MICHEZO: WACHEZAJI BORA 32 WANAOTARAJIWA KUNG'AA NA KUZIPAISHA TIMU ZAO KATIKA KOMBE LA DUNIA 2014

https://jaridahuru.blogspot.com/2014/06/michezo-wachezaji-bora-32-wanaotarajiwa.html
Kombe la Dunia ni uwanja mpana. Ni mahali ambapo vipaji na vipaji vya
wanasoka duniani huonekana. Madalali wa kuvumbua na kununua wachezaji
[scouts] hufurika kwenye mashindano kama haya wakijua wazi kabisa kwamba
pale ndipo watakapoona “lulu” kwa ajili ya vilabu vyao. Kwa maana hiyo
kuna kila aina ya harakati za kimichezo na kuonyesha na kuonyeshana
vipaji.
Hii sio kumaanisha kwamba wachezaji wote mahiri hapa duniani
walicheza katika fainali za Kombe la Dunia.La. Wapo wasakata kabumbu
kadhaa ambao hawakuwahi kugusa fainali hizi.Mfano ni George Opong Weah
na watu kama kina George West nk.
Lakini wakati wengine wakionyesha vipaji ili wang’amuliwe na
kubadilisha maisha yao ya kisoka,wapo wale ambao wanashuka dimbani
tayari wakiwa na majina [superstars] na ambao dunia tayari inakuwa
ikiwaangalia kwa makini kutaka kujua na kuona kile watakachokifanya.
Kila timu huwa na mchezaji ambaye hutizamwa zaidi. Kwa umombo unaweza
kumuita Key Player. Kila timu,kwa kupenda au kutopenda,huwa ina star
player. Hii haimanishi kwamba katika timu hakuna wachezaji wengine wenye
majina au wanaoweza pia kuwa stars.La. Ni sheria ya mmoja mmoja
inayozingatiwa hapa.
Kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali wa soka,wachezaji hawa 32 [mmoja
kutoka katika kila timu inayoshiriki fainali za Kombe la Dunia mwaka
huu] ndio watarajiwa kuchomoza zaidi huko Brazil. Mpangilio huu hapa ni
kutokana na makundi ya FIFA World Cup 2014.
NB: Orodha hii inaweza kubadilika kwani imeandikwa kabla timu
zote hazijathibitisha wachezaji wake 23 iliyowachagua mwisho. Wengine
wanaweza kuumia katika siku hizi za mwisho na hivyo kutokwenda
Brazil.Zingatia.
Hakuna ubishi kwamba Neymar anayechezea
soka la kulipwa Barcelona nchini Spain ndio gumzo kubwa kwa timu ya
Brazil. Anatarajiwa kuongoza mashambulizi ya The Kings Of Samba[Brazil]
Ingawa wachezaji wengine wa Mexico kama Chicharito na Giovani dos
Santos wanatajwa kama ma-star,Oribe Peralta ambaye anacheza katika ligi
ya nyumbani katika club ya Santos Laguna, ndiye anaaminika hivi sasa
kuwa star zaidi
Hakuna shaka kwamba Luka Modric ndiye mchezaji star zaidi hivi sasa
katika timu ya Croatia. Kiungo huyu ambaye hivi sasa anachezea timu ya
Real Madrid nchini Spain ameonekana wazi kuwa tegemeo sio tu katika club
bali nchi yake Croatia.
Ingawa ungetegemea mchezaji kama Samuel
E’too kuendelea kuwa star na tegemeo zaidi katika timu ya Cameroon,
golikipa Charles Itandje ndio tegemeo na ambaye wengi watapenda kumuona
akiokoa mikwaji. Charles ambaye anachezea timu ya Konyaspor nchini
Uturuki[kwa mkopo kutoka PAOK FC ya Ugiriki] aling’ara vilivyo katika
mchezo dhidi ya Tunisia wakati wa kuwania nafasi ya kwenda Brazil.Google
utaona alichofanya.
Ingawa bado kuna utata kuhusu hali yake
na kama atakuwa fit kabla ya kuanza kwa fainali za Kombe la Dunia huko
Brazil,Diego Costa mshambuliaji mahiri wa timu ya Atletico Madrid
anatarajiwa kuwa nyota wa Spain. Lakini pia huenda akawa ndiye mchezaji
atakayezomewa zaidi huko Brazil kwani Diego ni mzaliwa wa Brazil na
angeweza kabisa kuchezea Brazil mwaka huu kama asingeamua kuchezea
Spain[pia ni raia wa Spain].Wabrazil hawajaipenda hiyo.
Robben,mshambuliaji mahiri ambaye hivi
sasa anaendelea kuwika na timu ya Bayern Munich nchini Ujerumani,ndiye
mchezaji ambaye ni star zaidi na ambaye ameonyesha kuwa na kile kiwango
kinachoitwa “cha dunia”. Ana miaka 30 hivi sasa.
Arturo ambaye anachezea club ya Juventus
nchini Italia ni mchezaji “kiraka” wa Chile ambaye endapo Chile
itaushangaza ulimwengu wa soka huko Brazil,bila shaka mchango wake
utakuwa mkubwa.
