BUNGENI: BAJETI KUU YA SERIKALI 2014/2015 HATIMAYE YAPITISHWA

https://jaridahuru.blogspot.com/2014/06/bungeni-bajeti-kuu-ya-serikali-20142015.html
Dodoma. Bajeti Kuu ya Serikali ya 2014/15
imepitishwa jana bungeni mjini hapa na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya
akisema lazima wafanyabiashara walipe kodi inayostahili na iwapo kuna
anayedhani anapata hasara kwa kulipa kodi afunge biashara.
Akihitimisha mjadala wa bajeti hiyo kabla ya umeme
kukatika wakati wa upigaji kura kuipitisha, Mkuya alisema kama
mfanyakazi anatozwa kodi, mfanyabiashara anayepata faida hataachwa.
“Mfano hata hapa Dodoma wanakuja kuzungumza na
ninyi wabunge ili kuanza kuwafanyia ushawishi ili muwasaidie katika
kukwepa kodi, hilo haliwezekani,” alisema.
Alikemea wizi wa fedha za umma unaofanywa na
watumishi wa Serikali akisema unaumiza taifa na kuifanya Serikali ipate
hasara kubwa.
“Mfano kuna wakati mtu mmoja alileta taarifa za
kuidai Serikali Sh600 milioni, lakini tulipokwenda kuhakiki tukagundua
kuwa alikuwa anadai Sh600,000 tu, sasa wabunge tunaposema kuna wizi,
basi lazima muamini kuwa huo ndiyo wizi wa mali ya umma,” alisema Mkuya.
Alisema uhakiki huo ulipunguza deni la taifa kutoka Sh19 bilioni hadi Sh5 bilioni ambalo ndilo deni halisi kwa wadai wa ndani.
Mkuya alisema kuanzia sasa, Serikali haitalipa
fedha zozote za deni hadi uhakiki ufanyike kwa kuwa wizi umezidi ikiwamo
katika ununuzi wa magari na sasa hakutakuwa na taasisi itakayoruhusiwa
kununua magari yake hadi kwa kibali maalumu cha Hazina na yote
yatanunuliwa kwa pamoja kutoka kwa mzalishaji bila kupitia mawakala.
“Katika hilo tumejipanga pia kuhakikisha kuwa hatupeleki fedha katika taasisi zozote ambazo hazitaleta ripoti ya utekelezaji.”
Kuhusu suala la mikopo, alisema kuwa Tanzania
itaendelea kukopa kwa ajili ya maendeleo kwa kuwa deni la taifa
linahimilika kwa vyanzo vyake vyote, hivyo kusema wasikope siyo sahihi.
Akizungumzia suala la magari chakavu ambalo
lilipigiwa kelele na wabunge wengi, alisema msimamo wa Serikali utabaki
hivyo kwamba magari yanayoanzia umri wa miaka minane na kuzidi ni lazima
yatozwe ushuru mkubwa.
Alisema wamefanya hivyo baada ya kubaini kuwa
Tanzania imefanywa kuwa dampo la kutupa magari mabovu kutoka maeneo
mbalimbali duniani.
Alisema baada ya kubaini kuwa magari yaliyozidi
muda huo yamepandishwa kodi hapa nchini, bei za magari ya Toyota nchini
Japan zimeshuka.
Awali, Kamati ya Bajeti ililieleza Bunge kwamba Serikali
imeridhia kuongeza Sh115 bilioni kwa ajili ya kujazia fedha zilizopungua
kwa wizara mbalimbali.
Akizungumzia misamaha ya kodi, Naibu Waziri wa
Fedha, Mwigulu Nchemba alisema lengo la kufuta kwa misamaha ya kodi
isiyo na tija ni kuiongezea Serikali mapato na siyo kufukuza wawekezaji
nchini.
Akiwasilisha mapendekezo ya Kamati ya Bajeti,
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk Festus Limbu alisema Sh8.2 bilioni
ziliongezwa katika Wizara ya Mambo ya Ndani kwa ajili ya maboresho ya
Jeshi la Polisi ili kuimarisha mafunzo na vitendea kazi.
“Sh14.4 bilioni zimeongezwa kugharimia mahitaji ya
ziada ya kuhamisha makato ya kodi ya mishahara Zanzibar kutoka Ofisi ya
Makamu wa Rais, Sh16 bilioni zimeongezwa katika Wizara ya Mambo ya Nje
kwa ajili ya kugharimia mahitaji mapya ya Balozi za Comoro, The Hague
pamoja na safari za viongozi,” alisema Dk Limbu.
Alisema Sh13.7 bilioni zimeongezwa katika Wizara
za Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Kitengo cha Ngome kwa ajili ya
kulipa posho na Sh12.45 bilioni zimeongezwa katika Mfuko wa Bunge kwa
ajili ya kugharimia Bunge la Katiba.
“Sh5. 8 bilioni zimeongezwa Tamisemi kwa ajili ya
kugharimia matengenezo ya barabara, Sh1.25 bilioni zimeongezwa katika
Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo kwa ajili ya kulipia deni la
Televisheni ya Taifa (TBC), Bunge na maadhimisho ya sherehe za Muungano.
Wizara ya Ujenzi imeongezewa Sh43.36 bilioni kugharimia matengenezo ya
barabara,” alisema.