https://jaridahuru.blogspot.com/2014/08/jamii-operesheni-bodaboda-jijini-dar.html
OPERESHENI ya kukamata pikipiki maarufu kama bodaboda zinazoingia
katikati ya Jiji la Dar es Salaam, imedaiwa kuhatarisha maisha ya watu
kutokana na polisi kutozingatia usalama wa wapanda pikipiki hao
wanapowakamata na kuwasababishia ajali.
Baadhi ya waandishi wa habari walishuhudia kamata kamata hiyo
iliyolalamikiwa na baadhi ya wananchi katika makutano ya Mtaa wa Garden
na Azikiwe, Manispaa ya Ilala jana, huku ikisimamiwa na Kamanda C.N
Maro.
Ajali hizo zimekuwa zikitokea kutokana na polisi kuwakimbiza wapanda
pikipiki hao na kuwavuta kwa nguvu kutoka kwenye pikipiki huku wakiwa
kwenye mwendo kasi pindi inapotokea mhusika amekataa kusimama.
Baada ya kukamatwa, mhusika hufungwa pingu kwa kuunganishwa na
pikipiki yake na kuamriwa akae chini, kitendo kilicholalamikiwa, kwamba
ni ukiukwaji wa haki za binadamu.
Katika eneo hilo, zilikamatwa zaidi ya pikipiki 50, kati ya hizo
zikiwemo za baadhi ya kampuni na raia wa kawaida, ambazo zilikuwa na
vibali vya kuingia katikati ya jiji.
Hata hivyo, polisi hao walikataa kuwasikiliza kwa madai hawana
taarifa kuwa kuna vibali vinavyoruhusu pikipiki kuingia katikati ya
jiji.
Polisi hao, pia walimkamata na kumfunga pingu mtu mmoja ambaye jina
lake halikuweza kupatikana mara moja, kutokana na kuhoji utaratibu
uliokuwa ukitumika kuwa haukuzingatia usalama wa wahusika ambao
ungeweza kuwaletea madhara.
Katika hali isiyotarajiwa, polisi hao walimgeuzia kibao mtu huyo kuwa
alimpiga askari na kumfanya ashindwe kufanya kazi yake wakati haikuwa
kweli.
Waandishi walipofika katika eneo hilo kutaka kupatiwa ufafanuzi
kuhusu askari hao kuendesha operesheni hiyo kikatili huku wakiwa peke
yao bila mgambo wa jiji, Kamanda Maro alikataa kujibu na kuwaamuru
kuondoka.
“Ondokeni tufanye kazi yetu, haiwahusu,” alisema.
Alipotafutwa Mkurugenzi wa Jiji, Wilson Kabwe, alisema kuhusu
operesheni hiyo, mkoa umekubaliana iendelee na hilo la kufungwa pingu
inategemea mhusika alivyokuwa akitii sheria.
Pia, alishangaa kusikia kukamatwa kwa mtu aliyekuwa akihoji ukiukwaji
wa taratibu za ukamataji, na kusema hata hivyo atawasiliana na Kamanda
wa Kanda Maalum, Kamishna Seleman Kova, ili kupata ufafanuzi kuhusu
tukio hilo.