KITAIFA: MNIGERIA MWINGINE ANASWA NA MADAWA YA KULEVYA 'unga" UWANJA WA NDEGE DAR
https://jaridahuru.blogspot.com/2014/06/kitaifa-mnigeria-mwingine-anaswa-na.html
Dar es Salaam. Raia wa Nigeria, Anthony Ifeanyichukwa Okafor (52), amekamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akidaiwa kumeza kete 100 za dawa za kulevya aina ya cocaine ambazo thamani yake bado haijafahamika.
Tukio hilo limetokea takribani siku 22 baada ya
raia mwingine wa Nigeria, Olabisi Ibidun Cole (65) kuvunja rekodi ya
umri wa watu wanaokamatwa wakiwa na dawa za kulevya katika uwanja huo.
Cole alikamatwa Jumatatu ya Mei 19, mwaka huu saa
tisa alasiri akijiandaa kwenda Paris, Ufaransa kwa ndege ya Shirika la
Ndege la Ethiopia, akiwa amemeza kete 82 aina ya heroini zilizokuwa
zimefungwa kwenye karatasi zinazofanana na ganda la sigara, ambazo si
rahisi kuonekana katika mitambo.
Mkuu wa Kitengo cha Polisi cha Kupambana na Dawa
za Kulevya Tanzania, Godfrey Nzowa (pichani) alisema jana kuwa mtuhumiwa
huyo alidai kuwa amefika nchini kumfuata rafiki yake wa kike
aliyekutana naye Hong Kong, China na baadaye Douala, Cameroon.
Nzowa alisema mtuhumiwa huyo alisema rafiki yake huyo wa Tanzania ni mpenzi wake na wako pamoja katika kazi hiyo.
Kamanda wa Polisi wa Uwanja wa Ndege, Hamisi
Selemani alisema wauzaji wa dawa hizo siku hizi wamegundua mtindo mpya
wa kuwatumia watu wazima ili wasigundulike kutokana na mwonekano wao.
“Muda si mrefu ametoa kete mbili na kufikisha 100
na anavyoonekana bado ataendelea kutoa nyingine, tunaye hapa tunaendelea
kumhoji,” alisema Selemani na kuongeza kuwa alikamatwa Jumamosi
iliyopita saa saba usiku akitokea Douala kwa ndege ya Shirika la Ndege
la Ethiopia.
Alisema alikamatwa baada ya maofisa wa uwanja huo
kufuatilia mwenendo wa taarifa zake za safari na kuangalia nchi
alizokuwa akisafiri.
“Tunapomkagua mtu tunaangalia taarifa zake jinsi
alivyosafiri, tunaangalia nchi zenye matukio ya kuuza na kuchukua dawa
za kulevya,” alisema na kuongeza:
“Watu wanaofanya biashara hii ni wajanja sana na
hujiamini kama huyu Mnigeria, alituambia tufanye kazi yetu yeye yupo
fresh, hana kitu na tulipomfanyia uchunguzi wa kina tukabaini amemeza
dawa za kulevya.
“Huyu alitumia ujanja wa kwenda nchini Cameroon
kwa kuwa nchi ile haitengenezi dawa hizo hivyo alipitia huko aweze kuja
hapa nchini asigundulike,” alisema.