Tim Cahill-Australia
Tim Cahill anayechezea timu ya New York
Red Bulls katika ligi ya soka ya Marekani na Canada[Thiery Henry
alipitia hapo baada ya Ulaya] ndiye nyota kwa upande wa Australia.
Kwa upande wa Colombia Ramadel Falcao,
ndio mchezaji nyota zaidi.Lakini kuna kila aina ya dalili kwamba mwaka
huu hatoweza kucheza kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya goti.Hapo
ndipo James Rodriguez anapochukua nafasi. Rodriguez au Hames kama
anavyoitwa na mashabiki wa soka huko Colombia, anachezea AS Monaco ya
Ufaransa.
Kama yupo mchezaji kutoka barani
Afrika[bila kujali timu] ambaye sio tu anapendwa na mashabiki wengi
barani Afrika hivi na ambaye yupo kwenye kiwango cha juu,basi bila shaka
ni Yaya Toure. Hata wachezaji wenzake wa Ivory Coast kama vile mkongwe
Didier Drogba,wote wanamtaja Yaya kuwa kiongozi na mhimili wa timu yao.
Yaya anachezea mabingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza, EPL Champions,
Manchester City
Ingawa mashabiki wa Ligi Kuu ya Uingereza
bado hawajapata nafasi ya kuona vizuri makeke ya Kostas ambaye anacheza
katika klabu ya Fulham, ni wazi kwamba yeye ndio tegemeo kubwa la timu
ya Ugiriki katika mashindano ya mwaka huu.
Ingawa Japan wanao mastar wengine kama
vile Shinji Kagawa anayechezea Manchester United,hakuna ubishi kwamba
Keisuke Honda ndiye mhimili mkuu kwa sasa. Anachezea AC Milan nchini
Italy.
Ingawa msimu wa ligi kwa upande wa timu
yake ya Manchester United haukuwa wa kuvutia sana, Wayne Rooney au
ukipenda unaweza kumuita Wazza anabakia kuwa miongoni mwa wachezaji
tegemeo zaidi kwa upande wa timu ya taifa ya Uingereza. Hana historia
nzuri sana na mashindano ya Kombe La Dunia lakini endapo kelele za
waingereza[na wana kelele kweli] zitakuwepo,basi Wazza anaweza kuwa
chanzo.
Miaka kadhaa iliyopita[na hata hivi sasa
miongoni mwa watu] ni vigumu kuamini kwamba mtu mweusi ndio key player
kwa timu ya taifa ya Italy. Muda umebadilika na mchezaji huyu mwenye
mbwembwe,hasira na kila aina ya vituko ndiye ataangaliwa zaidi pindi
timu yake ya Azzurii itakapoteremka dimbani huko Brazil.
Kama ilivyo kwa Balotelli hapo juu,Luis
Suarez ni mchezaji mwingine ambaye ana kila aina ya vioja. Pamoja na
hayo ni mfungaji hodari na ndio tegemeo kubwa la Uruguay huko Brazil.Kwa
bahati nzuri au mbaya,Uruguay wapo kundi moja England na hivyo lazima
watapimana joto. Upinzani kutoka Liverpool utaendelea?Tutaona.
Sio mara nyingi sana kuwemo kwenye Kombe
la Dunia na kisha kutamba kwamba mchezaji wenu mhimili ni kipa.Costa
Rica wao wanaweza kusema hivyo kwani Keylor Navas anayechezea timu ya
Levante nchini Spain ndio mhimili na ambaye anategemewa kulinda mlango
na kuongoza wenzake.
Ukisema Franck Ribery wa Bayern Munich
basi bila shaka itabidi pia useme Franck Ribery wa Ufaransa. Ndio
tegemeo. Mwaka huu alikuwepo katika wachezaji watatu wa juu waliokuwa
wanawania tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa FIFA.
Endapo Switzerland itakuwa na mafanikio
makubwa huko Brazil,basi Xherdan ndio atakuwa mpishi mkuu.Anachezea
Bayern Munich pembeni ya Ribery na Arjen Robben.
Winga huyu ambaye anachezea Manchester
United ndio tegemeo kubwa la Equador katika mashindano ya mwaka
huu.Wenzake wanamuita “kiongozi”.
Emilio anachezea Celtic FC kule Uskochi.
Kwa upande wa Honduras ndiye tegemeo kubwa hususani kwa upande wa ulinzi
na kusukuma mbele mashambulizi.
Hakuna ubishi kwamba Messi ni miongoni
mwa wachezaji mahiri kabisa waliowahi kuucheza mchezo wa soka hapa
duniani.Hata hivyo, ana kasoro moja kwa mujibu wa wachambuzi wa soka na
hususani wasiompenda;hajawahi kushinda Kombe La Dunia. Kwa maana
hiyo,kama unadhani Neymar wa Brazil ana presha ya kuipa Brazil
kombe,Messi pia anayo na zaidi.Argentina na ulimwengu
unasubiri…ataiwezesha kushinda Kombe La Dunia mwaka huu?
