BUNGENI: KURA ZAILITABISHA BUNGE LA KATIBA, SITTA ACHANGANYA MADAWA
https://jaridahuru.blogspot.com/2014/09/bungeni-kura-zailitabisha-bunge-la.html
BUNGE Maalum la Katiba, limepitisha azimio la kuzifanyia marekebisho
kanuni za 30, 36 na 38 ili kuruhusu wajumbe watakaokuwa nje ya Bunge
(ndani au nje ya nchi), wapige kura za kuamua ibara na sura za rasimu ya
katiba popote watakapokuwa.
Kwa mabadiliko hayo, wajumbe wa dini ya kiislamu waliokwenda hija
mjini Macca nchini Saudi Arabia, wanaopata matibabu nchini India na
walio katika majukumu mengine ndani na nje ya nchi, watapiga kura kuamua
rasimu ya katiba mpya inayopendekezwa.
Hata hivyo, marekebisho hayo yalizua mvutano baina ya Mwenyekiti wa
Bunge hilo, Samuel Sitta na wajumbe watatu, Ezekiel Oluoch, Said Arfi na
Ali Omari Juma waliopinga, ambako aliwakemea mara kwa mara wakati
wakichangia, akiwaita waongo.
Kabla ya Sitta kumwita Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni, Ameir Pandu
Kificho awasilishe azimio hilo, alisema kuwa wakati huu wa kukaribia
kupiga kura wamelazimika kuzitazama kanuni ili kuona kama zinawawezesha
kupiga kura ndani ya muda.
“Tunatarajia wapiga kura sisi wajumbe si chini ya 480, kwa jinsi
kanuni zilivyokaa hivi sasa, kwamba kwa kura za wazi mjumbe anaitwa
jina, halafu anatamka ndiyo au hapana kwa ibara moja baada ya nyingine
na wale wa kura za siri wanakuja mbele kuandika maamuzi yao.
“Tukichukua kwamba kwa wastani kuchukua dakika mbili kwa kila mjumbe
basi hizo ni dakika 960 kwa ibara moja, tunatarajia ibara zitakuwa 300,
dakika 960 takribani saa 16, tukiendelea na utaratibu tutakuwa tunatumia
siku nzima kwa sura moja,” alisema Sitta na kumpa nafasi Kificho.
Akiwasilisha azimio hilo kwa niaba ya Kificho, mjumbe wa kamati hiyo,
Amon Mpanju, alisema kuwa kanuni ya 30 inafanyiwa marekebisho katika
vifungu vya (1), (2) na kuongeza fasili mpya ya 2A.
Sasa kifungu (1) kitasomeka kuwa; akidi kwa kila kikao cha Bunge Maalum itakuwa ni nusu ya wajumbe wote wa Bunge maalum.
Fasili mpya ya “(2A) kwa madhumuni ya fasili (1) na kwa ajili ya
kuzipigia kura ibara za sura za rasimu ya katiba zilizoandikwa upya na
rasimu ya mwisho ya katiba, wajumbe wa Bunge maalum walio nje ya maeneo
ya Bunge kwa ruhusa ya maandishi ya mwenyekiti, watajumuishwa kwenye
idadi ya wajumbe waliohudhuria kwenye kikao cha Bunge.
“Kuongeza fasili mpya ya (3A) Katibu atawapatia wajumbe wa Bunge
maalum waliomo ndani ya ukumbi wa Bunge orodha ya wajumbe wote waliopata
ruhusa ya kupiga kura wakiwa nje ya maeneo ya Bunge maalum.
“Baada ya kanuni ya 38 kuongeza kanuni mpya ya 38A.- (1) Mjumbe
yeyote aliye nje ya maneno ya Bunge maalum, anaweza kupiga kura mbele ya
ofisa aliyethibitishwa kwa maandishi na Katibu wa Bunge kuwa msimamizi
wa upigaji wa kura kwa masharti yafuatayo,” alisema na kuyataja;
(a) Awe ameruhusiwa kwa maandishi kuwepo nje ya ukumbi wa Bunge na
mwenyekiti na (b) awe ameomba kwa mwenyekiti na kuruhusiwa kwa maandishi
kupiga kura yake akiwa nje ya ukumbi wa Bunge maalum.
Baada
ya kuwasilisha marekebisho hayo, Oluoch ndiye alikuwa mzungumzaji wa
kwanza akisema haungi mkono wajumbe wasiokuwepo kuruhusiwa kupiga kura.
