BUNGENI: LISSU AWALIPUA TENA MAWAZIRI, ASEMA WANATUMIA FEDHA ZA SERIKALI KUJINUFAISHA KISIASA

https://jaridahuru.blogspot.com/2014/06/bungeni-lissu-awalipua-tena-mawaziri.html
Dodoma. Waziri wa Maji, Profesa Jumanne
Maghembe na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk
Binilith Mahenge, jana walituhumiwa kutumia vibaya nafasi zao kwa kuweka
fedha nyingi za miradi ya maji katika maeneo wanakotoka, huku sehemu
zenye matatizo ya huduma hiyo zikitengewa fedha kiduchu.
Ilielezwa bungeni jana kuwa Profesa Maghembe
ambaye ni Mbunge wa Mwanga, Kilimanjaro, wizara yake imetenga Sh1.4
bilioni kwa ajili ya miradi ya maji, ambazo ni zaidi ya mara saba ya
Sh190 milioni zilizotengwa kwa ajili hiyo katika Wilaya ya Ikungi,
Singida.
Akichangia Bajeti ya Wizara ya Maji jana, Mbunge
wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alihoji kile alichokiita
upendeleo wa wazi katika ugawaji wa fedha za maji, unaoipa kipaumbele
baadhi ya mikoa wanakotoka mawaziri.
Pia aliitaja Wilaya ya Makete, Njombe anakotokea
Dk Mahenge ambaye amewahi kuwa Naibu Waziri wa Maji kuwa imetengewa
Sh1.9 bilioni na kusema: “Upendeleo wa aina hii haufai kwa sababu
utaleta matatizo na siyo haki hata kidogo.”
“Profesa Maghembe atueleze sababu za kutenga
bajeti hii kwa upendeleo, huku mikoa isiyokuwa na vyanzo vya maji, mito
ya kudumu na mabwawa ya maana imepewa bajeti kidogo ikilinganishwa na
ile yenye mifumo mizuri ya maji,” alisema Lissu.
Alisema licha ya Profesa Maghembe katika hotuba
yake kutaja mikoa ya Dodoma, Singida, Simiyu na Shinyanga kuwa
inakabiliwa na upungufu wa maji, imetengewa kiasi kidogo cha fedha, huku
mikoa inayopata mvua za kutosha na vyanzo vya uhakika vya maji
ikitengewa mabilioni ya fedha.
“Dodoma imetengewa Sh7.2 bilioni, Singida Sh3.2
bilioni, Shinyanga Sh3.2 bilioni na Simiyu Sh2.8 bilioni, wakati mikoa
yenye vyanzo vya maji na mvua za kutosha imetengewa fedha nyingi; mfano
ni Tanga Sh10.7 bilioni, Kilimanjaro Sh6.3 bilioni, Mbeya Sh9.2 bilioni
na Mtwara Sh7.5 bilioni,” alisema.
Lissu alisema hali hiyo inaweza kutafsiriwa kuwa
mawaziri hao wanatumia mamlaka yao kujipendelea na kuhoji kama huo ndiyo
utaratibu wa Serikali ya CCM... “Kama utaratibu wa mgawanyo wa fedha
ndiyo huu sisi tunaotoka mikoa yenye ukame tutapataje maji?”
Jana Profesa Maghembe aliendelea kuwa katika
wakati mgumu, baada ya kuandamwa na Mbunge wa Ubungo (Chadema), John
Mnyika ambaye alimwita kuwa ni mzigo kutokana na kutokutolewa kwa fedha
za miradi ya maji.
Mnyika alionyesha kushangazwa na wabunge wenzake
kuunga mkono bajeti ya wizara hiyo, licha ya kuwa ndogo na fedha za
miradi zimekuwa hazitolewi kama inavyotakiwa.
“Kwa kufanya hivi sidhani kama tunamsaidia Profesa
Maghembe ambaye ni CCM. Fedha zilizotengwa mwaka jana kuisaidia wizara
hii hazijatoka na za bajeti hii hazitatoka kwa kiwango cha kuwezesha
utekelezaji. Namna bora ya kumsaidia ili viongozi wa CCM wasiendelee
kumwita mzigo ni kuikataa bajeti hii ili Serikali irudi mezani na
kujiuliza.”
Mnyika alisema kuwa hata ahadi ya Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda kuwa Serikali itaongeza Sh80 bilioni kwa wizara hiyo kabla
ya Mei 31 mwaka huu nayo haijatekelezwa na kusisitiza kuwa wabunge
wakiipitisha bajeti hiyo watakuwa wameuziwa mbuzi kwenye gunia.
Alisema kuwa hata miradi ya maji jijini Dar es Salaam ambayo
Profesa Maghembe aliahidi kuwa itakamilika mpaka sasa hakuna
kilichofanyika.
Mbunge wa Mbozi Magharibi (Chadema), David Silinde
alisema Profesa Maghembe amechota mabilioni ya fedha na kuyapeleka
katika miradi ya maji kwenye jimbo lake la uchaguzi wakati maeneo
mengine ameyaacha licha ya kuwa yana kipaumbele na kwamba anatumia
miradi ya Serikali kujinufaisha kisiasa.
“Ukitaka takwimu zote ninazo hapa, idadi ya watu
kwako ni wachache kuliko hata kwangu lakini kwa vipindi viwili mfululizo
umekuwa ukijitengea mabilioni ya fedha, wewe ni mzigo kabisa,” alisema
Silinde.
Mwandosya amtetea
Wakati akijibu hoja za wabunge, Profesa Maghembe
hakugusia tuhuma hizo na badala yake Profesa Mwandosya alimtetea akisema
miradi hiyo katika wilaya za Same, Mwanga na Korogwe ilianza wakati
yeye (Mwandosya) akiwa Waziri wa Maji... “Si kweli kwamba Profesa
Maghembe
anapendelea jimbo lake kwa sababu hakuwa waziri wa wizara hiyo wakati mradi huo unaanzishwa. Wananchi wa Same, Mwanga, Korogwe na Simanjiro wana haki ya kupata maji kama wananchi wa sehemu nyingine yoyote. Mwacheni waziri atekeleze majukumu yake ili watu hawa wapate maji”.
anapendelea jimbo lake kwa sababu hakuwa waziri wa wizara hiyo wakati mradi huo unaanzishwa. Wananchi wa Same, Mwanga, Korogwe na Simanjiro wana haki ya kupata maji kama wananchi wa sehemu nyingine yoyote. Mwacheni waziri atekeleze majukumu yake ili watu hawa wapate maji”.
Alisema mradi wa maji wa Same, Mwanga na Korogwe
ni muhimu sana kwa sababu utakuwa na uwezo wa kuhudumia zaidi ya watu
400,000 ambao hawapati maji kabisa.
Alisisitiza kuwa yuko tayari kubeba lawama juu ya
mradi huo na si Profesa Maghembe, kwani waziri huyo anafanya kazi nzuri
ya kutekeleza mradi huo ambao ulikuwapo hata kabla hajapelekwa katika
wizara hiyo.