Bosnia & Herzegovina ni wageni katika
fainali za Kombe La Dunia.Hii ndio mara yao ya kwanza. Pamoja na
hayo,wanaye Edin Dzeko mshambuliaji anayechezea mabingwa wa
Uingereza,Manchester City. Ndiye atagemewa kuwaongoza wenzake kufanya
“muujiza” huko Brazil.
Iran wanasema hawaendi Brazil
“kutalii”.Bila shaka wanasema hivyo wakiangalia wachezaji wao kama
Ashkan Dejagah ambaye anacheza soka ya kulipwa nchini Uingereza. Huyu
bwana anao pia uraia wa Ujerumani na alipokuwa mdogo aliwahi kuchezea
timu ya vijana ya Ujerumani akiwa na Mesut Ozil.
Ingawa ligi anayochezea[Uturuki] haina
umaarufu sana, hakuna ambaye anatilia shaka uwezo wa Emmanuel Emenike
katika soka. Ni mshambuliaji mahiri na makini. Anatarajiwa kuongoza
mashambulizi ya Nigeria[Super Eagles] timu ambayo inatarajiwa kufanya
vizuri huko Brazil.
Phillip Lahm-Germany
Miongoni mwa wachezaji wa timu ya
Ujerumani ambao ni vigumu sana kwa kocha wa Ujerumani,Joachim Low,
kupata mtu wa kuziba pengo lake[endapo itatokea akaumia au vinginevyo]
ni Kapteni Phillip Lahm. Mchezaji huyu ambaye anachezea Bayern Munich ni
muhimu na ndiye anaongoza Ujerumani huko Brazil ikitarajiwa kwamba
mwaka huu watafanya vyema zaidi.
Ghana au Black Star ni miongoni mwa timu
kutoka Africa ambazo zinatarajiwa kufanya vyema nchini Brazil. Kama
utakumbuka,Ghana katika fainali za Afrika Kusini mwaka 2010 walibakia
almanusura kutoboa na kufika nusu fainali. Majeed Waris anayechezea soka
la kulipwa FC Valenticiennes huko Ufaransa anajua vyema wakati gani
apige,akimbie nk.Ni mchezaji ambaye anatarajiwa kuipa forwardline ya
Ghana uhai mkubwa na kushirikiana vyema na Asamoah Gyan.
Hakuna ubishi kwamba mchezaji wa US
ambaye alikuwa anatizamwa na wengi kuongoza timu ya nchi hiyo ni London
Donovan. Kwa bahati mbaya kocha mjerumani Jurgen Klinsman, hakuona
hivyo. Donovan katemwa. Badala yake mchezaji Clint Dempsey ndiye ambaye
anatarajiwa kuongoza jahali za USA.
Hivi sasa ndiye anashikilia taji la FIFA
La Mchezaji Bora wa Dunia. Timu anayochezea,Real Madrid ndio mabingwa wa
Ulaya na yeye akiwa na rekodi ya magoli 17 ya Ligi ya Mabingwa. Hakuna
ubishi kwamba Portugal wanakwenda Brazil kutokana na mchango wake mkubwa
hususani katika ile mechi iliyowaweka pembeni Sweden. Ronaldo au CR7
ndiye mhimili mkubwa wa Ureno.
Swahiba wangu wa karibu,Esmail
Manambi,majuzi alinikumbusha kwamba Ubelgiji,ingawa sio miongoni mwa
timu zinazotajwa sana linapozungumziwa suala la Ubingwa wa Dunia,
wanaweza kuushangaza ulimwengu. Nakubaliana naye kabisa. Ubelgiji ya
mwaka huu imejaa wachezaji wenye vipaji na majina. Kuna kila
Kompany,Lukaku,Fellaini nk. Wote,hata hivyo,wanaangalia zaidi kwa Eden
Hazard ambaye mwaka jana Chelsea walikohoa paundi Milioni 32 kumnunua.
Kama utakumbuka wakati wa fainali za
South Africa kocha wa Uingereza wakati huo,Fabio Capello kidogo apate
wazimu.Ule utulivu wake uliisha ghafla. Wanasema kelele za Vuvuzela
zilizingua sana. Hivi sasa Capello ndio kocha wa Urusi. Na kama kuna
mchezaji ambaye anaweza kusaidia kutorudisha ule mzimu wa Capello South
Africa basi mchezaji huyo ni Roman Shirokov anayechezea Krasnodar.Ndiye
Kapteni wa Urusi.
Ingawa Korea Kusini inapewa nafasi ndogo
zaidi kunako Ubelgiji na Urusi katika kundi lao, endapo watasonga mbele
basi bila shaka mchango wa Ki Sung Yueng anayechezea Sunderland kwa
mkopo kutoka Swansea,hautokuwa mdogo.Ndiye tegemeo kubwa la Korea ya
Kusini.
Algeria ni timu nyingine kutoka Afrika
mwaka huu.Nchi hii ina uzoefu zaidi wa Kombe la Dunia. Kapteni wao
Madjid Bougherra anayecheza soka lake la kulipwa nchini Qatar na timu ya
Lekhwiya, ndiye anayetarajiwa kuongoza jahazi.Ameshachezea nchi yake
katika zaidi ya mechi 60.