VYUONI: NACTE YATANGAZA STASHAHADA YA UALIMU WA SHULE YA MSINGI (ODPE), VYUO VYA AWALI NI PAMOJA NA UDOM

https://jaridahuru.blogspot.com/2014/07/vyuoni-nacte-yatangaza-stashahada-ya.html
Dar es Salaam. Mafunzo ya stashahada ya ualimu wa shule za msingi (Ordinary Diploma in Primary
Education (ODPE) katika vyuo teule vya majaribio
na stashahada maalumu ya Ualimu wa Sekondari kwa waliomaliza Kidato cha
Nne (Hisabati na Sayansi), yataanza kutolewa katika Chuo Kikuu cha
Dodoma na yataanza rasmi Oktoba 6, mwaka huu.
Taarifa ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi
(Nacte) iliyotolewa jana mjini hapa, ilisema uombaji wa nafasi za
mafunzo hayo kwa mwaka 2014/15 ulianza Juni 23, mwaka huu, utamalizika
Agosti 31, mwaka huu.
Taarifa hiyo ilisema mafunzo yatatolewa katika
vyuo vilivyoteuliwa na Nacte, na baadhi ya vyuo vitatoa mafunzo hayo
chini ya uangalizi wa karibu wa baraza hilo, Taasisi ya Elimu na Wizara
ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dk Primus Nkwera
alisema waombaji wote wanatakiwa kuzingatia utaratibu wa uombaji ambao
ni kupitia njia ya mtandao ya mfumo wa udahili wa pamoja (Central
Admission System - (CAS) inayopatikana kwenye tovuti ya CAS au baraza na
hawatamtambua mwombaji yeyote atakayeomba kinyume na utaratibu
uliowekwa.
Dk Nkwera alisema lengo la mafunzo hayo ni kutoa
nafasi kwa walimu wa shule za msingi kuongeza uwezo na kujiendeleza kwa
masomo ya ngazi ya juu.
Alisema katika taarifa yake kuwa kwa muda mrefu
walimu wa shule za msingi hawana namna ya kuongeza na kuboresha taaluma
yao kutokana na kutokuwepo kwa kozi ya namna hiyo.