Mjumbe huyo ambaye alianza kwa kumtaka Sitta kutumia busara na kanuni
kuzingatia sheria zilizopo, akisema kuwa haoni sababu ya wajumbe
wasiokuwepo kulazimishwa kupiga kura kwa sababu ni kuvunja sheria.
“Kila raia wa nchi hii anayo haki ya kupiga kura akitimiza miaka 18
kikatiba, lakini haki hiyo imewekewa utaratibu kisheria, taratibu tulizo
nazo hazijaweka utaribu wa kwamba mtu ambaye hatakuwepo kwenye eneo la
kupigia kura ataruhusiwa kupiga kura…hatujawa na sheria hiyo,” alisema
na kukatizwa na Sitta;
Kura zipi wewe unasema…Oluoch akajibu, kura yoyote ile… Sitta
akauliza tena, wapi ebu nioneshe kifungu…Oluoch akaomba amalize aoneshe
kifungu lakini Sitta akasema; “Unasema uongo mtupu wewe, unasema sheria
ya uchaguzi, tunamchagua nani hapa?” alihoji Sitta huku Oluoch akisema
“ngoja niendelee japokuwa umeniita mwongo”.
Aliongeza kuwa anachokiona ni kutaka kutimiza mambo ambayo si msingi
wa sheria kwa kutaka wajumbe waliokwenda Macca kuhiji ili waweze kupiga
kura, suala alilosema linahitaji ufafanuzi wa kidini kutoka kwa Sheikh
Mkuu ili aeleze kama wajumbe waliokwenda kuhiji wanaweza kupiga kura.
Sitta aliendelea kuwabana wajumbe waliokuwa wakipinga azimio hilo
huku akionesha kuwapendelea wale waliounga mkono kiasi cha hata wakati
mwingine kuwapigia makofi walipokuwa wakichangia kwa kuingiza masuala
yaliyo nje ya azimio.
Mbunge wa Mpanda Mjini (CHADEMA), naye alikumbana na kizingiti cha
Sitta, pale alipokataa kuunga mkono azimio hilo akisema wenye haki ya
kupiga kura ni wale watakaokuwepo siku husika.
Wakati Arfi akifafanua kwamba si haki wala busara kwa wajumbe
wasiokuwepo kulazimishwa kupiga kura, akisema ni kinyume na matakwa ya
demokrasia, Sitta aliingilia kati na kuhoji…nani amekwambia
wanalazimishwa…nani analazimisha?
“Arfi alimjibu Sitta kwamba; “anavyotuingilia wakati tukichangia,
watanzania wanakuona…unashusha hesima yako,” alisema na kujibiwa na
Sitta kuwa anawajibu wa kuzungumza jambo la kweli, kwamba anaposema watu
wanalazimishwa onesha ushahidi.
Hata wakati Ali Omar Jumba akichangia na kukosoa azimio hilo na
kutaka shughuli ya upigaji kura isogezwe ikibidi ili waliokwenda hija
wawe wamerudi, Sitta alimparamia na kumkatiza akisema; “kuna dhana
inajitokeza kwamba walio nje wanalazimishwa kupiga kura. Hii sio sahihi
kwani yuko mjumbe anatibiwa India ameniomba kupigia kura akiwa huko.
“Wale wanaosimama hapa na kutaka kusema kwamba tunalazimisha wajumbe,
wasitupotezee muda hapa,” alisema Sitta ambaye alionekana kugadhabika.
Kwa mujibu wa Sitta, kamati ya uandishi iliomba siku moja zaidi ili
kukamilisha kazi yake na kwamba rasimu ya mwisho inayopendekezwa
itakabidhiwa Septemba 24 mwaka huu.
Septemba 25 wajumbe watakaa kwenye kamati kuona kama mapendekezo yao
yamewekwa ipasavyo kwenye rasimu hiyo na baada ya hapo Septemba 27 na
28, kamati ya uandishi itaiweka sawa rasimu hiyo ili Septemba 29 hadi
Oktoba 2 mwaka huu, ipigiwe kura.
Pia, Sitta alionekana kuwashawishi wajumbe hao, akiwataka kuipigia
kura ya ndiyo rasimu inayopendekezwa na Bunge ili wamalize kazi ya
kutunga Katiba na kuikabidhi kwa Rais Jakaya Kikwete ndani ya siku saba
baada ya Bunge kumaliza muda wake Oktoba 4.