MICHEZO: MANYIKA HARUDI SINGIDA UNITED NG'OO (BABA WA MANYIKA)


BABA mzazi na Meneja wa kipa wa Singida United, Peter Manyika, Manyika Peter amesema kuwa mwanawe hawezi kurudi katika timu hiyo licha ya viongozi wake kusema wanajipanga kumrudisha.
Hivi karibuni Manyika aliamua kuachana na timu hiyo kwa madai mabosi wake wameshindwa kukamilisha vipengele walivyowekeana kwenye mkataba, ikiwa ni pamoja na kutolipwa mshahara wake kwa muda mrefu.
Akizungumza na gazeti jana, Manyika alisema amepata taarifa kuwa Singida wanataka kuwaita mezani ili kuyamaliza, lakini akasisitiza kuwa wajiandae kupata masharti magumu zaidi ya yale ya awali ambayo wameyashindwa.
Alisema katika kipindi cha usajili kuna timu kadhaa zilikuwa zikimhitaji, lakini alipowafuata viongozi wa Singida wakamsisitizia kuwa watamalizana naye, lakini hawakufanya hivyo mpaka dirisha likafungwa na kukosa timu.
“Kwenye usajili niliwafuata kuwauliza kama wanamhitaji, wao wakasema watakamilisha kila kitu, kulikuwa na timu zinamhitaji lakini nikaona asisaini kwingine awasubiri wao cha ajabu hawakukamilisha walichoahidi,” alisema Manyika