https://jaridahuru.blogspot.com/2014/06/bungeni-jinsi-bunge-maalum-la-katiba.html
Dar es Salaam. Mbali na kubaki ‘njia panda’ ,
kuna baadhi ya Watanzania ambao wanaamini mshale wa saa bado unaendelea
kuonyesha dalili na matumaini ya kupatikana kwa Katiba Mpya.
Hatua hiyo inatokana na safari ndefu ya takriban
miezi 26 tangu Mchakato wa Katiba uanze Aprili 6, 2012, huku hatua
mbalimbali zikipitiwa, ikiwamo ukusanyaji wa maoni ya wananchi.
Hata hivyo, hatua iliyobaki inasubiria sala na
jicho la imani kutokana na upande wa kundi moja la Wajumbe wa Bunge la
Katiba (Ukawa), kutofahamika kwamba utarejee bungeni au la.
Hiyo imetokana na mvutano uliojitokeza wakati wa
mjadala wa sura mbili tu za awali, zinazopendekeza Muundo wa Muungano wa
Serikali tatu.
Mpasuko huo wa Wajumbe wa Bunge la Katiba, umeenda
mbali zaidi na kuwagawa Watanzania ambao nao wako njia panda kuhusu
uwezekano wa kupatikana kwa katiba hiyo mpya wanayoitazamia.
Makundi yanayoonekana kuwa njia panda ni yale ya
wanaharakati, vyombo vya habari, wanasiasa nguli na wasomi
wanaotegemewa. Wanasiasa ndiyo waliofanikiwa kuuteka mchakato huu.
Vyombo vya habari
Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo, Tanzania kuna vituo 93 vya redio, 28 vya
televisheni na magazeti 537 yenye mitazamo, sera, itikadi tofauti.
Katika mchakato huo, vyombo vya habari vilianza
kuripoti katika mitazamo mbalimbali inayolenga kuelimisha, kukosoa juu
ya kila hatua inayojitokeza. Hata hivyo, mjadala huo wa Katiba
ulipofikia sasa umewezesha kujenga mpasuko mkubwa miongoni mwa
wanahabari kama ilivyo kwa wanasiasa na makundi mengine.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Vyombo vya Habari
Tanzania (TMF), Ernest Sungura anasema inasikitisha kuona mwandishi wa
habari anapoyumbishwa na itikadi za kisiasa.
Sungura ambaye pia ni mwandishi nguli anaongeza
kuwa taaluma ya habari ina msingi pekee wa kusimamia, kueleza watu
ukweli katika jambo lolote linalojitokeza kwenye jamii.
“Tulitegemea kuona nafasi hii ya mjadala wa Katiba
waandishi ndiyo wajikite kuchambua, kutueleza ukweli, lakini wameingia
kwenye mitego ya wanasiasa,” anasema na kuongeza:
“Mwandishi unaweza kuandika kama maoni yako kupitia kolamu, yawe
ni mawazo yanayoeleza ukweli pia lakini inapofikia hatua ya kuandika
hoja za muundo wa serikali lazima kuhakikisha unaandika bila upendeleo
na kwa usawa.”
Aidha, anabainisha kwamba, waandishi kuajiriwa
katika vyombo vyenye itikadi, sera na mitazamo tofauti ni moja kati ya
sababu kuu iliyosababisha kuyumbishwa kitaaluma.
Wasomi
Wasomi nao wamekuwa wakitazamwa kwa jicho la
kuleta mapinduzi kwa jamii ya Watanzania. Lakini nao wamejikuta
wakisambaratishwa na kujikuta wakigawanyika makundi mawili. Wanaopingana
na rasimu iliyopendekeza Serikali tatu na wanaoiunga mkono rasimu hiyo
ya tume.
Pamoja na elimu yao, masilahi ya wanasiasa
yamepenyeza kwa wanasheria ambao wamekuwa wakiendea kutofautiana
kimtazamo juu ya uhalali wa kisheria katika Mkataba wa Muungano .
Mchakato huo wa Katiba pia umewasambaratisha
wachumi kupitia kipengele hicho cha Muundo wa Serikali. Wenyewe
wanagawanyika wakishindanisha hoja zao kuhusu gharama za uendeshaji wa
serikali hizo.
Viongozi wa dini
Katika hatua ya kushangaza zaidi hata viongozi wa imani mbalimbali za dini wamejikuta kwenye mpasuko wa makundi mawili.
Viongozi hao wa dini kutoka madhehebu ya Kikristo
na Kiislamu wameonyesha mitazamo tofauti katika kutafuta ukweli juu ya
muundo gani wa serikali ambao unafaa kwa Watanzania ndani ya Katiba
ijayo.
Kuna baadhi ambao wanaonyesha msimamo wao juu ya
maoni ya rasmu ya Katiba, huku wengine wakiunga mkono hoja za upande wa
serikali mbili, zinazopigiwa chapuo na CCM.
Wanaharakati
Kundi la wanaharakati ni miongoni mwa Watanzania
waliojizolea umaarufu na imani kubwa kwa wananchi. Katika kundi hilo pia
kuna wasomi, viongozi wa mashirika, asasi na taasisi za kijamii.
Hata hivyo, kwa bahati mbaya zaidi nao wamegawanyika.Mhadhiri wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally anasema inasikitisha kuona
fikra za wanaharakati zinageuzwa na masilahi ya wanasiasa.
Anasema kundi hilo limefika pabaya kutokana na
kujihalalishia kibali cha kutafuta ukweli kuhusu Mchakato wa Katiba,
huku wakiwa wamefunikwa na mkono wa masilahi ya wanasiasa.
“Mimi nimekuwa nikiogopa hata kuzungumza kutokana
na mazingira hayo, lakini kuna tofauti kubwa kati ya kutofautiana
mitazamo na mpasuko, kinachoonekana kwa sasa ni mpasuko unaotokana na
upotoshwaji kabisa,” anasema Bashiru na kuongeza:
“Watanzania hawawezi kujadiliwa hoja zao.
Kilichobakia wanaharakati wanatumikishwa kwa rushwa na makundi hayo ya
wanasiasa, tungewaachia wananchi wenyewe, wala tusiingilie na kupotosha
ukweli. .