SIASA: WAZIRI MKUU, MIZENGO PINDA ASEMA HAYAPENDI MASWALI YA PAPO KWA HAPO

Alisema hayo bungeni jana alipokuwa akijibu swali la Rajab Mbarouk Mohammed (Ole-CUF), aliyehoji kuhusu Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazoendesha shughuli za serikali kwa uwazi (OGP), mpango uliozinduliwa mwaka 2011, jijini New York, Marekani. Alitaka kujua wakati mpango huo ukiingia awamu ya pili, ni nini tathmini ya serikali juu ya mpango huo.
"Ndiyo maana kipindi hiki sikipendi sana, swali ni zuri lakini kunitegemea kuwa nitaweza kuwa na kila jibu kwa kila swali ni ngumu. Angeniuma sikio jambo hili ningelifanyia kazi vizuri na kutoa majibu mazuri," alisema Waziri Mkuu Pinda.
Alisema mpango huo ni miongoni mwa ambayo nchi huitumia ili kufanya shughuli za serikali kuendeshwa kwa uwazi, pia Tanzania ni sehemu ya uamuzi wa msingi wa mpango wa APRM, ambao ni namna nyingine ya kulifanya taifa kuangaliwa na mtu yeyote ili kuona namna serikali inavyoendeshwa ili Watanzania waridhike na uendeshaji wa serikali.
Chini ya mpango huo, alisema serikali imeshirikiana na nchi nyingine, wadau wa maendeleo katika awamu ya kwanza na kuweka misingi ya namna ya kushirikiana.
Alisema kinachofanyika ni kuweka mpango kuhusu mambo gani yafanyike kwa uwazi.
Alisema ni kutokana na hilo, bajeti inawekwa kwenye mitandao, pia wizara zote zina utaratibu wa kutoa taarifa kwenye mitandao.
"Ndiyo maana hata Bunge katika mambo mengine hatuna ugomvi nalo, kuna mambo tunatakiwa kuweka wazi na tunafanya hivyo," alisema.
Waziri mkuu alisema ataomba itolewe kauli ya serikali kuhusu jambo hilo na hata APRM ili kuona serikali inavyoweka mambo wazi.
CHANZO: NIPASHE