https://jaridahuru.blogspot.com/2014/08/katiba-warioba-na-tume-yake-waianika.html
JANA taifa lilisimama saa nne kwa Watanzania kuelekeza masikio na
macho kwenye runinga kusikiliza ufafanuzi wa wajumbe wa iliyokuwa Tume
ya Mabadiliko ya Katiba, juu ya upotoshaji wa viongozi waandamizi wa
serikali kuhusu mapendekezo yaliyomo kwenye rasimu ya katiba mpya.
Wajumbe wa yume hiyo wakiongozwa na Jaji mstaafu Joseph Warioba,
waliwataja viongozi hao kuwa ni Stephen Wassira, William Lukuvi, Anna
Tibaijuka na Mwigulu Nchemba katika mdahalo wa katiba mpya uliofanyika
Ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam, uliondaliwa na Taasisi ya
Mwalimu Nyerere na kurushwa na runinga ya ITV.
Jaji Warioba, alianza kwa kuweka hadharani namna watu wenye
propaganda za mfumo wa serikali mbili wanavyopotosha maana nzima ya
rasimu ya pili ya tume hiyo inayoelekeza mfumo wa serikali tatu.
Alisema watetezi wa serikali mbili, wamejikita kuelezea upungufu wa
serikali tatu huku wakiacha mazuri ya muundo huo pamoja na udhaifu wa
serikali mbili za sasa.
Jaji Warioba, alikanusha kauli iliyotolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu, Sera na Bunge, William Lukuvi, kuwa kuna maoni mapya
yamewasilishwa serikalini.
Alisema hajabadilika katika msimamo wake wa kutetea serikali tatu
kama wananchi walivyotaka, na kwamba kinachofanywa na wanaoeneza maneno
hayo ni uzushi wenye malengo maalum.
Alifafanua kuwa kilichofanywa na wao ni kupeleka serikalini yale
mambo ambayo waliyachuja na ambayo yasingekuwa na nafasi katika Serikali
ya Muungano zaidi ya kusubiri Katiba ya Tanganyika.
“Sijabadilika, na jambo la msingi ni kwamba yale tuliyoyachuja badala
ya kutupa tulisema tukakabidhi serikalini kwa ajili ya kusaidia kuwa
kumbukumbu kwao pale watakapoona wanakwama, lakini muhimu hayo
wanayosema tumepeleka kuonyesha kuwa tumebadilika ni vema waweke
hadharani,” alisema Jaji Warioba.
Alisema bado kuna haja ya viongozi kuendelea kuvumiliana na kutafuta
maridhiano yatakayozaa katiba bora ya Watanzania, huku akibainisha kuwa
hata wao walikuwa na tofauti zilizomalizwa kwa kuangalia maslahi ya
taifa badala ya makundi waliyotoka.
Kwamba kabla ya Bunge la Katiba kuanza, aliwashauri viongozi wa vyama
vya siasa kukutana na kukubaliana baadhi ya mambo, na kwamba viongozi
hao hawakuweza kufanya jambo hilo, hali iliyozalisha matokeo ya sasa ya
mchakato ulipofikia.
Jaji Warioba alikataa dhana ya wanasiasa na wachambuzi mbalimbali
wanaotaka Bunge hilo liahirishwe kwa muda kuchagua baadhi ya mambo
yatakayofanyiwa maboresho huku yakitajwa kuwa ni kuboresha Tume ya
Uchaguzi na kutoa fursa kwa mgombea binafsi.
Alisema, haafiki mambo hayo kuwa kipaumbele na kuachwa kwa mambo muhimu ya wananchi.
Aliyataja baadhi ya mambo muhimu ya kujadiliwa mbali na masuala ya
uchaguzi, kuwa ni pamoja na suala la uwazi na uwajibikaji, kwa madai
kwamba huwezi kuwa na utawala bora kama hakuna uwazi na uwajibikaji.
Pia, alisema suala la maadili na tunu ya taifa ni mambo ambayo
wananchi walizungumzia sana na haki za binadamu ambako walitaka kuwekwa
kwa utaratibu wa utekelezaji kwa kuwa hata zilizopo hazitekelezeki.
Aidha, Jaji Warioba aliwashangaa wale wanaohangaika na takwimu,
lakini akasisitiza kuwa itambulike wajumbe wa tume ndio waliozunguka
mikoani na kuzungumza na wananchi na kuna mengi yalisemwa kwa uwazi
kabisa ambayo wengi hawayajui.
Paramagamba aonya
Kwa upande wake, Profesa Paramagamba Kabudi akichangia katika mjadala huo, aliasa kuzingatia utu na kuheshimu mawazo ya wengine.
Alisema kwa upande wake, hawahofii Wazanzibar kwa kuwa wao wanayo
mambo yao na yanayojulikana, na kwamba Watanganyika mambo yao
wameyaficha mioyoni, jambo aliloeleza kuwa ni hatari kama hawatapatiwa
mahitaji yao mapema.
Alisema kwamba ni wakati muafaka hivi sasa Watanganyika wakapewa
serikali yao wakiwa wanaidai kwa amani, badala ya kusubiri waongezeke na
kuidai kwa nguvu.
