https://jaridahuru.blogspot.com/2014/06/makala-kwa-kweli-viroba-ni-janga-kwa.html
SIKU hizi limekuwa jambo la kawaida kukuta vijana mitaa mbalimbali wakiwa wameshikilia vifuko vidogo vyemba na hata vinene vya plastiki wakifyonza maji yaliyomo ndani mwake.
Maji haya si ya kunywa kwani ukimpitia karibu unasikia harufu ya ulevi na hapo unagundua kwamba kile kipati kilichofyonzwa haraka kilikuwa kumbe ni pombe. Pombe hizo katika mifuko ya plastiki maarufu hujulikana kama viroba.
Aidha, kumekuwa na taarifa ya kuwa ajali nyingi za usafiri wa pikipiki maarufu kama ‘Bodaboda’ zinasababishwa kwa kunywa pombe hizo.
Yote hayo yanatokana na udhibiti hafifu wa pombe hizo ambazo zipo kila pembe za mitaa tena kwa bei nafuu ambazo kila kijana, ‘akibomu’ fedha kidogo anaweza kuzimudu.
Kutokana na kuwepo kwa pombe hizo ambazo nyingine ni za nchini na nyingine hutoka nje ya nchi, huku yapo madai kwamba zingine zinasindikwa kienyeji, wakati umefika wa taifa hili kujiuliza kama limeamua kuwaachia vijana wake kuishia katika ulevi wa kupindukia jambo ambalo ni janga la taifa.
Katika kuona hilo, ikiwa ni pamoja na uchafuzi wa mazingira, Naibu wa Viwanda na Biashara Janeth Mbene anashauri pombe hizi zipigwe marufuku kwani zimekuwa zikiuzwa kiholela hadi katika mageti ya shule, barabarani, maduka ya bidhaa za vyakula na kwa akinamama lishe jambo ambalo ni hatari kwa jamii na kutaka manispaa kuangalia suala hilo.
Hivyo, ni dhahiri kuwa wakati muafaka umefika wa kufanyia kazi ushauri wa kupiga marufuku pombe hizo zinazosababisha vijana wengi kuanza kutumia vilevi mapema.
Mbene alisema kuna pombe nyingine toka nje ya nchi zinazodaiwa kusababisha athari kwa watumiaji kupata majipu katika fizi pamoja na uchafuzi wa mazingira kwa mifuko hiyo kutapakaa sehemu mbalimbali.
Hivyo anashauri kuondolewa katika soko na kuwekwa katika mfumo wa chupa ambao utaweza kudhibitiwa kuliko ilivyo sasa.
Napenda kuunga mkono ushauri wa Naibu Waziri huyo kwani hivi karibuni huko mkoani Mbeya zilikamatwa pombe za aina kama hiyo zilizoingizwa nchini kinyemela ambazo ni hatari kwa afya ya binadamu.
Kutokana na athari zilizoanza kujitokeza kwa kuwa na walevi kila kona ni vema ushauri wa Naibu Waziri huyu ukachukuliwa kwa uzito stahili ili kuweza kudhibiti pombe hizo ambazo ni kali na dhahiri kuwa zitakuwa na madhara kwa afya.
Napenda kushauri mamlaka zinazohusika kuchukua hatua stahili mapema iwezekanavyo ili kuhakikisha pombe hizi zinaondolewa madukani na kutafutiwa namna nyingine ya kufanya biashara kuliko ilivyo sasa.
Pia napenda kumshauri,Waziri Mbene kuwa Wizara yake inahusika na ndio inayoweza kushirikiana na wizara nyingine kuhakikisha kwamba Watanzania wanaondoka na utumwa wa pombe zinazopatikana kwa bei karibu na bure.
Tunaamini kuwa kitendo cha kuacha hali hii ikiendelea inaweza kuwa janga la kitaifa kwani si jambo la ajabu hapo baadaye kukuta wanafunzi wakinywa pombe hizo na kuingia darasani kwani wataona ni jambo la kawaida.