SIASA: MNYIKA SASA AMKALIA KOONI RAIS, ATAKA ATEKELEZE AAGIZO LA WANANCHI WA UBUNGO
![](https://resources.blogblog.com/img/icon18_edit_allbkg.gif)
https://jaridahuru.blogspot.com/2014/12/siasa-mnyika-sasa-amkalia-kooni-rais.html
Mbunge wa jimbo la Ubungo, Jon Mnyika,
amemtaka Rais Jakaya Kikwete kutekeleza ahadi ya kuwapatiwa wananchi
wake huduma ya maji aliyoitoa mwaka mmoja uliopita.
Ametoa wito huo jana alipokuwa
akifungua semina ya kuwajengea uwezo viongozi wa ngazi mbalimbali wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutoka kata zote 14 za jimbo
hilo.
“Namuomba Rais Kikwete
awaambie wananchi wa Ubungo ni lini kikao alichokiahidi Machi mwaka jana
kati yake, mimi, Dawasa na Dawasco kitafanyika ili kuwaondolea kero
wapigakura hawa. Afanye hili ili asionekane muongo mbele ya wananchi
hawa,” alisema.
Mnyika alieleza pia kuwa mradi
wa ujenzi wa mabomba makubwa ya maji uliokuwa unatekelezwa na kampuni
ya Kichina hauna tija kwani mabomba hayo hayatoi maji kama
ilivyokusudiwa na akaitumia nafasi hiyo kuhoji kama hilo nalo ni
miongoni mwa faida za ziara ya hivi karibuni ya rais nchini huko.
Alisema “ni matumizi mabaya ya
rasilimali za nchi kama mradi unaweza ukatekelezwa pasipokuleta matunda
yaliyokusudiwa. Rais awaeleze wananchi kama aliwauliza Wachina juu ya
kampuni iliyotekeleza mradi huo.”
Alifafanua kuwa ombi la
kukutana na Rais lilitolewa na wananchi wa kata ya Goba na limeungwa
mkono na wananchi wa jimbo zima kupitia viongozi wao waliohudhuria
semina hiyo inayowajengea uwezo na kuwaelimisha juu ya maadili na
misingi ya chama, nafasi ya chama katika kuchangia maendeleo pamoja na
kuwahamasisha kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Washiriki wa semina hiyo
walimhakikishia naibu katibu mkuu huyo wa Chadema bara kuwa tayari
wameandaa wagombea katika kila kata ambao watatoa upinzani wa kutosha
dhidi ya Chama Cha Matinduzi (CCM) na kuondoa mazoea ya kuwa na maeneo
yasiyokuwa na upinzani.