KATIBA MPYA: MTIKILA AKUSANYA SAINI KWA WANANCHI KUFUNGUA KESI YA KUSITISHA BUNGE LA KATIBA, ADAI HALINA TIJA
![](https://resources.blogblog.com/img/icon18_edit_allbkg.gif)
https://jaridahuru.blogspot.com/2014/08/katiba-mpya-mtikila-akusanya-saini-kwa.html
Dar/Arusha. Joto la kushinikiza kusitishwa kwa Bunge Maalumu la Katiba (BMK), linazidi kupanda nchini baada ya wabunge na vyama vya siasa kuendelea kusisitiza kuwa Bunge hilo halina tija kwa taifa.
Mwenyekiti wa Democratic Party (DP), Mchungaji
Christopher Mtikila amesema ameanza kukusanya saini za Watanzania
wanaopinga kuendelea kwa Bunge hilo ili kufungua kesi Mahakama Kuu ya
Tanzania, kusitisha vikao vinavyoendelea mjini Dodoma.
Mchungaji Mtikila akizungumza na Mwananchi
Jumapili alisema mchakato wa kukusanya saini hizo unaendelea katika
mikoa ya Arusha, Mwanza, Geita, Kagera, Dar es Salaam huku akibainisha
kwamba mwitio wa watu ni mzuri.
“Natafuta saini 20,000 za Watanzania na sasa
tayari tumekusanya saini zaidi ya 10,000 katika mikoa kadhaa na
natarajia Watanzania wataendelea kuniunga mkono ili kuhakikisha mchakato
huu. Nakwenda kuuzuia Mahakama Kuu na ninajua tu nitashinda,” alisema
Mchungaji Mtikila.
Alisema anakusanya saini hizo ili kudhihirisha
kuwa Watanganyika hawataki muungano, kwani mwaka jana Wazanzibari
walikusanya maoni 1,946 ya kupinga muungano.
Dk Chegeni
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Dk
Raphael Chegeni alisema kuendelea kwa Bunge hilo bila kuwepo kwa Ukawa
ni kuchezea fedha za umma.
Dk Chegeni alisema hayo jijini Arusha alipokuwa
akihudhuria vikao vya Bodi ya Wakurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya
Afya (NHIF), kwamba kuendelea na Bunge hilo ni kucheza kamari ya hatari
ambayo baadaye inaweza kusababisha malalamiko kwa wananchi na kuwagawa
wananchi.
“Sioni sababu ya haraka, huwezi kuandika katiba
bila ya maridhiano, haya mambo yenye utata itabidi yapatiwe muda mwafaka
na mchakato huu kuendelea baada ya uchaguzi mkuu mwakani.”
Dk Chegeni alisema, kwa kuwa kuna mahitaji ya
haraka yanayopaswa kuingizwa katika Katiba, ni busara Bunge la Novemba
kutumika kufanya mabadiliko hayo, ambayo ni pamoja na kuwa na Tume Huru
ya Uchaguzi, kuruhusu mgombea binafsi na pia kuingiza masuala ya haki za
binadamu kwenye Katiba.
Alisema hadhani kama kuna haraka sana wa kuandika
katiba wakati kuna kutoelewana, kwani Katiba inaweza kuandikwa hata na
utawala ujao, ingawa nia nzuri ya Rais Jakaya Kikwete ilikuwa ni
kuwaachia Watanzania Katiba Mpya.
Akizungumzia malumbano juu ya watu wanaotoa maoni
ya mchakato wa Katiba nje ya Bunge hilo, alisema wanapaswa kuachwa kwani
ni haki ya kila Mtanzania kutoa mchango wake ili kuwezesha kupatikana
Katiba mpya.