jaridahuru

Mitandao

BUNGENI: JK AKWEPA LAWAMA BUNGE LA KATIBA, UKAWA WALEGEZA KAMBA, WAAHIDI KURUDI BUNGENI

 



LICHA ya hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge Maalum la Katiba kutajwa kama chanzo cha kuvurugika kwa bunge hilo, Rais Jakaya Kikwete amejivua lawama hizo, akidai wajumbe wa vyama vya CCM, Chedema, CUF na NCCR-Mageuzi ndio walichafua upepo.

Pia Rais Kikwete aliwatuhumu wajumbe Bunge hilo kutoka CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi ambao wanaunda kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), akisema hawatoi sababu ya kujisusia badala yake wanaweka msimamo wa kutorejea.

Pamoja na Rais Kikwete kuwataka wajumbe hao wafikie muafaka na wenzao wa CCM na kurejea bungeni, wao UKAWA wametoma masharti mazito wakitaka makubaliano hayo yawe kwa maandishi.

UKAWA walisusia Bunge la Katiba wakipinga hatua ya wajumbe wa CCM kuchakachua rasimu ya katiba na kuibadili kutoka mapendekezo ya serikali tatu kwenda mbili ambao ndiyo msimamo wa chama hicho.

Pia walisema kuwa hawako tayari kuendelea na Bunge ambalo limejaa matusi, kejeli na upotoshwaji wa rasimu halali iliyotokana na matakwa ya wananchi.

Akizungumza jana katika maadhimisho ya miaka 75 ya Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Rais Kikwete alisema kuwa hadi sasa hajapata kauli yoyote ya wajumbe wa UKAWA ya kutaka kurejea bungeni.

Alisema kuwa yeye na wenzake walibuni wazo na kuanzisha mchakato wa katiba mapya, ila anashangaa kuona ‘mapepo’ yameingilia na kuuvuruga.

Huku akionesha kukwepa lawama za hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge hilo iliyolalamikiwa kuwa ilijaa vitisho na ushabiki wa siasa za chama chake, Rais Kikwete alisema kuwa kazi yake kubwa ilikuwa ya kulizindua Bunge hilo baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kuwasilisha rasimu ya pili ya katiba.

“Mimi sihusiki na mvutano uliojitokeza. Kazi ya Tume ya Jaji Warioba ilikuwa ni kukusanya maoni ya wananchi, wajumbe wa Bunge la Katiba walitakiwa waanze kazi ya kuijadili rasimu ya pili baada ya kukamilisha uundwaji wa kanuni,” alisema.

Alifafanua kuwa wajumbe hao baada ya kukamilisha kanuni hizo ambapo waliunda kamati 12, walikubalinana waanze kujadili sura ya kwanza na ya sita, ambazo zinawasilisha nchi na muundo wa muungana.

“Mambo yote yalikwenda vizuri, lakini shida ilianza wakati wa kupiga kura, hapo ndipo vyama vinne ‘vingunge’ walipovurugana kwa kushambuliana kwa matusi, kejeli na maneno makali,”alisema.
Rais Kikwete alivitaka vyama hivyo kuona uwezekana kwa kukwamua mchakato huo, huku akipongeza juhudi alizodai zinafanywa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi za kuvikutanisha vyama hivyo.

“Mimi nawapongeza kwa kuwa wameanza kukutana, tuwaombee wamalize kazi yao kwa amani na utulivu na wakubaliane kurudi bungeni, naona kuna mapepo yanavuruga,” alisema.
Awali, Askofu Mkuu wa TAG, Dk. Barnabas Mtokambali, alimuomba Rais Kikwete kunusuru mchakato huo uliyokwama kwa kuukwamua haraka ili UKAWA warejee bungeni Agosti 5, mwaka huu.

Akizungumza na waumini wa kanisa hilo jijini Mbeya katika sherehe hizo za miaka 75, Dk. Mtokambali, alimuomba Rais Kikwete amalize ngwe yake kwa amani na utulivu.
Alisema kuwa licha ya kanisa hilo kumpongeza kwa kuwa kiongozi bora wa Afrika na kukaribia kumaliza ngwe yake, wanamuomba Mungu amalize muda wake kwa amani na utulivu na kukabidhi kijiti kwa rais ajaye.

“Rais, mchakato wa katiba umekwama, nakuomba uingilie kati uukwamue ili wajumbe wote warudi, kwa pamoja wazingatie sheria, kanuni na taratibu,”alisema.

UKAWA wajibu
Nao wajumbe wa UKAWA kupitia kwa Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe wamemjibu Rais Kikwete wakisema watakuwa radhi kurudi Bunge la Katiba endapo kutafanyika tathmini na tafakuri ya kina kubaini sababu za kuvurugika kwa bunge hilo na kuzitazama kanuni zinazolisimamia pamoja na sheria ya mabadiliko ya katiba.

Pia UKAWA wametaka pawepo na makubaliano ya maandishi kwamba hakutakuwa na kauli za matusi, kudharauliana wala kejeli, bali kitakachojadiliwa ni maoni ya wananchi yaliyomo kwenye rasimu.

Msimamo huo, ulitolewa juzi na Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, alipokuwa akizungumzia mchakato huo wilayani Hai mkoani Kilimanjaro baada ya UKAWA kuwa wameombwa na viongozi mbalimbali warudi bungeni.

Alisema kuwa viongozi mbalimbali akiwemo Rais Kikwete na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wamewaomba warudi kwenye bunge hilo, lakini wao wametoa masharti kwamba kufanyike vikao vya pamoja vya kutathmni hali iliyojitokeza awali, kisha wawekeane utaratibu wa kufuata kimaandishi.

“Uwendawazimu ni kufanya mambo yale yale kwa kutumia watu wale wale na utaratibu ule ule, halafu utegemee matokeo tofauti. Tumetoka kwenye Bunge la Katiba ambapo tumeona matusi, kejeli, dharau, ubaguzi wa hali ya juu na kupuuzwa kwa maoni ya wananchi, halafu mnatuita turudi kwenye Bunge lile lile tukatukanane kisha mtegemee kupata katiba bora,” alihoji Mbowe.

Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinznai Bungeni alisisitiza kuwa hata wakikubaliana wakarudi kisha matendo yale ya awali yakajitokeza ikiwemo kupuuza maoni ya wananchi, hawatasita kutoka tena kwa lengo la kupigania kupatikana kwa katiba bora yenye kuzingatia maslahi ya wananchi wote.

Mbowe alisema kuwa, wabunge wa CCM hawawezi kuhitimisha mchakato huo wakiwa peke yao, kwa kile alichoeleza kuwa, Katiba inatakiwa kuandaliwa na makundi yote ya jamii.

Chanzo: Magazeti | Tanzania Daima

Related

Habari Mpya 8070791165315791957

Post a Comment

emo-but-icon

Wadhamini

UJUMBE

JH Katika Facebook

Nyayo zetu twitter

Za Juu

Mitandao

Piga Kura

Je ungependa Tanzania iwe na serikali ngapi?
  
pollcode.com free polls 

ADVERTISEMENTS

Msimamo wa ligi mbalimbali

Football results provided by whatsthescore.com

Mechi Live

Walioko Hewani Kwa Sasa

item