TANZIA: MHADHIRI MKUU MWANDAMIZI WA CHUO CHA SAUT-MWZ, NKWAMBI NG'WANAKILALA AFARIKI DUNIA

https://jaridahuru.blogspot.com/2014/06/tanzia-mhadhiri-mkuu-mwandamizi-wa-chuo.html
Mwanza. Mhadhiri Mwandamizi Idara ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine Tanzania (Saut), Nkwabi Ng’wanakilala, amefariki dunia katika Hospitali ya Rufaa Bugando.
Akizungumza kwa simu kutoka Dar es Salaam jana,
Kaimu Makamu Mkuu wa Saut, Profesa Cassian Magori alisema nguli huyo wa
habari alifariki dunia usiku wa kuamkia jana.
“Ni kweli tumepokea taarifa za kushtusha leo
(jana) asubuhi kwamba mhadhiri wetu amefariki dunia. Sipo Mwanza hivi
sasa kutokana na kukabiliwa na shughuli za kikazi hapa Dar es Salaam,
lakini taratibu zote zinaendeshwa na Padri Peter Mwanjonde anayekaimu
nafasi yangu,” alisema Profesa Magori.
Naye Padri Mwanjonde alisema Ng’wanakilala ambaye
aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Redio Tanzania (RTD), alifanyiwa upasuaji,
lakini hali yake iliendelea kuwa mbaya na kuwekwa Chumba cha Uangalizi
Maalumu (ICU).
“Nafahamu Jumanne alifanyiwa upasuaji ingawa
hakupata nafuu, baadaye alihamishiwa ICU kwa bahati mbaya asubuhi hii
(jana) tumepokea taarifa za kifo chake,” alisema Padri Mwanjonde na
kuongeza: “Tayari tumeunda kamati itakayojulisha chanzo cha kifo hicho
baada ya kupata cheti, au kushauriana na madaktari waliokuwa
wakimhudumia.”
Hata hivyo, Padri Mwanjonde alisema ni mapema
kuzungumzia shughuli za mazishi, kwa sababu uongozi wa chuo lazima
kwanza ushauriane na familia.
Msemaji wa familia
Akizungumza nyumbani kwao Malimbe Nyegezi, Lugendo
Ng’wanakilala ambaye ni mtoto wa marehemu, alisema mwili wa marehemu
unatarajiwa kusafirishwa kesho kupelekwa Dar es Salaam kwa maziko.
Alibainisha kuwa baba yake alifariki kutokana na utumbo kujikunja na kufanyiwa upasuaji Bugando.
Mtoto huyo wa marehemu alisema kuwa baba yake
alizidiwa mwanzoni mwa wiki hii na kupelekwa hospitali ambapo baada ya
kufanyiwa uchunguzi, ilibainika utumbo ulikuwa umejikunja na kutakiwa
kufanyiwa upasuaji.
“Jumanne alifanyiwa operesheni baada ya hapo
akapelekwa Chumba cha Uangalizi Maalumu (ICU), alikuwa akisaidiwa na
mashine kupumulia,” alisema.
Ng’wanakilala alifafanua kuwa Jumatano waliondoa mashine na aliweza kujaribu kuzungumza ingawa kwa tabu.
“Ijumaa tuliandikiwa kwenda kununua dawa kutokana
aina hiyo kutokuwa hospitalini hapo, wakati tunajiandaa asubuhi leo
(jana) kununua dawa siku ya tukapigiwa simu na mama mdogo kuwa mzee
amefariki dunia,” alisema Ng’wanakilala
Ng’wanakilala alizaliwa 1949 Kata ya Buhongwa,
mkoani Mwanza na kupata elimu sehemu mbalimbali. Ameacha watoto 11;
Wavulana watano na wasichana sita. Naye Mkuu wa Idara ya Uandishi wa
Habari na Mawasiliano ya Umma Saut, Imane Duwe alisema pengo lililoachwa
halitazibika, kutokana na utendaji na umahiri wake kazini.
“Alikuwa mtu mahiri na mweledi wa kutosha, itachukua muda kumpata mtu kama huyu kwenye idara yetu,” alisema Duwe.
Ng’wanakilala amefanya kazi kwenye tasnia ya
habari akiwa mhadhiri, mtafiti, mshauri, mchapishaji binafsi na
mwandishi. Alijiunga Saut Idara ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya
Umma, akiwa Mhadhiri Mwandamizi tangu Septemba 1999.
Pia, alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Majaji ya
Tuzo ya Mwangosi, ambayo iliratibiwa na Muungano wa Vilabu vya Waandishi
wa Habari Tanzania (UTPC).