jaridahuru

Mitandao

SIASA: MIAKA 38 YA CHAMA CHA MAPINDUZI, WENGI WAHOJI FALSAFAYA RASI BORA LAZIMA ATOKE CCM NI YA KWELI?


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mwishoni mwa wiki iliyopita kimeadhimisha miaka 38 tangu kuzaliwa kwake katika kaya hii. Mazuri na mabaya yake sitayajadili leo bali nitaangalia jambo moja nalo ni IMANI.

2015 ni mwaka wa uchaguzi. CCM kama chama tawala kinaingia kwenye kinyan’ganyiro hicho kikiamini falsafa ya ya kiongozi wake wa kwanza Mwalimu Julius Nyerere kuwa rais bora hawezi kutoka nje ya CCM.

Kwa masikio yangu mimi Mkuu wa  Kaya nilimsikia mwenyekiti wa chama hicho taifa, Jakaya Kikwete, akisherehesha imani hiyo alipokuwa anahutubia maelfu ya wafuasi wa CCM katika Uwanja wa Majimaji mjini Songea mkoani Ruvuma.

Najiuliza; imani ya chama hicho tawala inaambatana na matendo? Maana ni wazi Nyerere aliposema rais bora atatoka CCM alimaanisha CCM bora siyo dhaifu.
Msingi wa hiki ninachokisema unajengwa na kauli ya muasisi huyo pale aliposema: “Bila CCM imara nchi itayumba.” Hapa ndipo mahali pa kujadili.

Je, wakati mwenyekiti wa sasa akisisitiza imani ya chama chake mbele ya wanachama anaamini kuwa CCM anayoingoza ni bora kama zama za Mwalimu na kwamba ina sifa za kutoa rais bora? 
Namkumbusha; Kikwete aliposisitiza kuuenzi wosia wa Mwalimu anakumbuka kauli ya muasisi wake aliyosema; Watanzania wanataka mabadiliko na wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje?
Kwa mawazo ya leo, hakuna asiyejua kuwa kioo cha CCM kimemeguka vipandevipande na taswira zinazoonekana ndani zinatofautiana. Chama kimegawanyika katika makundi.

Leo hii mwenyekiti akisimama mbele ya kioo cha chama chake haonekani mwili mzima, amegawanyika kiasi cha kutoutambua utimilifu wake na  ndiyo maana anasisitiza ongezeko la wagombea urais wenye sifa kwa kuwa waliojitokeza hawajaweza kuziba ufa wa kioo chake.
Mwenyekiti angali anatishwa na kivuli cha makundi; Nyerere hakuwa mwoga, alikuwa jasiri, mwenye kusimamia anachokiamini. Waliofanya naye kazi wanashahidisha kuwa hakuongoza kwa matakwa ya chama bali ya wananchi.
Msingi huu ndiyo ambao CCM inapaswa kuufuata katika kuelekea kuipatia kaya hii mkuu mpya mwenye sifa ya ubora. Vinginevyo imani waliyorithishwa kuwa rais bora atatoka CCM itakuwa haina maana.
Mwananzengo wenzangu; wakati chama hicho kikiadhimisha miaka 38 ya uhai wake, falsafa tatu lazima tuzifikirie sana kwa mustakabali wa kaya hii, nazo ni RAIS BORA KUTOKA CCM, WATANZANIA WANATAKA MABADAILIKO NA BILA CCM IMARA NCHI ITAYUMBA.

Kuelekea kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu, lazima wananzengo tujihoji juu uimara wa chama tawala na kama kitaweza kumteua mgombea bora tunayemtaka. Maana tunaweza kuamini falsafa kuwa rais bora atatoka CCM lakini wakubwa wakajiteulia mgombea atakayelinda maslahi yao na sisi tukadanganywa kwa imani iliyokufa na kuzikwa kuwa rais bora lazima atoke CCM. Tusikubali!
Jambo la pili ni uhitaji wa mabadiliko. Mgombea ajaye lazima awe na kigezo cha kuiletea kaya hii mabadiliko ambayo Wanazengo wanayataka. Tukiletewa mgombea ambaye hana sifa hii tutoke usingizini tuyatafute mabadiliko yetu nje ya CCM!
Mwisho wake ni CCM dhaifu kuiyumbisha nchi. Kama nilivyosema, chama hiki kutokana na makundi ya urais yanayonyukana kuingia ikulu, yanaweza kukidhoofisha chama hicho.  Hilo likitokea tusikubali kuyumbisha nchi nzima, badala yake tukiache chama kiyumbe chenyewe na ikiwezekana kianguke madarakani kabisa!
Huu ndiyo msimamo wangu mimi Mkuu wa Kaya.  Shime Wananzengo wenzangu, niungeni mkono katika mawazo haya!

Related

Siasa 3869684359494509533

Post a Comment

emo-but-icon

Wadhamini

UJUMBE

JH Katika Facebook

Nyayo zetu twitter

Za Juu

Mitandao

Piga Kura

Je ungependa Tanzania iwe na serikali ngapi?
  
pollcode.com free polls 

ADVERTISEMENTS

Msimamo wa ligi mbalimbali

Football results provided by whatsthescore.com

Mechi Live

Walioko Hewani Kwa Sasa

item