BUNGENI: MBATIA AWAPIGIA DEBE MAJENERALI, AIASA SERIKALI KUWAONGEZEA PENSHENI

https://jaridahuru.blogspot.com/2014/06/bungeni-mbatia-awapigia-debe-majenerali.html
MBUNGE wa Kuteuliwa na Rais, James Mbatia ameiomba serikali iwaongeze pensheni wastaafu nchini, ikiwemo majenerali wa jeshi, kama vile Jenerali Mirisho Sarakikya na Brigedia Jenerali Hashim Mbita. Alisema hayo wakati akichangia Hotuba ya Wizara ya Fedha, iliyowasilishwa bungeni mjini hapa jana.
Mbatia ambaye ni mbunge wa NCCR-Mageuzi, alisema viwango vya sasa vya pensheni vinavyotolewa na serikali ni vidogo mno na vimepitwa na wakati.
Alisema ni kitu kinachoumiza kukuta hata majenerali wa jeshi waliotumikia Taifa kwa uadilifu na uaminifu mkubwa, wanalipwa pensheni ndogo mno.
“Majenerali wa jeshi kama Jenerali Sarakikya analipwa pensheni ya shilingi 50,000, mwingine ni Mzee Hashim Mbita hali yake si nzuri, mwingine ni mzee Apiyo aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi” alisema Mbatia akitoa mifano. Alitoa mfano wa mtu mwingine kuwa ni Mzee Sylivester Barongo.
Alisema Barongo alikuwa Mkurugenzi wa muda mrefu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), lakini kwa sasa pensheni yake kwa miezi sita ni Sh 480,000 yaani Sh 2,000 kwa siku.
“Pensheni hii anayolipwa mzee Barongo kwa miezi sita ni sawa na per diem ya mbunge,” alisema na kuomba serikali kurekebisha viwango vya pensheni, ili wastaafu wote, ikiwemo majenerali wa jeshi, wapate pensheni inayolingana hali ya sasa.” Ndipo Naibu Spika, Job Ndugai alisema:
“Kama pensheni hiyo ndiyo anayolipwa Jenerali Sarakikya basi ni hatari, hivyo inabidi hali hiyo irekebishwe”. Mwingine aliyetaka viwango vya pensheni kwa wastaafu virekebishwe ni Mbunge wa Mbogwe, Augustino Masele (CCM).
Alisema wastaafu wengi nchini kwa sasa wanalipwa Sh 20,000 kwa mwezi na kwamba kiwango hicho ni kidogo mno. Wakati huo huo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara imeiomba serikali kuwapa bure wafanyabiashara Mashine za Kielektroniki za Kodi (EFDs) za Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA).
“Kamati inahoji kwa nini serikali serikali isitoe mashine hizi bure kwa wafanyabiashara, hususan wale wa kipato cha chini ya milioni 40 kwani EFDs ni kifaa cha TRA katika kukusanya kodi, ” alisema Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Luhaga Mpina.
Mpina alihoji, “baadhi ya makampuni ya huduma za simu yamekuwa hata yakitoa vifaa pamoja na mitaji kwa mawakala wao, iweje serikali ishindwe kufanya hivyo kwa wafanyabiashara?” Alisema wafanyabiashara wanahoji kuwa mashine hizo za EFDs, zina laini ya simu ndani ambayo inatoa ishara ya taarifa za biashara.
“Mita Tanesco zinakuwa mali ya Tanesco huku mita za maji nazo zinakuwa ni mali ya Mamlaka za maji, hivyo kwa nini mashine hizo za EFDs zisimilikiwe na TRA wenyewe?” Alihoji Mpina ambaye ni Mbunge wa Kisesa (CCM).
Alisema hata mita hizo za Tanesco zinapoharibika, zinatengenezwa na wao wenyewe, hivyo kwa vipi mashine za EFDs zikiharibika anatengeneza wakala ambaye siyo TRA mwenyewe.
Mpina alisema kamati yake inahoji kwanini mashine hizo za EFDs zinauzwa na wazabuni, badala ya TRA wenyewe.
Alisema kwa upande wa TANESCO mita za LUKU huuzwa na shirika lenyewe na siyo wazabuni na pia matengenezo ya mita za LUKU hufanywa na shirika.
Aidha, alisema kamati yake inataka matengenezo ya mashine hizo za EFDs, yapatikane kila wilaya na kwa umbali usiozidi kilometa 40 ili kuwarahisishia wafanyabiashara kuendesha biashara kwa ufanisi zaidi. Akizungumzia deni la taifa, Mpina aliitaka serikali kupunguza kwa kiasi kikubwa deni hilo.
Alisema deni la taifa hivi sasa limefikia asilimia 47 ya Pato la Taifa .
“Katika muda mfupi tumeshuhudia ongezeko kubwa la deni la Taifa kutoka Sh trilioni 21.2 mwezi Juni mwaka 2013 hadi Sh trilioni 29.477 mwezi Januari 2014,” alisema.