MBUNGE wa Muhambwe mkoani hapa, Felix Mkosamali (NCCR Mageuzi),
amemlipua Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Philip Mangula
akidai kuwa ameondoka katika hoteli aliyofikia bila kulipa pango.
Akihutubia mamia ya wananchi wa Kibondo mkoani hapa jana kwenye
mkutano wa hadhara, Mkosamali alisema Mangula alifanya hivyo alipokuwa
katika ziara ya mikutano ya ndani ya chama hicho katika Jimbo la
Muhambwe.
Mkosamali aliyasema hayo katika mfululizo wa mikutano ya NCCR-Mageuzi
mkoani Kigoma, ikiongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Mosena
Nyambambe, Naibu Katibu Mkuu, Moses Machali ambaye pia ni Mbunge wa
Kasulu Mjini na Katibu Mwenezi, David Kafulila ambaye pia ni Mbunge wa
Kigoma Kusini.
Mbunge huyo alisema awali, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa alitaka kufikia hotelini hapo,
lakini Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, Venance Mwamoto aliuambia uongozi wa
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) linalomiliki hoteli hiyo kuwa Dk. Slaa
haruhusiwi kufikia hapo.
“Nimeshindwa kuelewa, ilikuwaje Dk. Slaa akazuiliwa kufikia katika
hoteli hiyo, lakini Mangula amefikia katika hoteli hiyo, tena akaishi na
kuondoka bila kulipia? Tunajifunza nini? Kwanini CCM wanaendelea
kutumia madaraka yao vibaya?” alihoji Mkosamali.
Aidha, Mkosamali aliwaambiwa wananchi wa Kibondo kuwa anakerwa na
tabia ya DC Mwamoto, kwani amekuwa akiwaelekeza askari wa Jeshi la
Wananchi kuwapiga raia hata wanaokwenda hospitalini, kwa kile
kilichoitwa kufanya usafi wa mji wa Kibondo siku ya Alhamisi.
“Usafi tunapenda wote, lakini DC amekuwa akiwatumia JWTZ kuwapiga
wananchi wasiofika kufanya usafi hata kama wanakwenda hospitali, raia
wanapigwa wanalazwa.
“Sasa ni utekelezaji gani huu wa sheria hata kama usafi tunapenda?
Tena siku hizi ukikamatwa unakula muwa unalipishwa 5,000 kwa amri ya
mkuu wa wilaya, mbona mambo haya hatukukubaliana katika vikao? Kwanini
DC anaruhusu ufisadi wa aina hii?” alihoji Mkosamali.
Katika mkutano huo, Mkosamali na Machali, walitoa tuhuma nzito kwa wakuu wa Wilaya ya Kibondo na Kasulu.
Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Dani Makanga, anatuhumiwa
anafanya ubaguzi wa kikabila, hivyo anaruhusu wafugaji kuharibu mashamba
ya wakulima wa Kagerakanda.
Wakati hayo yakisemwa kuhusu Makanga, Mkosamali alimtuhumu Mwamoto
kuwa anataka kuhamisha isivyo halali Kijiji cha Nduta, ambacho wananchi
walikabidhiwa baada ya kambi ya wakimbizi kufungwa katika eneo hilo.
“Mwamoto anataka kuwahamisha wakazi wa Nduta, lakini yeye mwenyewe
tayari amejiorodhesha na watu wengine kujipatia eneo la ekari 73 katika
kijiji hicho, sasa kwanini anafukuza wananchi hao na yeye anataka
kujimilikisha eneo hilo bila kufuata utaratibu?
“Huu sio utawala bora, DC kujichukulia eneo kubwa katika makazi ya
wanakijiji, tena sasa yeye na wana CCM wenzake wameanzisha ufugaji wa
nyuki katika maeneo karibu na Shule ya Msingi Ndutu, jambo linaloleta
usumbufu kwa wanafunzi wa shule hiyo,” alisema.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kigoma Kusini, Kafulila,
ameendelea kuwaambia wananchi juu ya ushahidi wake kuhusu suala la
tuhuma za wizi katika akaunti ya Tegeta Escrow, huku akieleza sababu
zake ni kwanini anataka Bunge lichunguze badala ya mdhibiti na mkaguzi
wa hesabu za serikali na ofisi hiyo.