MHEMUKO wa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakiwemo viongozi
wa serikali kukimbilia kutangaza nia ya kumrithi Rais Jakaya Kikwete
mwakani, umezigawa taasisi mbalimbali za serikali, binafsi na umma hivyo
kuzorotesha utendaji wa kila siku.
Hivi karibuni, baadhi ya wanachama wa CCM wamekuwa wakitamka
hadharani nia zao za kuwania urais mwakani, huku wakijinasibu kwa hoja
mbalimbali.
Baadhi ya wana CCM waliotangaza nia ya kuwania urais mwakani ni
pamoja na Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye, Naibu Waziri wa Sayansi
na Teknolojia, January Makamba huku Edward Lowassa, Bernad Membe,
William Ngeleja, Steven Wassira wakitajwa matendo yao kuonyesha nia
hiyo.
Wakati ikiwa hivyo huku chama tawala kikishindwa kudhibiti, hali hiyo
imeanza kuzorotesha utendaji serikalini kwa kile kinachoelezwa
watendaji kugawanyika kulingana na wagombea hao.
Uchunguzi wa Tanzania Daima unaonyesha kuwa baadhi ya watendaji
serikalini wanashindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo au
wanalazimika kutekeleza baadhi ya mambo kwa hofu ya kuonekana wako
upande wa mtangaza nia fulani.
“Ndugu yangu, hivi sasa kwa kweli tuko mtegoni, maana ukifanya hiki
hata kama kina nia nzuri unajihisi kama kitampendeza nani kati ya
wanaoonyesha kugombea urais mwakani, na mbaya zaidi, baadhi yao wamekuwa
wakitutamkia wazi kuwa tunachokifanya tuko upande wa fulani wakati
kumbe sie hatuko huko… hii inatutia hofu na tunatekeleza majukumu yetu
kwa hofu badala ya kuzingatia taaluma, taratibu, kanuni na sheria,”
alisema mtendaji mmoja katika Wilaya ya Korogwe ambaye aliomba jina
lihifadhiwe kwa maslahi ya kibarua chake.
Chanzo kingine kiliipasha Tanzania Daima kuwa hali hiyo ya hofu si tu
kwa watendaji wa serikali, bali pia hata kwa taasisi nyingine, ikiwamo
vyama na mashirikisho ya michezo ambayo pia yanaathiriwa na harakati za
urais mwakani.
Kilisema kuwa pia mpango wa diplomasia ya michezo ulioibuliwa na
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa mara ya kwanza
mwaka huu tangu nchi kupata uhuru, una mlengo wa kisiasa zaidi hususan
kuelekea uchaguzi mkuu wa mwakani.
“Suala la programu za maandalizi na hata ushiriki wa timu za taifa
nje ya nchi kimsingi ziko kwenye wizara yenye dhamana na michezo, sasa
kitendo hiki cha Wizara ya Mambo ya Nje kinaonekana kuishusha wizara
husika ya michezo, kwani mipango hiyo ilitakiwa kufanywa na wizara yenye
dhamana na michezo, hivyo badala ya kuonekana ni jambo la kujenga
limeibua chuki miongoni mwa watendaji wa wizara hizo,” kilisema chanzo
chetu.
Inaelezwa tayari vyama na mashirikisho mbalimbali ya michezo
yameingia katika mkumbo huo na kujikuta yakitumika na baadhi ya
waonyesha nia ya kugombea urais mwakani, jambo linalowagawa viongozi na
hivyo kuzorotesha ufanisi.
Chanzo hicho, kilitaja baadhi ya mashirikisho ya michezo ambayo
yameingia kwenye mtego wa wagombea urais mwakani ni pamoja na Shirikisho
la Soka Tanzania (TFF), Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), klabu
kongwe ya Simba, klabu ya wasanii wa maigizo (Bongo Movie), kampuni na
taasisi mbalimbali zinazojishughulisha na masuala mbalimbali ya kijamii.
