BUNGENI: MUHONGO AIAGIZA REA IWATIMUE WAKANDARASI WAZEMBE IFIKAPO MWEZI JULAI

https://jaridahuru.blogspot.com/2014/06/bungeni-muhongo-aiagiza-rea-iwatimue.html
Dodoma. Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ameiagiza Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) kuwafutia mikataba makandarasi wote ambao watakuwa hawajaanza kazi ifikapo Julai Mosi, mwaka huu.
Profesa Muhongo alisema hayo bungeni jana akijibu
hoja mbalimbali za wabunge zilizotolewa wakati wakichangia Bajeti ya
Serikali kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
“Napenda kutoa agizo kupitia Bunge lako kuwa
ikifika Julai Mosi mkandarasi ambaye atakuwa hajaanza kazi, Rea lazima
wamtoe waweke mwingine,” alisema Profesa Muhongo.
Aidha, aliwataka mameneja wa Shirika la Umeme
Tanzania (Tanesco), kuhakikisha kuwa wateja wanaoomba kufungiwa umeme
katika vijiji vilivyopo pembezoni mwa miji hawatozwi gharama za
kuunganisha umeme za mijini.
“Vijiji vilivyoko pembezoni mwa miji ni wale watu
wana mazizi ya ng’ombe, wana makaburi ya wazee wao, naomba wale wapewe
umeme kwa gharama za wanavijiji,” alisema. Alisema gharama za
kuwaunganishia wateja hao katika awamu ya pili ya Rea ni Sh27,000 na
Sh5,000 kwa ajili ya ada ya fomu ya maombi.
“Hakuna rushwa, hakuna hongo na kampuni ambayo
italetwa wizarani kuwa wafanyakazi wake wameomba rushwa itanyang’anywa kazi na tumeshakubaliana hivyo,” alisema.
Wachimbaji wadogo kupewa ruzuku
Kuhusu wachimbaji wadogo wa madini, Profesa
Muhongo, alisema Serikali katika bajeti ya mwaka huu, itawapa wachimbaji
wadogo wa madini ruzuku ya Dola za Marekani 50,000 (Sh80 milioni)
ambazo hawatatakiwa kuzirejesha.
“Nendeni mkawaambie wachimbaji wadogo kuwa wakati
wa neema ni sasa... Tunawapatia bure tunataka waboreshe uchimbaji wao,”
alisema.
Mwakyembe kicheko
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe
amewataka wabunge kuwapongeza mawaziri wa fedha kwa sababu fedha zote
walizoomba kwa ajili ya utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa
(BRN), kwenye sekta ya reli zimetolewa.\
“Nilitarajia katika mkutano huu Waziri wa Fedha na manaibu wake
wapongezwe kwelikweli kwa kufanikisha miradi yote ya BRN ambayo kwa
kweli imekwenda kwa asilimia 95,” alisema na kuongeza:
“Wamefanya hivyo si kwa kuipendelea wizara ila kwa
sababu ya kutambua kuwa sekta ya uchukuzi ni muhimu katika kuleta
mabadiliko ya uchumi nchini.”
Dk Mwakyembe alisema Shirika la Reli
lilipobinafsishwa halikuleta mafanikio kama mashirika mengine na ndiyo
maana Serikali iliamua kulichukua.