ELIMU: WANAFUNZI SHULE ZA MSINGI SASA KUSOMA KWA 'LAPTOP', WAZIRI MKUU ATHIBITISHA TAYARI KWA BAADHI YA SHULE
https://jaridahuru.blogspot.com/2014/06/elimu-wanafunzi-shule-za-msingi-sasa.html
WAZIRI Mkuu, Bw.
Mizengo Pinda, amesema Serikali itaendelea kutatua changamoto
zinazokabili sekta ya elimu nchini kwa awamu ambapo hivi sasa, wanafunzi
wa darasa la kwanza hadi la saba katika baadhi ya shule, wameanza
kutumia kompyuta mpakato (laptop), zilizounganishwa na vitabu vyote
wanavyopaswa kuvisoma wakiwa shuleni.
Bw. Pinda aliyasema
hayo bungeni Mjini Dodoma jana katika kipindi cha maswali ya papo kwa
papo na kusisitiza kuwa, kompyuta hizo zitawasaidia wanafunzi kutobeba
mzigo wa vitabu
Majibu ya Bw. Pinda
yalitokana na swali aliloulizwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Bi. Mariam
Msabaha (CHADEMA), aliyetaka kujua ni lini wanafunzi wa shule za
Tanzania watatumia kompyuta mpakato darasani kama ilivyo kwa wanafunzi
wa nchi jirani ya Kenya.
Akijibu swali hilo, Bw.
Pinda alisema changamoto zinazoikabili sekta ya elimu ni nyingi hususan
nyumba za walimu, madarasa ambapo kwa hivi sasa hitaji kubwa lipo zaidi
kwenye shule za sekondari.
“Changamoto hizi
zinaendelea kufanyiwa kazi...Serikali imechukua maamuzi makubwa juu ya
suala hili lakini pia ni lazima Bajeti ya Wizara ya Elimu izidi kukua
ili tuendelee kuzifanyia kazi,” alisema Bw. Pinda.
Upinzani wakubali hoja
Katika hatua nyingine,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, jana imeunga mkono hoja iliyotolewa
bungeni na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Bi. Jenista
Mhagama kuhusu Chuo cha Ustawi wa Jamii Tengeru kuwa taasisi
inayojitegemea.
Kwa nyakati tofauti,
baadhi ya wabunge wa upinzani waliunga mkono hoja hiyo na kuitaka
Serikali iangalie jinsi ya kuzitatua changamoto zilizopo katika chuo
hicho likiwemo tatizo la ardhi na kujenga maktaba.
Kwa upande wake, Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Bw. Stephen Wassira,
alisema inafurahisha kuona upinzani wananga mkono hoja hiyo lakini
wasiiachie Serikali pekee kutatua changamoto zilizopo.
Alisema jambo la msingi
ni jinsi gani wahitimu wa chuo hicho wataweza kutumika kwenye jamii ili
kuleta maendeleo nchini ambapo kuwatumia watu hao ni kitu cha msingi.
Mbunge wa Viti Maalumu,
Bi. Cecilia Pareso (CHADEMA), naye aliunga mkono hoja ya chuo hicho
kujitegemea ili kiweze kutoa wataalamu wa maendeleo ya jamii ambao wengi
wao ndio wanaosimamia miradi mingi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii
(TASAF).
“Mimi ni mjumbe katika
kamati hiyo iliyokwenda kuangalia mazingira ya chuo hiki...baada ya ombi
hili kukubalika tunataka bodi iundwe haraka kwani kumekuwa na
ucheleweshaji wa kuundwa kwa bodi katika maeneo mengi.
“Pia tatizo la ardhi
katika chuo hiki, lipatiwe ufumbuzipamoja na kuweka miundombinu...sh.
bilioni moja zinahitajika ili kujenga maktaba ya kisasa,” alisema
Pareso.
Mbunge wa Iringa Mjini,
Mchungaji Peter Msigwa (CHADEMA), alisema kwa mara ya kwanza anaunga
mkono hoja bila tatizo ambapo vyuo kama hivyo vinapaswa kutumika kwa
kubadili fikra tofauti.
Wabunge wengine
waliuunga mkono hoja hiyo ni Bw. Moses Machali na Bw. Kombo Khamis Kombo
ambao licha ya kuunga mkono hoja, walitaka kujua ni jinsi gani Serikali
itahakikisha chuo hicho kitapata fedha za kutosha ili kiweze
kujiendesha chenyewe.
Imechapishwa na
Sebastian