jaridahuru

Mitandao

KATIBA: UKAWA YAIKALIA SERIKALI KOONI, YAAMUA KUANGALIA UWEZEKANO WA KUSITISHA MCHAKATO WA KATIBA



SERIKALI imeonesha dalili za kukata tamaa ya kuendelea na mchakato wa Katiba mpya kutokana na wajumbe wa kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kutolegeza msimamo wa kurejea bungeni, hatua inayozidisha ugumu wa upatikanaji wa theluthi mbili ya kura ya uamuzi.

Pamoja na kutambua ugumu huo, bado serikali imekubali kodi za wananchi ziendelee kutumika kulipa posho za wajumbe wanaoendelea na Bunge la Katiba, kwa maelezo kwamba iwapo watabaini kura hizo zitashindikana, itawalazimu kurudi katika Bunge la kawaida na kufanya mabadiliko katika baadhi ya vipengele vya muhimu.

Hatua hiyo ya kukata tamaa inaongeza ufa ndani ya serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM), na hivyo kufifisha kabisa ndoto na tambo za Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta anayelazimisha Bunge hilo liendelee kujadili rasimu kwa imani kwamba UKAWA watarejea na katiba mpya itapatikana.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema huku akionesha kutokakuwa na matumaini, alisema kuwa uwezekano wa kukosekana kwa Katiba mpya upo wazi iwapo UKAWA hawatarejea bungeni.

Jaji Werema alisema jambo hilo sio muhimu kuliweka wazi sasa kwa kuwa ndani ya kamati za Bunge Maalum zinazoendelea, idadi ya wajumbe inatimia.

“Kama tutashindwa kupata idadi ya wajumbe hao, huko mbeleni itatulazimu kurudi katika Bunge la kawaida na kufanya mabadiliko kwa mfano katika suala la muhimu kama Tume ya Uchaguzi, Mamlaka ya Rais, suala la mgombea binafsi na mengine,”alisema.

Alisema kuwa wanaendelea na shughuli la Bunge hilo kwa sasa kutokana na Rais Jakaya Kikwete kuwapa siku chache (60) na kugoma kuwaongezea, hivyo inawalazimu kukimbizana na muda huo.
Kuhusu UKAWA, Jaji Werema alisema kuwa amekuwa msuluhishi katika suala la maridhiano baina ya pande mbili zinazopingana kwa kipindi kirefu.

“Nimeshakutana na pande hizo na wengine ninawasiliana nao kwa njia tofauti nikiwaomba warejee bungeni…najua watatumia busara walizonazo na watarejea ili waendelee kuwasilisha mawazo ya wananchi katika maeneo mengine,”alisema.

Alisema kuwa suala la muundo wa serikali sio msingi wa katiba pekee pamoja na kuwa wamepingana katika s hilo. “Ni lazima UKAWA wakaelewa kuwa hakimu wa masuala yote wanayohitaji yawemo katika Katiba ni wananchi ambapo kama hawataki serikali mbili au tatu hao ndiyo watakaochuja,”alisema.

Jaji Werema alisema kuwa jambo hilo linapaswa kuepukwa na kulifanya la vyama kwani hata wale wajumbe wanaoendelea na vikao katika kamati kwa sasa wamekuwa na msimamo tofauti.

Kuvunjwa Bunge
Alisema kuwa kutokana na sheria ya mabadiliko ya katiba kutotoa mwanya kwa kiongozi yeyote hata Rais Kikwete kulivunja Bunge hilo, amezungumza na Rais Kikwete na kumemueleza kuwa hana mamlaka na ikiwa atatekeleza hilo basi atakuwa anaivunja Katiba ambayo aliipa kuilinda.

Werema alisema kuwa Bunge linaweza kusitishwa kama watakubaliana kufanya hivyo ili kufikia maridhiano lakini kwa sasa haoni haja ya kufanya hivyo kutokana na kukosekana kwa hoja za msingi.

“Kwa mfumo wa sheria ulivyo sasa, kinachoweza kufanya Bunge hilo kusimama ni pale baada ya kuundwa kwa Katiba itakayokuwa inapendekezwa na masharti yatakayotokana na masharti ya mpito, ndipo utaweza kulivunja lakini sio vinginevyo,” alisema.

Bunge la Katiba linaloendelea mjini Dodoma, limeendelea kupoteza uhalali wake kutokana na wajumbe wengi wakiwemo wa CCM kutorejea hadi sasa zikiwa takribani wiki mbili tangu lianze.
Hadi kufikia Ijumaa wiki hii, wajumbe waliokuwa wamefika na kujisajili ni 462 kati ya 628 wanaounda Bunge hilo. Kwa idadi hiyo ina maana wajumbe 166 hawajaripoti Dodoma.

Mgawanyo huo wa wajumbe 628 uko katika makundi matatu ya wabunge 346, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi 82 na kundi la 201. Na kwa mgawanyo wa nchi, Tanzania Bara ina wajumbe 416 wakati Zanzibar wako 212.

Related

Habari Mpya 8505337607439103029

Post a Comment

emo-but-icon

Wadhamini

UJUMBE

JH Katika Facebook

Nyayo zetu twitter

Za Juu

Mitandao

Piga Kura

Je ungependa Tanzania iwe na serikali ngapi?
  
pollcode.com free polls 

ADVERTISEMENTS

Msimamo wa ligi mbalimbali

Football results provided by whatsthescore.com

Mechi Live

Walioko Hewani Kwa Sasa

item