BUNGENI: SUGU ALIPULIWA TENA, WASEMA HAJUI HISTORIA WALA HANA UZALENDO, NI BAADA YA KUHOJI MBIO ZA MWENGE
https://jaridahuru.blogspot.com/2014/06/bungeni-sugu-alipuliwa-tena-wasema.html

KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Bi. Rachel Kasanda, amemshukia Mbunge wa Mbeya Mjini, Bw. Joseph Mbilinyi kwa jina maarufu ‘Sugu’, (CHADEMA), akipinga kauli yake aliyoitoa bungeni Mjini Dodoma, Mei 20,2013 akitaka Mwenge huo uwekwe Jumba la Makumbusho kama sehemu ya kivutio cha utamaduni badala ya kuzungushwa nchi nzima.
Katika hotuba yake aliyoitoa bungeni, Bw. Mbilinyi alidai Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, imekuwa ikihoji maana nzima ya kutumia mabilioni ya walipa kodi maskini kwenye mbio za mwenge badala yake fedha hizo ziingizwe katika programu za maendeleo ya vijana waweze kujiajiri
Wakati Mwenge huo ukianza mbio zake mkoani Mbeya, Kasanda alipingana na hotuba ya Bw. Mbilinyi na kusisitiza ni vyema mbunge huyo ajinyonge ili mwili wake uwekwe makumbusho.
Akionesha kukerwa na maneno hayo, alisema ni wazi Bw. Mbilinyi ameonekana hajui historia ya nchi na hana chembe ya uzalendo.
Alisema mapokezi makubwa yaliyofanywa na wakazi wa jiji hilo katika Uwanja wa Shule ya Gombe, yanaonesha wapigakura jimboni humo hawakumtuma mbunge huyo kwenda kuutukana Mwenge bungeni.
“Alichokifanya Bw. Mbilinyi kimeonesha uwezo wake mdogo alionao, lazima Watanzania wafahamu tulikotoka ambapo Mwenge huu uliwashwa kwa lengo la kuondoa utawala wa wakoloni Waingereza na sisi kupata Uhuru wa kujiamulia mambo yetu kwa amani, utulivu na mshikamano.
“Hayati Mwalimu Julius Nyerere wakati akiuwasha Mwenge, alisema maneno mazito kuwa, sisi tumekwisha kuuwasha Mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro umulike hata nje ya mipata yetu, ulete tumaini pale ambapo hakuna matumaini, upendo mahali pale ambapo kuna chuki na heshima mahali ambapo pamejaa dharau,” alisema Kasanda.
Aliongeza kuwa, maneno hayo yanaonesha jinsi ambavyo Mwenge huo ulivyo na maana kubwa katika kuhakikisha Tanzania inakuwa huru ikiwa imeondoa vikwazo vyote hivyo kitendo cha Bw. Mbilinyi kutaka uwekwe makumbusho ni kutojua historia ya Tanzania ilikotoka na inakoelekea.
Naye Mkimbiza Mwenge Kitaifa, Bw.Wito Mlemela, alisema anafahamu kuwa Mkoa huo una watu wenye upendo na makini hivyo maneno ya Bw. Mbilinyi, yanapaswa kupuuzwa kwani hajui historia.
Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Bi. Rosemary Senyamule, alisema wakazi wa jiji hilo wanaipenda Serikali yao ndiomaana wamejitokeza kwa wingi ambapo Mwenge huo utazindua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi yenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni moja.
Chanzo:Majira
Imechapishwa na
Sebastian