MAONI: KUHUSU SERIKALI NA MPANGO WA KUHAMIA DODOMA, YAPINDISHWA NA KUTAKIWA KUWA MAKAO MAKUU YA VYUO VIKUU
https://jaridahuru.blogspot.com/2015/02/maoni-kuhusu-serikali-na-mpango-wa.html
Mjadala kuhusu Serikali kuhamia Dodoma juzi uliibua mapya bungeni kwa baadhi ya wabunge kusema hicho siyo tena kipaumbele cha Taifa, huku wengine wakisema azima ya Serikali kuhamia Dodoma lazima ibaki palepale. Tofauti na mijadala iliyofanyika bungeni huko nyuma, juzi kwa mara ya kwanza baadhi ya wabunge wa CCM walipinga wazi mpango huo na kusema hakuna tena sababu ya kuendelea kupoteza fedha za umma wakati Serikali haina dhamira ya kuhamia Dodoma. Mmoja wa wabunge hao alikwenda mbali zaidi na kusema kuwa, iwapo Serikali ingetaka kuhamia Dodoma ili kumuenzi mwasisi wa mpango huo, yaani Baba wa Taifa, basi ingemuenzi pia kwa kuendeleza Azimio la Arusha badala ya kulifuta.
Ikumbukwe kwamba mwaka 1973, yaani miaka 42 iliyopita Serikali iliamua kuhamisha Makao Makuu kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma. Wakati huo, Taifa letu lilishuhudia mitikisiko mikubwa, ambapo nchi za Angola, Zimbabwe, Msumbiji na Namibia zilikuwa katika harakati za kuwatoa wakoloni zikisaidiwa na Tanzania na Zambia. Pia, wakati huo Afrika ya Kusini ilikuwa bado ikiongozwa na utawala wa kibaguzi, hivyo Tanzania na Zambia zikaanzisha mapambano ya kuzikomboa nchi hizo.
Katika hali hiyo, Tanzania na Zambia zilichukuliwa na mabeberu kama maadui zao wakubwa. Zambia ilikuwa ikishambuliwa kijeshi na majeshi ya kibeberu mara kwa mara, huku mabeberu wa Kireno wakifanikiwa kumuua kwa bomu mjini Dar es Salaam kiongozi wa Frelimo, Dk Edwardo Mondlane. Hivyo, kwa kuzingatia ukweli kwamba Tanzania na Zambia zilikuwa vitovu vya majeshi ya ukombozi na hifadhi ya maelfu ya wakimbizi kutoka nchi hizo, usalama wa nchi hizo mbili bila shaka ulikuwa mdogo. Hivyo, uamuzi wa kuhamisha Makao Makuu ya Serikali kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma uliwapa Watanzania faraja kubwa.
Inashangaza kuona kwamba miaka 42 tangu uamuzi huo wa kihistoria uchukuliwe, hakuna lolote la maana lililofanyika. Serikali ilitakiwa kuhamia Dodoma ifikapo mwaka 1986. Lakini hilo halikufanyika na hadi hivi sasa ni taasisi na wizara chache sana ndizo ‘zimehamia’ Dodoma, kwani nyingi zimefanya hivyo kinadharia, siyo kwa vitendo. Watanzania wanaona tatizo ni viongozi kukosa utashi wa kisiasa na kugeuza mpango huo kuwa mradi wa kujipatia fedha kwa kujilipa posho, kugharimia ofisi, magari, makazi na watumishi katika miji hiyo ya Dodoma na Dar es Salaam kwa wakati mmoja.
Mamlaka ya CDA, ambayo mwaka 1976 ilipewa jukumu la kuendeleza Makao Makuu ili Serikali iweze kuhamia, imewekwa pembeni. Wizara saba ambazo ni Ikulu; Fedha; Mambo ya Nje; Katiba na Sheria; Nishati na Madini; Ulinzi; na Mambo ya Ndani zilipangiwa kuhamia Dodoma kati ya mwaka 1988 na 1993, lakini zaidi ya miaka 22 imepita bado zimejichimbia jijini Dar es Salaam.
Kwa kuwa Ikulu na wizara nyingi bado zipo Dar es Salaam na majengo mengi ya Serikali na balozi za nje zilizopo nchini yanaendelea kujengwa, hiyo ni ishara tosha kwamba mpango wa Serikali kuhamia Dodoma haupo tena, kwa maana ya kutokuwa tena kipaumbele cha Taifa. Umefika wakati viongozi wawaambie wananchi ukweli kwamba mpango wa Serikali kuhamia Dodoma umefutwa ili fedha za walipakodi zielekezwe kwenye miradi yenye tija kwa Taifa.