IMANI: KANISA LA MORAVIAN LAENDELEZA TIMUATIMUA, LAWATIMUA WACHUNGAJI 18 WA KANISA HILO KWA UTOVU WA NIDHAMU

ASKOFU wa Kanisa la Moravian Tanzania, Jimbo la Kusini, Dk. Lusekelo Mwakafwila, amewavua uchungaji waamini 18 wa kanisa hilo baada ya kuridhika kwamba walikaidi uamuzi halali wa Sinodi na kufanya uasi dhidi ya katiba yao.
Wachungaji hao ni Mosted Kibona, Alinanuswe Mwakilema, Fred Mwakyusa, Anyasime Kasebele, Fanny Ndemange, Dk. Clement Fumbo, Noel Mwakalinga na Mariam Kasendeka.
Wengine ni Azaria Lwaga, Nyambilila Lwaga, Eliza Kipesile, Lugano Anganisye, Baraka Mwakijale, Tumaini Lwinga, Emaus Bandikile, Angelina Mwamakula, Kenedy Kalagho pamoja na Nobert Namwinga.
Taarifa ya Askofu Mwakafwila, iliyotolewa mwishoni mwa mwezi uliopita, ilieleza kuwa uamuzi huo ni wa kikatiba kulingana na mamlaka aliyonayo.
“Wachungaji hawa wameendelea kufanya ukaidi na dharau dhidi ya kiti cha askofu, walikataa wito wa kuhudhuria vikao mbalimbali kikiwemo kikao cha sinodi ya dharura iliyofanyika mkoani Morogoro Desemba 26-29 mwaka jana,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Wachungaji hao hawatatakiwa kushiriki shughuli za kanisa kama wachungaji, badala yake watakuwa waamini wa kawaida.