JAMII: MAMA WA MSICHANA WA KAZI ALIYECHOMWA NA PASI APIGA YOWE WODINI NA KUSIMAMISHA HUDUMA, ADAI MWANAWE

Kelele za vilio jana zilisimamishwa kwa muda shughuli katika Wodi ya Wanawake ya Hospitali ya Mwananyamala, Dar es Salaam baada ya mama mzazi wa msichana, Yusta Lucas (20) anayedaiwa kuteswa kwa kung’atwa na kuchomwa kwa pasi mwili mzima kumwona mwanawe kwa mara ya kwanza.
Zilikuwa dakika 10 ngumu kwa mama huyo, Modesta Simon kuamini hali aliyomkuta mwanaye aliyelazwa hospitali hapo kuuguza majeraha kutokana na kufanyiwa ukatili na tajiri yake Amina Maige.
Akizungumza huku akitokwa na machozi, Modesta alisema: “Jamani Amina kweli amekufanya hivi, kila nikiuliza wananiambia hujambo kumbe umeharibika hivi…”
Alisema habari za mateso na kulazwa kwa mwanaye alizipata kutoka kwa ndugu yake anayeishi Arusha…
“Alhamisi nilipata simu kutoa kwa ndugu yangu Marieta Shitindi yeye anakaa Arusha, akaniambia ameona kwenye runinga kwamba Yusta amelazwa baada ya kupigwa na Amina ndipo nikafunga safari kutoka Tabora kuja kuhakikisha.Amina ni mtoto wa mjomba wangu kabisa na sikuwahi kuambiwa chochote, niliamini wanaishi vizuri na sikudhani kama anaweza kulifanya jambo hili.”
Modesta alisema awali alikuwa na mawasiliano na mwanaye kupitia simu ya mama yake Amina ambaye wanaishi karibu, lakini hivi karibuni alianza kupata wasiwasi baada ya kila alipohitaji kuongea naye alipatiwa sababu hivyo akaomba Yusta kurudishwa na aliahidiwa angepelekwa mwezi huu.
“Aliniahidi mwezi huu atamleta Yusta nyumbani alisema anataka muda amnunulie na cherehani ili akija apate shughuli ya kufanya…” alisema.
Ofisa Muuguzi katika wodi aliyolazwa Yusta, Erica Massawe alisema hali ya binti huyo imeimarika na alisharuhusiwa kutoka tangu Ijumaa iliyopita na kwamba wanasubiri maelekezo ya Polisi na Ustawi wa Jamii kwani ndiyo wahusika wakuu.