Inaelezwa kuwa kitendo cha Rais wa TFF, Jamal Malinzi na Rais wa
Simba, Evans Aveva kumtembelea Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa,
kimekuwa nongwa, kwamba kinawaathiri wao binafsi na taasisi wanazoongoza
kwa madai kuwa wanamuunga mkono kuelekea uchaguzi mkuu mwakani.
Watu kutoka ndani ya mashirikisho na klabu ya Simba, wanaeleza kuwa
kuna baadhi ya mipango ilikuwa ifanikishwe kupitia mashirika mbalimbali
ya umma na binafsi imesitishwa, kisa kikiwa hatua ya viongozi hao
kuonekana na mmoja wa wanaotajwa kuwania urais mwakani.
“Kwa kweli kuelekea uchaguzi wa mwakani ni lawama, maana tunashindwa
kutekeleza majukumu yetu itakiwavyo, ukifanya hivi unaambiwa uko kambi
ya fulani, ukitaka kumwalika mgeni rasmi katika matukio yetu, suala la
urais mwakani linawekwa kipaumbele, kwa kweli siasa inatutia hofu,
inatuchanganya na inatugawa,” alisema mmoja wa viongozi wa michezo.
Inaelezwa kitendo cha Rais wa RT, Anthony Mtaka, ambaye pia ni Mkuu
wa Wilaya (DC) ya Mvomero mkoani Morogoro kuishambulia waziwazi Wizara
ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwamba ni dhaifu siku ya kuagwa
kwa wanamichezo wa Tanzania kwenda kwenye kambi ya mazoezi nje ya nchi
kujiandaa na michezo ya Jumuiya ya Madola, Glasgow, Scotland kilikuwa na
mlengo wa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwakani.
Timu za ngumi, riadha, judo, kunyanyua vitu vizito na mpira wa meza
ziliagwa Aprili 29, mwaka huu kwenye ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa
Mwalimu Nyerere, ambako mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Membe.
Akitoa neno la shukrani, Rais wa RT, Mtaka, mbali na kummwagia sifa
Waziri Membe, wasaidizi wake na wizara yake kwa ujumla kwa kufanikisha
kambi hizo za nje ya nchi kupitia mpango huo wa diplomasia ya michezo,
katika hali ya kushangaza na kushtua aliiponda waziwazi wizara yenye
dhamana na michezo na kudai imegeuka wizara ya kulipana mishahara tu,
hivyo ibadilike na iige wizara ya Waziri Membe.
Kauli hiyo ilionekana kuwashtua na kuwaweka kwenye butwaa Waziri
Membe, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Leonard Thadeo ambaye
alimwakilisha waziri mwenye dhamana na michezo, Naibu Mkurugenzi wa
Michezo, Juliana Yasoda ambaye pia alikuwa ni mshehereshaji siku hiyo na
baadhi ya wanamichezo na wadau waliohudhuria hafla hiyo.
Katika kuweka sawa, kwa unyonge Yasoda alieleza kuwa wote ni serikali
kwa maana ya wizara hizo, na kwamba ziara hiyo ya mafunzo nje ya nchi
imefanikishwa na wizara hizo.
Kauli hiyo ya Mtaka, inaelezwa ililenga kumbeba Membe na
kuidhalilisha Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, jambo
ambalo hadi sasa limejenga chuki hususan katika suala hilo la michezo
ya Madola.
“Haiwezekani, kuna kitu, Mtaka licha ya kuwa kiongozi wa michezo, ni
kiongozi wa serikali, kimsingi haikuwa busara kukiponda na
kukidhalilisha mbele ya jamii chombo kingine cha serikali, kule ni
kuvuana nguo na kuna ajenda,” alisema ofisa mmoja wa wizara yenye
dhamana na michezo.
Harakati za wanachama wa CCM kuutaka urais mapema kabla hata taratibu
ndani ya chama kuwekwa hadharani, zimekuwa zikipigiwa kelele na baadhi
ya watu, lakini imeonekana kushindwa kupatiwa dawa, licha ya hatua
kadhaa kudaiwa kuchukuliwa ikiwamo baadhi yao kuwekwa chini ya
uangalizi.