JAMII: ILE AJALI YA MOTO ILIYOUWA FAMILIA NZIMA DAR YAZUA KIZUNGUMKUTI MSIBANI, NDUGU WAGEUKA MBOGO
https://jaridahuru.blogspot.com/2015/02/jamii-ile-ajali-ya-moto-iliyouwa.html
Dar es Salaam. Waombolezaji kwenye msiba uliotokana na ajali ya moto ulioteketeza watu sita wa familia moja, wamelaumu Kikosi cha Zimamoto cha Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kushindwa kufika kwa wakati eneo la tukio.
Juzi familia ya watu sita ya Mzee David Mpira na mkewe Celina, iliteketea kwa moto ikijumuisha Lucas Mpira, Samwel Yegela, Pauline Emmanuel na Celina Emmanuel. Chanzo cha moto huo inadaiwa kuwa ni hitilafu ya umeme.
Katika tukio hilo, Emmanuel Mpira ndiye pekee aliyenusurika katika ajali hiyo kwa kuwa wakati moto unatokea yeye alikuwa ametoka kwenda matembezini.
Jana, waombolezaji hao ambao wengi ni wakazi wa Kipunguni A ilipoteketea nyumba hiyo, kwa nyakati tofauti walisema hakuna haja ya kuwepo kikosi hicho ambacho mara kwa mara kimekuwa kikifika kimechelewa kwenye maeneo ya matukio ya ajali na hata kama wakiwahi wanakuwa hawana maji. “Tumepiga simu tangu saa 10.00 usiku mara baada ya kuona moto unateketeza nyumba lakini wamefika hapa saa 12.00 asubuhi wakati moto umeshateketeza kila kitu,” alisema Abdallah Mlele mkazi wa eneo hilo.
Mlele alikuwa akiungwa mkono na wenzake ambao walisema kwa utendaji unaonyeshwa na chombo hicho ni bora kisiwepo.
“Hakuna haja ya kuwapigia simu ‘fire’ wakati wanakuja kuzima moto wakiwa wamechelewa na wakati mwingine hawana maji,” alisema.
Akizungumzia hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi Maalumu, Profesa Mark Mwandosya ambaye ni ndugu wa familia hiyo, alisema si vizuri kuzungumzia suala hilo katika kipindi hiki bali kinachotakiwa ni kusubiri uchunguzi.
“Huwezi ukawalaumu zimamoto kwa sasa, au Tanesco kutokana na hili, tusubiri uchunguzi ndipo tupate pa kuzungumzia,” alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Mary Nzuki alisema jana kuwa wanaendelea na uchunguzi ili kufahamu chanzo cha moto huo.
“Bado haijafahamika thamani ya vitu vilivyoungua na chanzo cha moto huo, tunaendelea kuchunguza ili kubaini chanzo hasa,” alisema Nzuki.
Naye Msemaji wa familia hiyo, Godfrey Mwandosya ambaye ni mdogo wake na Profesa Mwandosya alisema shughuli zote za mazishi zitaanza kesho saa 5.00 asubuhi kwa kuaga miili ya marehemu kabla ya kupelekwa kwenye Kanisa Katoliki la Ukonga kwa ajili ya ibada.
Alisema baada ya hapo, miili hiyo itapelekwa kwenye makaburi ya Airwing Ukonga kwa maziko yatakayofanyika kuanzia saa 10.00 jioni
Kuhusu ndugu yake, Emmanuel ambaye amenusurika, alisema: “Emmanuel tunamwacha apumzike…tumeona ni vizuri akakaa sehemu ambayo hataona yanayoendelea hapa nyumbani kwani hali hiyo inaweza kumuathiri kisaikolojia,” alisema.
Hata hivyo, Emmanuel ambaye alikuwa kwenye nyumba ya jirani hakuzungumza chochote wala kujibu salamu ya mwandishi wa habari.
Waliokaribu, walisema amekuwa akizungumza mara chache na marafiki zake na muda mwingi amekuwa akikaa kimya.
Majirani
Majirani walisema Celina Mpira mke wa Mzee David enzi za uhai wao waliishi kwa upendo na majirani zake na kwamba walikuwa wameanza kuwaaga majirani zake.
Neema Kalinga ambaye ni jirani alisema familia hiyo ilikuwa inataka kuhamia eneo la Kibeberu Kitunda kwa sababu wakazi wote wa Kipunguni A wanatakiwa kuhama eneo hilo ili kupisha upanuzi wa uwanja wa ndege.
“Walikuwa wanakamilisha ujenzi wa nyumba yao nyingine huko Kibeberu, alikuwa ameshaanza kutuaga, kumbe ilikuwa ni safari ya milele,” alisema.
Jirani mwingine Athumani Ismail alisema marehemu David enzi za uhai wake alikuwa mshabiki wa mpira, “tulikuwa tunataniana sana kuhusu vilabu vyetu vya ndani na nje ya nchi,”
Diwani wa Kata ya Kipawa, Bonna Kaluwa ambaye alikuwa miongoni mwa waombolezaji alisema, “huu ni msiba wa wana Kipunguni wote kwa sababu moto umeteketeza familia yote, tushirikiane katika kipindi hiki kigumu.”
Wanafunzi
Miongoni mwa waliokufa ni watoto Pauline Emmanuel anayesoma Shule ya Chekechea ya Tumaini na Celina Emmanuel anayesoma darasa la nne katika shule ya msingi ya Minazi Mirefu, Ukonga, Dar es Salaam.
Hao ni watoto wa Emmanuel Mpira aliyenusurika katika ajali hiyo na mama Mwajuma Issa. Watoto hao walikuwa wakiishi na babu yao.