KITAIFA: MAGUFULI AWAWAKIA MAOFISA WA TANROADS WANAOHUJUMU TAIFA KWA KULA RUSHWA
https://jaridahuru.blogspot.com/2014/07/kitaifa-magufuli-awawakia-maofisa-wa.html
Mwanza. Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli amewajia juu maofisa wa Wakala wa Barabara (Tanroads) mkoani Mwanza baada ya kubaini wanataka kulipa fidia ya zaidi ya Sh100 milioni kutokana na uamuzi wao wa kupitisha barabara kwenye eneo lisilo katika mipango.
Hayo yalitokea jana wakati Waziri Magufuli
akihitimisha ziara ya ukaguzi wa barabara ya Usagara-Kisesa yenye urefu
wa kilometa 17.8. Magufuli alieleza kushangazwa na Tanroads kupitisha
barabara katika eneo la Halmshauri ya Wilaya ya Magu, hivyo kutakiwa
kulipa fidia na kuacha eneo la wazi ambalo halihitaji malipo.
Waziri Magufuli alisema kuna mbinu za kutaka
kujenga kituo cha mafuta kwenye eneo ambalo limeachwa wazi na Tanroads,
hivyo kuamuru barabara hiyo irejeshwe kwenye eneo lililopangwa.
Waziri Magufuli alisema hawezi kuvumilia kuona
barabara inachelewa kwa madai ya ulipaji fidia, huku maeneo ambayo
hayatakiwi kulipiwa fidia yanachwa wazi bila sababu za msingi.
“Ucheweshaji huu wa kipande hiki cha kilometa
tano, ni jambo la ajabu kuona mnaacha kupitisha barabara kwenye eneo
ambalo halina vikwazo vyovyote,” alihoji Dk Magufuli.
Dk Magufuli alisema anatambua kila kitu
kinachoendelea katika ujenzi wa barabara hiyo na suala la fidia
halifanywi kwa bahati mbaya.
“Hivi nyie mnadhani fedha za Serikali zinachotwa
tu… naomba majibu kwanini mmekuja kwenye eneo la halmashauri na kutaka
kulipa fidia wakati barabara ya zamani kuna eneo kubwa ambalo linatosha
bila kulipa hata senti tano? Mtambue kwamba barabara hii inajengwa na
fedha za Serikali zaidi ya Sh17 bilioni,” alisema na kuongeza:
“Au hizi nyumba mnazotaka kulipa fidia ni za ndugu
zenu. Nafahamu kuna mbinu ya kutaka kupitisha huku ili kule muache eneo
la ujenzi wa kituo cha mafuta. Kuanzia sasa naomba ujenzi huu urudi
kule.”
Awali, akisoma taarifa ya ujenzi, mkandarasi wa
madaraja, Elias Boniface alisema ujenzi wa barabara hiyo unaofanywa na
kampuni ya Nyanza Road Work Limited umekamilika kwa asilimia 37.5
Alisema barabara hiyo itakuwa kiunganishi cha magari yanayotoka nchi jirani kwenya Mkoa wa Mara na nchini Kenya.