SIASA: SUMAYE MAKAMBA VITA KALI URAIS 2015, SUMAYE ASEMA HAKUNA KIJANA YEYOTE MWENYE SIFA KUWA RAIS

https://jaridahuru.blogspot.com/2014/07/siasa-sumaye-makamba-vita-kali-urais.html
WAZIRI Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye, amewashukia wale wanaotumia
kete ya umri kuwania urais na kwamba, hawafai kuwa viongozi wa taifa la
Tanzania.
Kauli hiyo, inaonekana ni kujibu mapigo ya Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba (40), ya kuwataka
wazee wakae pembeni na kuwachia vijana kuwania urais katika uchaguzi
mkuu ujao.
Sumaye, aliyasema hayo jana wakati akihojiwa na kituoa cha runinga cha Star cha jijini Mwanza jana.
“Nakumbuka mwaka 2005 wakati Rais Jakaya Kikwete hajawa Rais,
akigombea nafasi hiyo kulitawala msemo huo wa kumtaka kwa turufu ya
kusema ni kijana, huku wakati huo alikuwa na miaka 55, wengine tukawa
tunajiuliza hivi, kumbe mwenye miaka 55 ni kijana,” alihoji Sumaye.
Alibainisha kuwa, kwa kufuata misingi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),
hafikirii kama kuna kijana hata mmoja ambaye ana sifa ya kuwa Rais,
kwani chama hicho kinamtambua kijana ni yule mwenye miaka 18 hadi 35.
“Kwa misingi hiyo, sijajua kama kijana anayemaanishwa kwa sasa ni
huyo au mtu mzima ambaye hajazeeka, hivyo kwa maoni yangu kiongozi
anayetufaa ni mtu tunayemuona ana nguvu, muadilifu, mchapakazi na
anayetaka kutuongoza na sisi tunaona anatufaa, bila kujali kama ni
kijana,
mwanamke, mlemavu au ni wa dini gani, anatoka wapi, ili mradi ni
mtanzania, kwa dhamira ya wazi huyo atatusogeza mbele na ndiye
tutakayemtaka na si kwa sababu ya ujana au uzee wake,” alisema.
Sumaye, alimnukuu Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kuwa, aliwahi
kuzungumzia suala hilo wakati lilipojitokeza katika chaguzi zilizopita
akisema; “Ujana si sifa, nani hajawahi kuwa kijana?’.
Sumaye alisema, ujana ni hatua ya binadamu ya kukua na haiwezi kuwa sifa ya urais, kwani sifa ni tofauti na ujana.
“Simaanishi kwamba vijana hawafai kuwa viongozi, ila kama yupo
anayefikiria kwa maana anaitwa ‘fulani fulani’ anaona ana uwezo wa
kuendesha hii nchi na watu wakakubali kwamba anao uwezo, ni muadilifu,
anajua matatizo ya Watanzania na atasimamia maslahi ya umma,
tutamchagua, lakini asiende pale kwa kigezo cha kwamba yeye ni kijana,
kwa sababu hiyo si miongoni mwa sifa za uongozi na ukitaka uongozi kwa
misingi hiyo, utakuwa hutufai,” alisema Sumaye.
Akizungumzia kuhusu nafasi za uongozi kwa vijana, Sumaye alisema
kuwa, wapo wanaoshika nyadhifa mbalimbali ikiwamo bungeni, ukuu wa
wilaya na hata kwenye vyama, kuna timu ya vijana wengi, hivyo kama
wanania ya kubadilisha nchi wanaweza kubadili kwa kupitia nafasi hizo.
“Naamini vijana wengi hawakupewa uongozi serikalini, ukiachilia wale
wa nafasi za uwakilishi wa vijana wanaoingia bungeni kwa kufuata sheria
ya CCM, lakini kama mkuu wa Wilaya, Rais humteua kwa uwezo na si ujana
wake, kwa hiyo suala la ujana au uzee lisitupotezee muda, kwa sababu
lina nia ya kutuondoa kwenye ajenda bila sababu.
“Natoa wito kwa Watanzania tusiyumbishwe ili tuweze kumchagua Rais
tunayemtaka bila ya kujali sifa za ujana, udini na jinsia, kwani si moja
wapo ya sifa zinazotakiwa kwa rais anayetufaa,” alisema Sumaye.
Akifafanua madai kwamba wazee wamekuwa wakiwabana vijana kuchukua
nafasi za juu, Sumaye alisema, hilo halina ukweli kwa sababu katika
ngazi za Chama Cha Mapinduzi, zipo Jumuiya za Vijana ambazo zinatoa
nafasi pana kwa kuwapa uwakilishi.
“Naamini iwapo vijana wanataka kuleta mabadiliko, hakuna wa kuwazuia,
kwani tangu nimekuwa ndani ya chama hakuna hoja yoyote ya mabadiliko
iliyotolewa na vijana ikapingwa na wazee,” alisema.
Kauli hiyo ya Sumaye, imekuja baada ya hivi karibuni, January
kutangaza nia ya kuwania urais huku akitoa wito wa kuwataka wazee kukaa
pembeni ili vijana walete mabadiliko chanya ya uongozi.
January alisema kuwa, ameamua kwa asilimia 90 kujitokeza kuwania
urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na asilimia zilizobaki
zitategemea mambo mengine.
Katika ukurasa wake kwenye mitandao ya kijamii wa Facebook na
Twitter, January alisema, uongozi wa kizazi kipya upo tayari kushika
hatamu za uongozi na kuijenga Tanzania mpya, fikra mpya na maarifa
mapya.
Alisema, mabadiliko yaliyotokea Tanzania, yalidaiwa na kuongozwa na
vijana na kwamba, vijana nchini wanaweza kushika usukani wa kuleta
mabadiliko wanayoyataka.
“Ukiona kijana anamwambia kijana mwenzake hana uzoefu, basi kazi ya
kuleta mabadiliko ni kubwa zaidi na kutokuwa na uzoefu ni sifa ya
kijana,” aliandika.
Alisema kuwa, tusi kubwa kwa Rais wa Marekani, Barack Obama mwaka
2008, lilikuwa ni kukosa uzoefu na kukosa rekodi, lakini tusi hilo
liligeuka kuwa muziki kwa wapiga kura wa nchi hiyo.
“Tanzania mpya inahitaji viongozi wapya, mazoea mapya, fikra mpya na
maarifa mapya. Inahitaji kuthubutu mambo makubwa, siyo kulinda uzoefu wa
nyuma,” aliandika January.