BNGENI: DR. KASHILILLAH AWASIHI WABUNGE WANAWAKE KUSHIRIKI KATIKA MAAMUZI MUHIMU
https://jaridahuru.blogspot.com/2014/07/bngeni-dr-kashilillah-awasihi-wabunge.html
Arusha. Wanawake barani Afrika wametakiwa kushiriki katika uamuzi ili kufikia malengo waliyoyakusudia.
Katibu wa Umoja wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola wa
Kanda ya Afrika (CPA), Dk Thomas Kashilillah aliyasema hayo jana
alipozungumza katika Kikao cha Kamati ya Wabunge Wanawake wa jumuiya
hiyo kilichojadili masuala mbalimbali ikiwamo kuwawezesha katika
uwakilishi.
Dk Kashilillah ambaye pia ni Katibu wa Bunge la
Tanzania alisema umefika wakati wanawake wa Afrika kushiriki katika
shughuli za kikanda ili kujijengea uwezo.
“Sasa ni wakati mwafaka kwa wanawake kwenye kanda
yetu kushiriki katika semina na makongamano mbalimbali yatayowajengea
uwezo zaidi katika shughuli zenu,”alisema Dk Kashilillah.
Aliwataka wanawake kuanzisha jukwaa lao
litakalowawezesha kujadili maslahi yao ambalo linaweza kuwakutanisha
mara mbili kwa mwaka ili kutimiza malengo hayo.
Mjumbe wa kamati hiyo kutoka hapa nchini, Anna
Abdallah alisema kupitia mipango ya aina hiyo ya uwezeshaji wanawake,
Tanzania imeweza kupiga hatua kubwa kwa kuwajengea wanawake uwezo wa
kuongoza na kuingia katika vyombo mbalimbali vya uamuzi.
Alisema Tanzania ni moja ya nchi zilizo na
uwakilishi wa kutosha wa wanawake katika ngazi za uongozi na ushiriki wa
nafasi walizonazo umekuwa na manufaa.