ELIMU: WANAFUNZI KATIKA SHULE MBALIMBALI WAHIMIZWA KUSOMA MASOMO YA SAYANSI
https://jaridahuru.blogspot.com/2014/07/elimu-wanafunzi-katika-shule-mbalimbali.html
WANAFUNZI wa shule mbalimbali nchini wametakiwa kujifunza masomo ya
sayansi kutokana na umuhimu wake katika ugunduzi wa vitu ili kusaidia
taifa kimaendeleo.
Imeelezwa kuwa idadi kubwa ya wanafunzi na walimu hukimbia masomo
hayo na kusababisha watu kuamini ni magumu hasa kwa jinsi
yanavyofundishwa.
Akitoa rai hiyo jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Shirikisho
la Wanasayansi Chipukizi (YS), Dk. Gozibert Kamugisha, alieleza kuwa
taifa linakabiliwa na changamoto ya wataalamu wa masomo hayo, hivyo
kusababisha kutofikia hatua ya kugundua vitu kama ilivyo kwa nchi
nyingine.
Kamugisha alisema kuwa idadi kubwa ya wanafunzi na walimu wanashindwa
kujua jinsi ya kujifunza masomo hayo hatimaye kuchangia ongezeko kubwa
la upungufu wa wasomi kwenye sekta ya sayansi.
“Wanafunzi wengi wanajifunza sayansi kwa njia ya kukariri na sio
vitendo, hivyo kuna tija tubadilike ili nchi yetu iendane na mifumo
mipya inayoendana na mabadiliko ya dunia, hasa kwa vitendo,” alisema
Kamugisha.
Alisema kuwa miongoni mwa masomo ambayo yanakimbiwa ni Hesabu,
Fizikia, Biolojia, Kemia na Sayansi ya Jamii, hivyo kupunguza idadi ya
ugunduzi wa vitu mbalimbali vinavyofanywa na watu wengine duniani.
Hata hivyo, Kamugisha alifafanua kwamba, katika kutumia njia za
kuwavutia wanafunzi na walimu kupenda masomo hayo, shirikisho lao
limekuwa likiandaa mashindano kila baada ya mwaka, lengo likiwa
kushindanisha shule mbalimbali ili kujifunza masomo hayo kwa njia ya
vitendo.
