SIASA: ZITTO AIBUA UOZO MWINGINE WA MAPATO YA TANZANITE, WAZIRI MGENI WA NISHATI AKIONA KITI KICHUNGU
https://jaridahuru.blogspot.com/2015/02/siasa-zitto-aibua-uozo-mwingine-wa.html
Dodoma. Bunge limeagiza kuwa swali lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Kidawa Hamid Saleh kuhusu kiasi cha mapato yaliyotokana na mauzo ya Tanzanite katika kipindi cha mwaka 2011 hadi 2014, lijibiwe tena na Serikali.
Agizo hilo lilitolewa jana na Mwenyekiti wa Bunge Mussa Zungu baada ya kutokea hali ya mabishano kwa wabunge kuhusu thamani ya madini ya Tanzanite katika soko la nje.
Katika swali hilo, Saleh alihoji ni kiasi gani cha fedha kimepotea kutokana na vito vya Tanzanite kwa kuuzwa kwa njia isiyo halali katika kipindi hicho.
Awali akijibu, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Mwijage alisema katika kipindi hicho Sh5.92 bilioni ziliingizwa katika pato la Taifa ikiwa ni mrahaba.
“Mwaka 2011 zilikuwa Sh1.24 bilioni, 2012 Sh1.53 bilioni, wakati mwaka 2013 zilifikia bilioni 1.67 na 2014 zikawa Sh1.48 bilioni,” alisema Mwijage.
Kuhusu kiasi kilichopotea alisema ni Dola 400 milioni za Kimarekani.
Hata hivyo, majibu hayo hayakuwaridhisha wabunge, akiwamo Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe ambaye aliomba mwongozo na kutaka swali hilo lijibiwe upya.
Mwenyekiti wa Bunge, Zungu alikubali ombi hilo.