jaridahuru

Mitandao

BUNGENI: UKAWA WAMLAMBISHA SITTA GARASA, WASISITIZA KUTOHUDHURIA KIKAO CHA USULUHISHI

 



KIKAO cha Kamati ya Mashauriano kinachotarajiwa kufanyika leo chini ya Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta, huenda kisifikie lengo lake la kutafuta suluhu ya kunusuru Bunge hilo liweze kuendelea Agosti 5, kutokana na wajumbe wa kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kushikilia msimamo wao wa kutohudhuria.

UKAWA wasipohudhuria kikao hicho, ni wazi mchakato wa kunusuru Bunge la Katiba utakuwa umegonga mwamba kwa mara nyingine, baada ya juhudi za Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi za kujaribu kuwakutanisha CCM na UKAWA nazo kutozaa matunda.

Sitta kwa kushirikiana na Makamu Mwenyekiti, Samia Hassan Suluhu, wameteua wajumbe 30 wa Bunge hilo kushiriki katika kikao cha Kamati ya Mashauriano kitafachofanyika leo na kesho katika ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam.

Wajumbe walioteuliwa katika kamati hiyo ni aliyekuwa Mwenyekiti wa muda wa Bunge hilo, Pandu Ameir Kificho, Profesa Costa Ricky Mahalu, James Mbatia, Freeman Mbowe, Ibrahim Lipumba, Peter Kuga Mziray, Vuai Ali Vuai, Askofu Donald Mtetemela, Sheikh Thabit Norman Jongo na Job Ndugai.

Wengine ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, Amon Mpanju, Dk. Francis Michael, Tundu Lissu, Margareth Abdallah, Kidawa Hamid Saleh, Shamsi Vuai Nahodha, Abubakar Khamis Bakari, Dk. Asha Rose Migiro, na Othman Masoud Othman.

Wapo pia Stephen Wasira, Hamad Rashid Mohamed, Askofu Amos Muhagachi, Susan Lyimo, Sheikh Hamid Masoud Jongo, Anne Kilango Malecela, Mary Pius Chatanda, Profesa Mark Mwandosya, Magdalena Sakaya na Khalifa Suleiman Khalifa.

Tangu Sitta alipotangaza kuunda kamati hiyo na kuwaita wajumbe hao kwa ajili ya kujadiliana kutafuta suluhu, wajumbe wa UKAWA wameapa kutoshiriki huku wakimtuhumu kwamba ndiye alishindwa kulimudu Bunge la Katiba na hivyo kuwa sababu ya wao kutoka nje. Msimamo wao ni kukutana na Rais Jakaya Kikwete wakidai kuwa ndiye aliyelikoroga, hivyo lazima alinywe.

Hadi jana jioni, baadhi ya wajumbe wa UKAWA waliozungumza na gazeti hili, walisisitiza kutohudhuria kikao hicho wakidai kuwa msimamo wao unaeleweka tangu awali, kwamba vinginevyo labda wapate maelekezo kutoka kwa viongozi wao.

“Juzi kikao chetu na Jaji Mutungi kilimalizika bila muafaka kutokana na CCM kuleta mapendekezo yasiyotekelezeka na ambayo kimsingi hayawezi kutuondoa katika hoja kuu… sasa tunaenda kufanya nini huko kwa Sitta?

“Isitoshe msimamo wa chama changu kupitia Kamati Kuu iliyokaa mwishoni mwa wiki iliyopita ni kutoudhuria kikao hicho cha Sitta kwa kuwa hakina hoja za msingi zaidi ya kwenda kutuvuruga,” alisema mmoja wa wajumbe kutoka CHADEMA.

Viongozi wakuu wa vyama vinavyounda UKAWA hawakupatikana jana kuthibitisha kama hawatashiriki kikao hicho au la kutokana na kile kilichoelezwa kwamba walikuwa na kikao cha faragha.

Tanzania Daima lilimtafuta Sitta kupata kauli yake kama amepata taarifa rasmi za wajumbe wa UKAWA kutohudhuria kikao chake, ambapo alisema kuwa hawana sababu ya msingi ya kutohudhuria.

“Kikao cha mashaurino kipo kama kilivyopangwa leo na kesho… naamini wajumbe wote wanayo taarifa ya kuhudhuria na sehemu kitapofanyikia, hivyo sidhani kama wajumbe wa UKAWA hawatahudhuria, hawana sababu ya kutohudhuria.

“Nafikiri kikao hicho kitakuwa na ajenda nyingi, waje watuambie yapi yaliyo magumu ama tulipokosea katika vikao vya Bunge vilivyopita ili tujirekebishe na kutovirudia katika vikao vijavyo,” alisema Sitta.

Katibu wa Bunge Maalum la Katiba, Yahya Khamis Hamad aliliambia gazeti hili kuwa maandalizi kwa ajili ya kikao hicho yamekamilika.

Alipoulizwa kama anazo taarifa zozote za kutohudhuria kwa wajumbe wa UKAWA, alisema hana.
“Kama kungekuwa na taarifa zozote za wajumbe wa UKAWA kutohudhuria ningekueleza, kwa maana tangu notisi ya siku 10 na barua itolewe kwa mjumbe mmoja mmoja ya kuhudhuria kikao, hakuna aliyefika kunijulisha kuwa hatahudhuria, hivyo sina taarifa,” alisema Hamad.

Chimbuko
Aprili 16 mwaka huu, wajumbe wa vyama vinavyounda UKAWA, walisusia kikao cha Bunge hilo kwa madai ya upendeleo na ubaguzi uliokuwa unafanywa na CCM dhidi yao, na kwamba wasingeweza kuvumilia matusi yaliyokuwa yakiporomoshwa kwa aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.

Wajumbe hao kutoka vyama vya CUF, CHADEMA, NCCR-Mageuzi na wa vyama vingine, walichukua hatua hiyo pia wakituhumu kauli ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, waliyodai kuwa ni ya ubaguzi na vitisho akiwa kanisani kwamba Wazanzibari wanaotaka serikali tatu wanataka Zanzibar ijitenge ili iwe nchi ya Kiislamu.
Pia UKAWA wanataka wajumbe wa Bunge hilo wajadili rasimu iliyowasilishwa na Tume ya Warioba badala ya waraka wa maelekezo kutoka CCM, unaoshinikiza muundo wa serikali mbili na kutupilia mbali mapendekezo ya wananchi ya serikali tatu.

Related

Habari Kuu 3897137256335652740

Post a Comment

emo-but-icon

Wadhamini

UJUMBE

JH Katika Facebook

Nyayo zetu twitter

Za Juu

Mitandao

Piga Kura

Je ungependa Tanzania iwe na serikali ngapi?
  
pollcode.com free polls 

ADVERTISEMENTS

Msimamo wa ligi mbalimbali

Football results provided by whatsthescore.com

Mechi Live

Walioko Hewani Kwa Sasa

item