jaridahuru

Mitandao

SIASA:KANALI WA JESHI AISHAURI CCM KUJIANDAA KUUNDA SERIKALI YA MSETO,

Mbarali. Wapo wastaafu wengi wa Serikali ambao wanafuatilia kwa karibu nyenendo za siasa nchini, mmoja wapo ni Kanali Mstaafu Edmund Mjengwa (68) ambaye amekitahadharisha chama cha CCM kwamba kijiandae kwa Serikali ya mseto.
“Na endapo Rais atatoka CCM na wabunge wengi ndani ya Bunge wakawa ni wa upinzani, basi lazima Rais huyo akubali kufanya kazi na upinzani.
“Itabidi akubali kuunda Serikali ya mseto, japo sitarajii kufika huko. CCM ni imara, lakini tuwe na fikra hizo pia kwa nia nzuri ya kuiweka nchi katika amani,” ni kauli ya Kanali Mjengwa ambaye pia ni mkuu wa wilaya mstaafu.
Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili nyumbani kwake Mbarali, Kanali Mjengwa alisema licha ya upinzani kuwepo na kujipambanua kwa wananchi, lakini bado siyo tishio kwa CCM na itaendelea kushika dola tu kwani inaaminika na Watanzania wengi.
“Upinzani kuingia Ikulu bado sana, ila kwenye nafasi ya ubunge na udiwani ndiko kutakuwa na changamoto kubwa. Kuna uwezekano mkubwa wa wabunge wengi wakatoka upinzani lakini siyo Rais.
“Lakini niseme tu kwamba pamoja na CCM kuendelea kuaminiwa na wananchi wengi, isibwete wala kupuuza upinzani. Hawa jamaa wanazidi kujitanua kweli kweli, hivyo wanaweza kuiyumbisha,” alisema Kanali Mjengwa.
Kanali Mjengwa alisema CCM bado inaaminiwa na Watanzania wengi, lakini tatizo linalomkera na mabalo kwa maoni yake linaharibu adabu na sifa ya CCM ni kitendo cha wana-CCM kuchafuana majukwaani.
Alisema CCM imetoka mbali na inatakiwa kuongoza kwa vitendo na siyo kupiga kelele za kuchafuana majukwaani kama ambavyo ilivyo hivi sasa.
Kwa mujibu wa Kanali Mjengwa anachukia  kuona mwana-CCM anatumia jukwaa kumchafua mwenzake kisa tu wote wametangaza nia ya kugombea nafasi fulani ya uongozi.
“Kama unona mwana CCM fulani amekwenda ndivyo sivyo kuna taratibu za vikao ndani ya chama, wakazungumzie na kumaliza tofauti hizo ndani ya Chama ili kulinda heshima ya Chama na si vinginevyo.
“Na kitendo hicho ndicho kinachowapa nguvu wapinzani kwa kusemea na kutunanga kwa Wananchi hatimaye CCM inaonekana kutokuwa na watu makini,” alisema.
Kanali Mjengwa alisema katika kuelekea uchaguzi mkuu hali ya kisiasa inazidi kupamba moto na kila chama kinazidi kujipambanua kivyake kwa wananchi kikitaka kuungwa mkono.
Alisema tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi kumekuwa na upinzani mkubwa, japo CCM kimekuwa kikiibuka na ushindi kwa nafasi ya urais na majimbo mengi ya ubunge.
Kanali Mjengwa alisema bado anaamini kwamba uchaguzi wa mwaka huu utakuwa salama na amani, kama Watanzania hususan wanasiasa wataamua uwe hivyo.
Kuhusu mgombea urais, alisema mgombea atakayeteuliwa na CCM ndiye atakayekuwa rais. “Na kuhusu karata yangu naitupa kwa nani… kundi la wana-CCM wanaoonekana kutangaza nia hiyo atatoka kwenye kundi hilo na mimi namfahamu ila siwezi kukutajia kwa sasa ila ujue hivyo,” alisema.
Akizungumzia umuhimu wa amani, kuwa wanasiasa wengi wanahubiri mfarakano bila kutambua kwamba na wao ni Watanzania, na amani ikivurugika na wao watasambaratika.
“Kiongozi wa siasa anapopanda jukwaani na kuhubiri eti nchi haitatawalika, damu itamwagika huwa najiuliza hivi huyo siyo Mtanzania? Na hajui kama hayo yakitokea na yeye damu yake na ya ndugu zake itamwagika?, alisema.
Hivi karibuni Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki alinukuliwa na gazeti hili akitabiri kuwa CCM ina “kazi kubwa”, katika uchaguzi mkuu ujao.
Balozi Kagasheki pia alikitahadharisha chama hicho dhidi ya kuzidi kukua kwa nguvu ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) akisema iwapo umoja huo utamchagua mgombea makini, CCM itakuwa na kazi ngumu.
Kauli yake iliungana na za vigogo wengine wa CCM waliotahadharisha mwenendo wa chama hicho dhidi ya ongezeko la nguvu ya upinzani, akiwamo Waziri Mkuu wa zamani, Fredrick Sumaye, ambaye alisema rushwa inakimaliza chama hicho, na Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, January Makamba, ambaye alisema kuwa chama hicho kisitegemee ushindi wa kishindo.

Related

Siasa 337143122723947907

Post a Comment

emo-but-icon

Wadhamini

UJUMBE

JH Katika Facebook

Nyayo zetu twitter

Za Juu

Mitandao

Piga Kura

Je ungependa Tanzania iwe na serikali ngapi?
  
pollcode.com free polls 

ADVERTISEMENTS

Msimamo wa ligi mbalimbali

Football results provided by whatsthescore.com

Mechi Live

Walioko Hewani Kwa Sasa

item