https://jaridahuru.blogspot.com/2014/06/kitaifa-serikali-yamaliza-ugomvi-wa.html
Siku
chache baada ya Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Steven Maselle kutaka
Balozi wa Uingereza nchini Dianne Melrose, ajipime kwa kile
kinachodaiwa kuingilia mambo ya ndani ya nchi, Serikali imemsafisha
balozi huyo ikisema imeshalimaliza suala hilo.
Akizungumza
bungeni mjini Dodoma, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema kuwa
alimwagiza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard
Membe ambaye alikutana na balozi huyo na kuzungumza naye kabla ya
kuwakutanisha na Maselle na wakaafikiana kwa njia ya kidiplomasia.
"Mheshimiwa
Naibu Spika, napenda kutoa ufafanuzi kidogo kuhusu jambo hili ambalo
sote tunalifahamu kuwa liliibuka hapa bungeni, ni kweli nilimwagiza
Waziri Membe na akafanya kazi ya kuwakutanisha na kuwasuluhisha wawili
hawa na kwa kweli walishalimaliza kwa hiyo naomba tusiliendeleze tena,"
alisema Pinda.
Alitoa
kauli hiyo kutokana na mwongozo ulioombwa na mbunge wa Viti Maalumu,
Suzana Lyimo aliyetaka kauli ya Serikali kuhusu tuhuma dhidi ya balozi
huyo nchini Tanzania.
Akizungumza
katika sherehe za siku ya kuzaliwa ya Malkia Elizabeth wa Uingereza
zilizofanyika nyumbani kwa balozi huyo Dar es Salaam hivi karibuni,
Waziri Membe alisema hakuna mgogoro wowote wa kidiplomasia utakaowekwa
na Tanzania dhidi ya balozi huyo kutokana na uhusiano wa kina uliopo
baina ya nchi hizo mbili.
"Tumeshatuma
watu nchini Uingereza kupeleka masikitiko yetu na kuomba radhi kutokana
na kauli iliyotolewa bungeni. Hii ni kutokana na uhusiano mzuri
tulionao Uingereza na Tanzania na hatutaki kuuharibu uhusiano huo,"
alisema Membe.
Membe
alisema kwa kuwa Serikali haipo tayari kuharibu uhusiano kati ya nchi
hizo mbili, Waziri Mkuu Mizengo Pinda atalizungumzia suala hilo hivi
karibuni bungeni, ili kumhakikishia balozi huyo kuwa hana tuhuma za
kujibu.
Mei 30
mwaka huu, Waziri Maselle alimlipua balozi huyo wakati akichangia hoja
iliyotolewa na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila(NCCR-Mageuzi)
bungeni iliyoihusisha Uingereza na urejeshwaji wa Sh76 bilioni za chenji
ya Rada.
Akichangia
hoja hiyo, Maselle alimshutumu Balozi wa Uingereza kuhusika na kuratibu
vikao jijini Dar es Salaam na Dodoma kinyume cha taratibu na hadhi ya
kidiplomasia.
Alidai
kuwa balozi huyo amekuwa akihusika katika kusambaza ujumbe mfupi
unaodaiwa kutaka kukwamisha Bajeti ya Nishati na Madini pamoja na
kuwashawishi marafiki wa kimaendeleo wasitishe misaada ya kibajeti kwa
Tanzania.
Katika
maelezo yake, Membe alisema tuhuma zilizotolewa hazina ukweli wowote na
ni lazima zitolewe ufafanuzi ndani ya Bunge ili kudumisha urafiki wa
nchi hizo mbili.
"Kama
kauli hiyo ilivyotolewa bungeni kumshutumu balozi, hali kadhalika
tutahakikisha tunaomba msamaha kwa kile kilichotamkwa dhidi ya balozi.
Uchunguzi umefanyika na tumegundua kuwa hakuna tuhuma zozote zenye
ukweli dhidi yake," alisema.