KITAIFA: MCHUNGAJI MSIGWA AIKALIA KOONI WIZARA YA MALIASILI, ATAKA GMS KUJIBU HOJA DHIDI YA TUHUMUMA 11 ALIZOTOA

https://jaridahuru.blogspot.com/2014/07/kitaifa-mchungaji-msigwa-aikalia-kooni.html
WAZIRI Kivuli wa Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa, amewataka wamiliki wa Kampuni ya uwindaji ya kitalii ya Green Mile Safari Ltd (GMS), wajibu hoja za msingi dhidi ya tuhuma 11 alizozitoa dhidi yao.
Msigwa ambaye pia ni Mbunge wa Iringa Mjini (CHADEMA), aliyasema hayo wakati akihojiwa na kituo kimoja cha redio jijini Dar es Salaam jana.
Alisema kuwa anaishangaa kampuni hiyo kuhama kwenye hoja za msingi na kuingiza nyingine ambazo hazihusiani na madai yake.
Mchungaji Msigwa, Julai 4 mwaka huu akiwa jijini Dar es Salaam, alikutana na waandishi wa habari na kuwaonyesha ushahidi wa video namna Kampuni ya GMS ilivyokiuka sheria za uwindaji, ikiwamo kuua na kutesa wanyama kinyume na sheria ya wanyamapori ya 2009 na kanuni za wanyamapori.
Kwa mujibu wa Msigwa, GMS ilifanya uwindaji wa kukiuka sheria katika kitalu cha Gonabis/Kidunda – WMA na kitalu cha MKI – Selous, kipindi cha uwindaji cha mwaka 2012.
Kutokana na tuhuma hizo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, akitumia wataalamu wa wizara yake, alifanya uchunguzi na kubaini kampuni hiyo kuvunja sheria na kuifutia leseni.
Hatua hiyo ilipingwa na GSM ikidai Waziri Nyalandu anatumika na kampuni moja ya Kimarekani, na kwamba wametengeza utatu mtakatifu kati ya Nyalandu, Msigwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maliasili na Mazingira, James Lembeli ili kuhujumu kampuni za Kiarabu.
Kampuni hiyo iliomba Ikulu iingilie kati na ikishindikana itakwenda mahakamani.
Akizungumzia madai ya kampuni hiyo, Msigwa alisema inatakiwa ijibu tuhuma 11 alizoziainisha na si kukimbilia kuibua hoja za kidini na mgogoro wa kimaslahi kati yake na Kampuni ya Wengert Windrose Safaris Ltd (WWS), iliyokuwa ikimiliki kitalu cha Lake Natron Game Controlled Area (East) kwa miaka 15.
Msigwa alisema hoja hizo hazina mantiki, bali wanatakiwa wasimame kwenye hoja ya msingi ya kukiuka sheria ya uwindaji.
Aliongeza kuwa kama walikuwa na hoja ya kimaslahi, walitakiwa kuwasilisha mezani, na kama kweli, angeweza kuwatetea pia, lakini kwa kuwa wamevunja sheria hawezi kukaa kimya, kwani anatetea maslahi ya taifa.
Kuhusu hoja ya kuunda ‘utatu’, Mchungaji Msigwa alisema kama utatu wenyewe ni katika hilo la kupinga vitendo vya kuhujumu maliasili za taifa, basi hauna budi kuungwa mkono na Watanzania kwani una manufaa.
Kwa suala la kwenda mahakamani, alisema ni haki yao, ila si kuibua hoja za kupindisha ukweli.