AFYA: MGONJWA ATOKA HOSPITALI NA UGONJWA MWINGINE, YAMBIDI AKIMBILIE KWA MGANGA WA KIENYEJI
https://jaridahuru.blogspot.com/2014/06/afya-mgonjwa-atoka-hospitali-na-ugonjwa.html
Geita. Mgonjwa aliyepooza nusu mwili ambaye alikuwa amelazwa Hospitali ya Rufani Bugando Mwanza, amejikuta katika hali ngumu baada ya kuruhusiwa kurudi nyumbani akiwa na kidonda kikubwa sehemu ya makalio kilichotokana na kulala kwa muda mrefu kitandani bila kugeuzwa.
Joseph Luhogola (38), ambaye amepooza mwili
kuanzia usawa wa kifua hadi miguuni, amelazimika kwenda kwa mganga wa
Kienyeji kutumia miti shamba kutibiwa ugonjwa unaomsumbua.
Luhogola, mkazi wa Kijiji cha Mganza, wilayani
Chato, mkoani Geita, licha ya kuruhusiwa kutoka hospitalini, ndugu na
jamaa waliokuwa wakimuuguza hawakutambua kama alikuwa na kidonda kikubwa
sehemu hiyo.
Ndugu zake akiwamo mkewe, Kefline Kafaransa (36)
hawakutambua kama alikuwa kwenye hali hiyo hadi walimpofika nyumbani kwa
mdogo wake, baada ya kumvua nguo ndipo walipobaini hali hiyo.
Hali hiyo ilisababisha mdogo wake, Mustafa
Luhogola (36) mkazi wa Nyankumbu mjini Geita kupoteza fahamu kwa dakika
35 kutokana na mshtuko baada ya kuona kidonda hicho.
Luhogola alifikishwa Bugando Aprili 22 mwaka huu,
baada ya kupata ajali iliyotokana na gari dogo la kubeba abiria
kupinduka Kijiji cha Lubambagwe, Chato.
Akizungumza kwa shida huku akiwa amelazwa chumba
maalumu cha mganga wa kienyeji, Luhogola alisema baada ya kutokea ajali
hiyo alipoteza fahamu na kujikuta akiwa Bugando.“Kwa sasa sijitambui
kuanzia sehemu ya kifuani hadi miguuni, kidonda kinachosemwa kwenye
makalio sikitambui ingawa nakumbuka maelekezo ya wauguzi kunitaka nilale
chali bila kugeuzwa,” alisema Luhogola.
Mkurugenzi wa Hospitali ya Bugando, Dk Charles
Mjinge alipoulizwa juu ya mgonjwa huyo alisema hajui iwapo kidonda hicho
kilisababishwa na ajali au la na kwamba, inawezekana kulala muda mrefu
kutokana na kupooza ndiyo chanzo.“Ili kuweza kueleza haya mgonjwa aje
tuone, tutafute jalada lake tuweze kufuatilia kilichotokea, siyo kawaida
mtu kumruhusu akiwa na kidonda kikubwa kama unavyokielezea,” alisema Dk
Majinge na kuongeza:“Labda walimweleza mgonjwa hawakuwaeleza ndugu,
ndiyo maana hawakujua kama ana hali hiyo, sasa mwambie aje na nyaraka za
taarifa zake, lakini kuna tatizo la watu kama hao wamekuwa wakiomba
ruhusa ili waende kwa waganga wa kienyeji hasa hao wenye kupooza mwili.”
Mganga wa kienyeji anena.
Mganga wa kienyeji ambaye anamtibu Luhogola, Paulo
Chasama alisema yeye ni mtalaam wa kutibu mifupa iliyovunjika na watu
waliopooza mwili tangu mwaka 1997 alipoanza kazi.
Kuhusu mgonjwa huyo, Chasama alisema uhakika wa
kupona ugonjwa wa kupooza upo na kwamba, ndani ya mwezi mmoja atakuwa
kwenye hali nzuri isipokuwa tatizo kubwa ni kidonda.
“Walichokosea huko hospitali ni kule kumlaza chali
kila siku bila kumgeuza, hali iliyosababisha kuwa na kidonda kama hiki,
lakini suala la kupooza halitachukua muda mrefu atapona,” alisema