“Ni busara kuwapa Watanganyika serikali yao wakati wanaiogopa, badala
ya kusubiri waidai wakati wakiwa wengi na muda wa kuwaongoza ukiwa
haupo,” alisema Profesa Kabudi na kutoa mfano wa Baba wa Taifa, Mwalimu
Nyerere, ambaye wakati wa mchakato wa taifa kuingia mfumo wa vyama vingi
miaka ya 90 mwanzoni, licha wakati ule waliokuwa wakitaka vyama vingi
walikuwa wachache, alivikubali, kwani alijua ni bora kuliko waliokuwa
wakiunga mkono wangepuuzwa na kuja kuvidai kwa nguvu.
Kuhusu muundo wa rasimu, Profesa Kabudi alisema inatoa fursa ya rais
wa muungano kushitakiwa kwa uhaini kama atakiuka mambo yaliyoamuliwa na
mahakama ya muungano.
Alisema tatizo kubwa lililopo, ni kwa watu waliojivika upumbavu
kushupalia kila jambo hata kama hawana uwezo nalo, wakiamini nguvu
zitawalinda huku akisisitiza kuwa, hakuna aliye mkubwa juu ya sheria.
Butiku amshangaa rais
Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, kwa upande
wake alieleza kuwa Rais Kikwete alipokubali mchakato wa katiba na kuunda
tume, hakuwa na mamlaka ya kuiingilia tena.
Alisema jambo la msingi ni wahusika kufuata kile kilichokusanywa kwa
wananchi na kuheshimu, badala ya yale wanayoyakwaza kwenda kupata
ushauri ndani ya chama.
“Ninyi simamieni kile mnachoamini kilichokusanywa na tume, hapa
hakuna nani wala nani, hata Wassira hayupo, watu wanasema tume imesema
uongo, lakini tunajua namna umri wetu ulivyo, tutasema uongo kwa ajili
ya nini, huu mchakato ni wa wananchi,” alisema Butiku.
Alisema katika mazingira ya sasa wanapoamua kusema wanaitwa
wachochezi, na kwamba wananchi wanapaswa watafakari kwanini baadhi ya
vitabu walivyokusanyia maoni vimefichwa na tovuti ya tume imefungwa.
Aliongeza kuwa Jaji Warioba anaficha baadhi ya mambo, ikiwamo kueleza
wazi kuwa kutungwa kwa katiba ya Zanzibar ya 2010 kulivunja uwepo wa
muungano.
Alipoulizwa kama hotuba ya Rais Kikwete aliyoitoa bungeni iliharibu
mchakato mzima wa Katiba Butiku, alisema nchi ina Rais na anaheshimiwa
sana na kwamba heshima ina pande mbili huku akizitaja kuwa njia mojawapo
ya kumheshimu rais ni kutokuficha ukweli na kwamba upande wa pili ni
heshima ya kuficha ukweli.
Alisema mtu atakayeficha ukweli atakuwa hamuheshimu rais, na kwamba
kitendo cha kusema hakushauriana na tume kinapaswa kifikiriwe kwa makini
kwa kuwa wao walishauriana nae vya kutosha.
Butiku alisema rais anapaswa kuheshimiwa na hata eneo alilotolea
kauli hiyo linapaswa kuheshimiwa, na kwamba muhimu Watanzania wajue kuwa
walishauriana kwa kina.
Polepole afichua siri
Aliyekuwa mjumbe wa tume hiyo, Humphery Polepole, alisema wakati
wakikusanya maoni, viongozi mbalimbali wa kiserikali waliojitokeza mbele
yao walitaka muundo wa serikali tatu na hata tasisi wanazozisimamia
zilibainisha umuhimu wake.
Alizitaja taasisi hizo kuwa ni Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano, Tume
ya Makatibu na Viongozi wa Serikali ya Zanzibar, pamoja na Ofisi ya
Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
Alisema anapowaona baadhi ya viongozi waliotoa maoni ya serikali tatu
wanavyotumia nguvu ya kutaka serikali mbili wakiwa hadharani,
anashindwa kuwaelewa wana dhamira gani kwa Watanzania.
Kuhusu gharama za Serikali ya Muungano, Polepole alisema hakuna
gharama kubwa zaidi ya kupunguza matumizi na kubainisha kuwa haziwezi
kuzidi sh trilioni 2.
Awadh Said ashangaa madai ya gharama
Mwanasheria Awadh Said ambaye naye alikuwa mjumbe wa tume hiyo,
alisema anashangazwa na watu wanaokimbilia takwimu na gharama katika
suala zima la rasimu huku wakishindwa kuainisha idadi ya wabunge
watakaopungua kwa kupatikana serikali tatu.
Alisema muundo mzima wa wabunge wote wa muungano kwa sasa una watu
434 na kwamba katika Serikali ya Muungano iliyopendekezwa idadi hiyo
itapungua kwa wabunge 100.
Kwamba tume haikuelekezwa ichukue takwimu bali uzito wa hoja, na kwamba hoja zilizotolewa ndizo zimezaa rasimu iliyopo.
“Nashangaa wengine wanajiita wachumi huku wakishindwa kuona namna
gharama zitakavyopungua katika muundo wa serikali tatu, lakini katika
hali ya sasa wanapaswa watuambie ni wizara gani inayofanya kazi yake
Zanzibar ukiacha zile za muungano na sana sana ile ya Mambo ya Ndani,”
alisema huku akihoji kama Wizira ya Nyumba na Maendeleo ya Makazi
imewahi kwenda kusimamia maendeleo ya ardhi Zanzibar.
Aliongeza kuwa kwa sasa Zanzibar inajisimamia kwa masuala mbalimbali,
ikiwamo ardhi, hivyo kusema uwepo wa serikali tatu ni gharama ni
kuudanganya umma.