SIASA: MAKAMU MWENYEKITI CCM, PHILIP MANGULLA AIFAGILIA UKAWA. ASEMA UKAWA ITAWAPA NGUVU ZAIDI UPINZANI

https://jaridahuru.blogspot.com/2014/06/siasa-makamu-mwenyekiti-ccm-phili.html
Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula amevipongeza vyama vya upinzani kwa kuungana na kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) akisema hatua hiyo itawafanya kuwa na nguvu zaidi.
Katika kuonyesha kufurahishwa na hatua hiyo ya
upinzani, Mangula alihitimisha salamu zake wakati wa ufunguzi wa Mkutano
Mkuu wa sita wa CUF jana, kwa kusema: “Ukawa oyee,” na kuwafanya
wajumbe kumshangilia kwa nderemo na vifijo.
Mangula alisema umoja ni nguvu na utengano ni
udhaifu: “Ninawapongeza kwa kuungana na kuunda Ukawa, hata Mwalimu
Julius Nyerere aliwahi kusema angependa kitokee chama cha upinzani
chenye nguvu ambacho kinaweza kushindana na CCM ili kuwaletea wananchi
maendeleo.”
Msimamo
Wakizungumza katika mkutano huo viongozi wa Ukawa
walisisitiza kwamba hawatarejea katika Bunge Maalumu la Katiba hadi
yafanyike mabadiliko ya kujadili Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba
badala ya kujadili rasimu ya CCM.
Msimamo huo ulitolewa kwa nyakati tofauti na
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa Chadema,
Freeman Mbowe na Makamu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Leticia Mosole.
Akifungua mkutano huo, Profesa Lipumba alisema:
“Kamwe haturudi bungeni kujadili Rasimu ya Katiba ya CCM, bali tutarudi
kujadili Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji
Joseph Warioba, huo ndiyo msimamo wetu.
“Rais Jakaya Kikwete afahamu msimamo wetu mapema
ili aweze kuchukua hatua za kunusuru mchakato huu, yeye ndiye
atakayeamua kama turudi au tusirudi,” alisema huku akishangiliwa na
wajumbe ambao kila aliposema Ukawa… wajumbe waliitikia ‘tumaini letu’.
Katika salamu zake, Mbowe alimtaka Mangula
kumpelekea salamu Rais Kikwete kwamba Ukawa hawarudi katika Bunge
Maalumu la Katiba hadi madai yao yatimizwe.
“Kwa kuwa Mzee Mangula upo hapa leo tunakuomba
uwapelekee salamu wenzako, waeleze kwamba haturudi bungeni, waeleze
kwamba huo ndiyo msimamo wetu usioyumba,” alisema na kuongeza:
Mosole licha ya kuunga mkono hoja hiyo akisema
ndiyo msimamo wa chama chake, aliukosoa uchaguzi wa CUF: “Nimekuja hapa
lakini nashangazwa kwa nini hakuna wanawake wanaogombea nafasi za juu za
uongozi wakati wapo wenye uwezo, naomba mbadilike.”
Kupokezana vijiti
Wakati Profesa Lipumba na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif
Hamad wakitetea nafasi zao, Makamu Mwenyekiti wa CUF, Machano Hamis Ali
alitangaza kuachia ngazi akisema uongozi ni kama mchezo wa kupokezana
vijiti.
“Sijachukua fomu za kugombea nafasi yoyote kwa
sababu ya afya yangu siyo nzuri, pia nafahamu kwamba uongozi ni
kupokezana vijiti.”