, kama kuna ufisadi
katika zabuni hii mtajulishwa na hatua zitachukuliwa,” alisema.
‘Nukuu’
Viongozi tuwe wasikivu kwenye matatizo ya watu